Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt John Jingu wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa Maadhimisho ya siku ya wajane duniani ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo June 23, kila mwaka.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Wajane duniani yaliyofanyika Mkoani Dar es Salaam leo Juni 23,2021 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt John Jingu.
Wakili wa serikali kutoka RITA, Edna Kamala akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Wajane duniani yaliyofanyika Mkoani Dar es Salaam leo Juni 23,2021 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Maafisa RITA wakitoa huduma kwa wajane waliofika katika viwanja vya Mnazi Mmoja wakati wa kusheherekea siku ya wajane duniani ambayo ufanyika kila Juni 23 kila Mwaka.
Picha na Emmanuel Massaka, Michuzi TV

Na Avila Kakingo, Globu ya Jamii
TAKWIMU zinaonyesha kuwa idadi ya wajane Duniani ni takriban milioni 258 kati ya hao, wajane 115 milioni wanadhulumiwa, wanafanyiwa ukatili, wanakabiliwa na umasikini na kutengwa na jamii na mmoja kati ya wajane 10 anaishi katika umasikini uliokithiri.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis wakati akizungumza wakati wa Maadhimisho ya siku ya Wajane Duniani iliyofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Mkoani Dar es Salaam leo Juni 23,2021.

Amesema kuwa hapa nchini wajane wanakadiliwa kuwa laki 8.8 ambayo ni sawa na asilimia 3.1 ya wanawake wote nchini ambao wanakadiriwa kuwa milioni 28.5 kwa mwaka 2020.

"Katika baadhi ya jamii, hadhi ya mwanamke inahusishwa zaidi na maisha yake na mumewe, na hivyo mume anapofariki, mwanamke anakuwa hana nafasi yoyote kwenye jamii. Wengine hutakiwa kuolewa na ndugu wa mume bila ridhaa zao. Na huo ni mwanzo tu wa baadhi ya kero zinazo wakabili wajane." Amesema Mwanaidi

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inawatambua na kuwaenzi wajane katika jamii ikiwajuhudi mbalimbali zimefanywa na Serikali ikiwa ni pamoja na Kuitambua Siku ya Wajane kitaifa na kuhamasisha wadau wote kuiadhimisha na hivyo kuweza kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wajane.

Aidha amesema kuwa jumla ya kodi, ada na tozo 108 kati ya 139 zimefutwa ili kupunguza kero kwa wanawake wajasiriamali wakiwemo wajane ili kuondoa kero kwa wajasiriamali wakiwemo Wajane, mama lishe na wauza mbogamboga kwa kupatiwa maeneo rasmi ya kufanyia biashara yenye ukubwa wa hekta 15,822.64 katika Halmashauri 150 nchini.

Hata hivyo amesema kuwa serikali itaweka na kuimarisha mifumo ya kulinda haki za Wanawake wakiwemo Wajane kwa Kuanzisha madawati ya jinsia na watoto 427 katika vituo vya polisi na vituo 153 katika Jeshi la Magereza kwa lengo la kutokomeza ukatili wa Kijinsia kwa Wahanga wakiwemo Wajane.

Pia serikali itaongeza huduma za msaada wa sheria kutokana na kutungwa kwa Sheria ya Msaada wa Kisheria Na. 1 ya mwaka 2017, ambayo imewezesha makundi maalum ikiwemo Wajane na watoto kupata haki zao katika vyombo vya usimamizi wa sheria. Aidha, taasisi 125 za kutoa huduma za msaada wa kisheria zimetambuliwa na Wasaidizi wa Kisheria 3,721 wamesajiliwa kote nchini.

Serikali inawawezesha Wanawake kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu ili kuwapa fursa Wanawake Wajasiriamali wakiwemo Wajane kupatiwa mikopo hiyo inayotolewa na Halmashauri, mikopo hiyo ya asilimia 4 kwa Wanawake, 4 kwa Vijana na 2 kwa walemavu hutolewa iwapo walengwa watakuwa wamekidhi vigezo vinavyotolewa katika hamashauri ikiwa ni pamoja na kuunda kikundi cha wanawake kuanzia watano hadi 10, wawe na umri isiozidi miaka 18 na kuendelea pamoja na kutimiza vigezo vingine vinavyohitajika.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt John Jingu amewaasa wajane na jamii kwa ujumla kuchukua tahadhari juu ya Ugonjwa wa COVID-19 kwa ugonjwa huo ni hatari sana kwa jamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Widows Association (TAWIA), Rose Sterwart amesema kuwa wajane ni kundi maalumu na maadhimisho yaliyofanyika leo ni kwaajili ya kutafakari changamoto zinazowakabiri wanawake hasa wajane.

Hata hivyo amewaasa wajane kutokukaa na changamoto zinazowakabiri na kuibua vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na wanadugu mara baada ya mume au kufariki dunia.

Licha ya hayo ameiomba serikali kufanya mabadiliko ya Sheria na sera zinazohusiana na kulinda haki za wajane kwa jamii nzima.

Tanzania huadhimisha Siku ya Wajane kwa lengo la kujenga hamasa, mshikamano na uelewa ndani ya Jamii kuhusu haki na Ustawi wa Wajane, maadhimisho yamwaka huu yanatoa fursa ya pamoja katika kubaini changamoto za wajane na namna ya kukabiliana nazo.

Mwaka huu Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani yameongozwa na Kaulimbiu “Mapambano Dhidi ya COVID-19, Wajane Washiriki Kikamilifu.”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...