Charles James, Michuzi TV

WADAU wa zao la Kahawa wametakiwa kutumia uzoefu wao na weledi katika kuhakikisha kuwa sekta ya Kahawa inabadilika kwa kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa zao hilo.

Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba wakati akifungua Mkutano wa 11 wa wadau wa kahawa jijini Dodoma ambapo amesema wana jukumu kubwa la kuhakikisha zao hilo linakua.

RC Mgumba amesema zao la kahawa ni mojawapo ya mazao ya kimkakati yaliyochaguliwa na Serikali hivyo yanapaswa kubadilika na kukua ili yaweze kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Nchi sambamba na kuwa mwarobaini wa ajira kwa vijana.

Amesema kwa sasa uzalishaji wa zao hilo Siyo mzuri hivyo wadau hao wanapaswa kutumia kongamano hilo ili liweze kuwasaidia kujadili changamoto zinazolikabili zao hilo na kutoka na mawazo ya pamoja ya namna gani wanaweza kulikuza na kuwa msaada kwa Taifa.

" Kahawa nayo ni mojawapo ya mazao ya kimkakati kwa Nchi yetu, linatakiwa kukua na kutoa mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wetu, kama tutatumia mkutano huu vizuri kupata majibu ya changamoto zinazolikabili zao hili basi naamini tunaweza kuifanya Kahawa kuwa mojawapo ya kilimo kitakachoajiri kundi kubwa la vijana.

Tutumie kongamano hili kila mmoja kwa uwezo, taaluma na uzoefu wake kujadiliana kwa pamoja kutatua changamoto hii ya uzalishaji mdogo hata kule kwangu Songwe uzalishaji umeshuka siyo kama zamani," Amesema Mgumba.

RC Mgumba ametaja changamoto zinazoikabili sekta ya kahawa kuwa ni pamoja na tija ndogo, uzalishaji mdogo, kuyumba kwa bei ya kahawa katika soko la Taifa, ukosefu wa mitaji kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kushindwa kukopesheka kwenye taasisi za fedha ambayo yote yanalifanya zao hilo kuonekana halilipi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Nchini, Prof Aurelia Kamuzora amezungumzia umuhimu wa zao hilo huku akisema limemsaidia yeye binafsi kwenye maisha yake na kutoa rai kwa wadau wa kahawa kuungana kwa pamoja kukuza kilimo hiko.

Mkutano huo wa 11 wa wadau wa kahawa unafanyika kwa siku mbili jijini Dodoma ambapo unawakutanisha wadau wa kahawa kutoka maeneo tofauti ambapo linakwenda sambamba na kauli mbiu isemayo " Uzalishaji wenye tija ndio nguzo ya maendeleo ya sekta ya kahawa"

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba akizungumza wakati akizindua mkutano wa 11 wa wadau wa Kahawa Nchini jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Nchini, Prof Aurelia Kamuzora akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa 11 wa wadau wa kahawa Nchini unaofanyika jijini Dodoma.
Wadau wa zao la kahawa wakimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Nchini, Prof Aurelia Kamuzora akizungumza kwenye ufunguzi wa kongamano la wadau wa zao hilo unaoendelea jijini Dodoma.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...