Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani akionesha kifaa cha UMETA kwa wananchi wa kitongoji cha Mtakuja, kijiji cha Kibumba, Kata ya Makurugusi, wilaya ya Chato, tarehe 13 Juni, 2021 alipofanya ziara kukagua na kuwasha umeme rasmi kwenye kitongoji hicho.
Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani akikabidhi kifaa cha UMETA kwa familia mbili za wanakijiji cha kitongoji cha Mtakuja, kijiji cha Kibumba, Kata ya Makurugusi, wilaya ya Chato, tarehe 13 Juni, 2021 alipofanya ziara kukagua na  kuwasha umeme rasmi kwenye kitongoji hicho.
Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wanakitongoji cha Mtakuja, kijiji cha Kibumba tarehe 13 Juni, 2021 alipofanya ziara kukagua na kuwasha umeme rasmi kwenye kitongoji hicho kilichopo katika kata ya Makurugusi Wilayani Chato.


Ø * Awasha umeme rasmi kwenye kitongoji cha Mtakuja, kijiji cha Kibumba

Na. Dorina G. Makaya - Chato

WAZIRI wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani, amewahimiza wananchi wenye nyumba ndogo isiyozidi vyumba vitatu ambao kwa sasa hawana fedha za kutandaza nyaya kwenye nyumba zao (Wiring) kutumia kifaa cha UMETA (Umeme Tayari) ili kuhakikisha wanapata huduma muhimu ya umeme.

Dkt. Kalemani aliyasema hayo tarehe 13 Juni, 2021 alipofanya ziara kukagua na kuwasha umeme rasmi kwenye kitongoji cha Mtakuja, kijiji cha kibumba wilayani Chato.

Waziri Kalemani alisema, anatambua uwepo wa wananchi ambao katika kipindi ambacho mradi unatekelezwa wanakuwa hawana fedha ya kutandaza nyaya kwenye nyumba zao (Wiring) lakini wanahitaji huduma hiyo muhimu hivyo ni muhimu wakatumia kifaa hicho cha UMETA.

Alisema, wananchi hao wanayo fursa ya kuunganishiwa umeme kwenye mfumo wa umeme wa nyaya za kawaida mara watakapopata fedha na kukamilisha kutandaza nyaya kwenye nyumba zao.

Waziri Kalemani alikumbushia kuwa, UMETA ni kifaa kilichosanifiwa kitaalamu ambacho hupachikwa ukutani na kina matoleo ya kuwasha taa tatu (bulb), runinga, radio na pasi ya umeme na hivyo kukidhi mahitaji muhimu kwa nyumba ndogo isiyozidi vyumba vitatu.   

Aidha, Waziri Kalemani aligawa vifaa 20 vya UMETA kwa wananchi wa kitongoji hicho ili kuhamasisha kaya ambazo hazina uwezo wa kutandaza nyaya kwenye nyumba zao wakati wa mradi, kutokosa fursa ya kupata huduma ya umeme.

Waziri Kalemani pia aliwataka wanakitongoji cha Mtakuja pamoja na wananchi wote nchini, kutunza nguzo za umeme na kutandaza nyaya za umeme kwa wale ambao bado hawajaunganishiwa umeme ili waweze kupatiwa huduma hiyo muhimu.

 

Kuwashwa rasmi kwa umeme katika kitongoji cha Mtakuja kulishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali wa Wilaya ya Chato.

Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani aliambatana na mwakilishi wa Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Edson Ngabo na wataalam kutoka TANESCO na REA.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...