Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha ACT Wazalendo, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema wataendelea kusimamia ufuatwaji wa sheria na kanuni zilizowekwa nchini kwa lengo la kufikia maendeleo ya Tanzania.

Akizungumza na viongozi pamoja na wanachama wa ACT Wazalendo katika kikao cha ndani huko Masai Camp Mbagala Kuu jijini Dar es salaam, Mheshimiwa  Othman amesema Tanzania ni nchi yenye utajiri mkubwa kuliko nchi nyingi za Afrika ambao umekuwa hauonyeshi faida yake kutokana na uwepo wa baadhi ya viongozi wenye changamoto za kutokuwa na misingi bora ya uwajibikaji, hivyo basi juhudi za pekee zinahitajika ili kuona utajiri huo unawanufaisha Watanzania wote. 

Mheshimiwa Othman aliwahimiza wanachama wa ACT Wazalendo kuendelea kuungana pamoja na kuhakikisha wanafuata kanuni zilizopo katika chama hicho ili lengo la  kuinyanyua Tanzania kimaendeleo lifikiwe.  

"Mambo hayawezi kuwa sawa kwa kuunga mkono juhudi, bali yatakaa sawa kwa kutenda juhudi ili kuleta maendeleo nchini, " alinasihi Mhe.Othman juu ya wanachama wanaohama hama vyama vyao vya siasa kwa maslahi binafsi.

Sambamba na hayo Makamu huyo wa Kwanza wa Rais alisema kwamba ili kupata maendeleo endelevu nchini basi ni vyema haki, amani na usawa vizingatiwe hususani katika nyakati za uchaguzi. Aliongeza kuwa uchaguzi huru na wahaki ni muhimu sana ili kuwapata viongozi ambao ni chaguo la wananchi wenyewe.

Pamoja na hayo Mhe. Othman alisisitiza umuhimu wa kuwa na katiba mpya ili kuifanya nchi kuendana na wakati.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa Ndg. Doroth Semu amesema chama hicho kinaamini kwenye demokrasia, maelewano na mshikamano katika kutimiza dhamira yake, hivyo wataendelea kumuunga mkono Mhe. Othman pamoja na mawaziri waliomo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, GNU, kwa lengo la kuona chama hicho kinafanya vizuri kwa upande wa Zanzibar.

Akifungua mkutano huo Mwenyekiti wa ACT Wazalendo mkoa wa Dar es salaam Ndg. Salum Rajab Sudi alisema kuwa mkoa huo umeandaa mikakati mbali mbali yenye lengo la kuhakikisha kuwa chama hicho kinachukuwa nafasi katika eneo hilo hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi wa marudio wa kata unaotarajiwa kufanyika katika kata ya mbagala kuu.

Kabla ya kikao hicho, Mhe. Othman alipata fursa ya kuwajulia hali wagonjwa na wenye matatizo mbali mbali katika maeneo kadhaa ya Mbagala.





 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...