SERIKALI kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) imeshusha viwango vya uchangiaji kwenye Mfuko huo ambapo sasa waajiri kutoka Sekta Binafsi watachangia asilimia 0.6 ya mishahara ya wafanyakazi wao kutoka asilimia 1 waliyokuwa wakichangia hapo awali.


Akitoa ufafanuzi wa uamuzi huo wa serikali, mbele ya waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya Mfuko huo leo Mkoani Dar es Salam Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amesema waajiri wote kutoka sekta binafsi wataanza kuchangia kiwango hicho kipya cha asilimia 0.6 ya mshahara wa mfanyakazi kuanzia mwezi Julai, 2021.

Aidha amesema lengo la mabadiliko hayo ya kiwango cha uchangiaji ni kumpunguzia mzigo mwajiri ili fedha alizokuwa akitumia kuchangia azielekekeze kwenye maeneo mengine ya uendeshaji wa shughuli za uzalishaji.

“ Uamuzi huu ni utekelezaji wa maelekezo ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,amekuwa akitoa kuhusu Taasisi za Serikali kuhakikisha zinaweka mazingira bora ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili kukuza uchumi wa nchi na kulinda rasilimali Watu” Amesema.

Dkt. Mduma amewahakikishia waajiri na waajiriwa kuwa licha ya punguzo hilo, mafao yanayotolewa na Mfuko yatabaki kama yalivyo kama ambavyo sheria iliyoanzisha Mfuko ya mwaka 2016 inavyoeleza.

“ Tuliona hili liwekwe bayana isije kuonekana kwamba kwa kupunguza kiwango cha uchangiaji basi huenda na Mafao nayo yatapungua, lakini Mafao yatabaki kama yalivyo kwani tumejihakikishia kwa kushirikiana na wataalamu kuwa kwa kufanya hivyo Mfuko utabaki imara na kuwa endelevu.” Amesisitiza.

Vilevile Dkt. Mduma amesema mchakato huo umepitia sehemu mbalimbali na kutoa shukrani kwa Chama cha Waajiri nchini (ATE) na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) kwa kushirikiana na Mfuko huo na kufikia katika jambo hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma (katikati) akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari Makao Makuu ya Mfuko jijini Dar es Salaam Julai 26, 2021. Pamoja na mambo mengine alisema kuanzia Julai mwaka huu serikali imeshusha viwango vya uchangiaji kwenye Mfuko ambapo sasa Waajiri kutoka Sekta Binafsi watachangia asilimia 0.6% ya mishahara ya wafanyakazi wao kutoka asilimia 1% waliyokuwa wakichangia hapo zamani wakati waajiri kutoka sekta ya Umma wao wataendelea kuchangia asilimia 0.5% kama ilivyokuwa hapo awali. Wengine pichani kushoto ni Mkurugenzi wa Uendeshaji, Bw. Anselim Peter na kulia ni Dkt. Abdulsalaam Omar, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba. 
Pichani kushoto ni Mkurugenzi wa Uendeshaji, Bw. Anselim Peter akifafanua mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani),kuhusu namna mfuko huo ulivyoshusha viwango vya uchangiaji, ambapo sasa Waajiri kutoka Sekta Binafsi watachangia asilimia 0.6% ya mishahara ya wafanyakazi wao kutoka asilimia 1% waliyokuwa wakichangia hapo zamani wakati waajiri kutoka sekta ya Umma wao wataendelea kuchangia asilimia 0.5% kama ilivyokuwa hapo awali
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma, akijibu maswali ya waandishi wa habari.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bi. Laura Kunenge (aliyesimama), akiongoza mkutano huo.
Baadhi ya waandishi wakisikiliza


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...