Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka Watendaji wanaofanya kazi ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali katika Minada, Mialo na Vituo vya Ukaguzi kufanya kazi hiyo kwa uaminifu na uadilifu huku akionya kuwa hawataweza kuendelea kuwa na Mtendaji atakayejihusisha na vitendo vinavyosababisha upotevu wa mapato ya Serikali.

 Waziri Ndaki aliyasema hayo katika kikao cha Tathmini ya Ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali kwa mwaka uliopita na kuweka malengo mapya ya ukusanyaji mapato kwa mwaka 2021/ 2022 kilichofanyika jijini Dodoma Julai 23, 2021.

 Akiongea na Watendaji hao aliwaeleza bayana kuwa ili waweze kufikia malengo ya kukusanya Shilingi Bilioni 90 walizojiwekea kukusanya kwa mwaka huu wa fedha ni lazima wafanye kazi hiyo kwa uaminifu na uadilifu kinyume na hapo hawatafanikiwa kufikia malengo.

 "Katika kipindi ambacho nimekuwa hapa Wizarani nimepata taarifa nyingi kuhusu baadhi yenu kujihusisha na vitendo vya upotevu wa mapato, acheni kufanya hivyo kwa sababu tukikugundua hatutaweza kuendelea na wewe," alisema Ndaki

 Aliongeza kuwa kumekuwa na vitendo vingi vya upotevu wa maduhuli ya Serikali ambavyo  vimekuwa vikifanywa na baadhi ya maafisa  wasiokuwa waaminifu na  kupelekea serikali kutopata mapato yanayostahili.

 Waziri Ndaki aliendelea kusema kuwa Mhe. Rais, Samia Suluhu Hassan amewaahidi Watanzania mambo mengi mazuri na  ili mambo hayo yaweze kutekelezeka yanahitaji pesa, na miongoni mwa pesa zinazotegemewa na Serikali ni pamoja na zile zinazokusanywa kutoka kwenye minada, mialo na vituo vya ukaguzi.

 Aliendelea kubainisha kuwa kwa mwaka huu atafuatilia kwa karibu utendaji kazi wa watendaji hao na amepanga kukutana nao kila robo mwaka ili kupima utendaji kazi wa kila mmoja ili kuona kama yale malengo yaliyowekwa yanafikiwa.

 "Nitaendelea kuwatembelea katika vituo vyenu vya kazi, nitakuja kwa taarifa na wakati mwingine bila taarifa na nikifika nitataka kujua mmefikia wapi kuhusu ukusanyaji wa maduhuli," alisisitiza Ndaki

 Aidha, Waziri Ndaki aliwaelekeza Watendaji hao kupelekea taarifa ya minada isiyo rasmi ili aitambue na kuifuta  kwa sababu imekuwa ni kikwazo kwa minada inayotambulika kisheria.

 Pia aliwasisitiza Watendaji hao kuendelea kufanya kazi ya Serikali kwa haki ikiwa ni pamoja na kuzuia uvuvi haramu na utoroshaji wa mifugo kwani vitendo hivyo vimekuwa ni sehemu ya upotevu wa mapato ya Serikali.

.Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (katikati) akimueleza jambo Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Amos Zephania (kushoto) muda mfupi baada ya kumaliza Kikao cha Tathmini ya Ukusanyaji wa Maduhuli kwa mwaka uliopita na kuweka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2021/ 2022. Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Emmanuel Bulayi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliohudhuria Kikao cha Tathmini ya Ukusanyaji wa Maduhuli kwa Mwaka wa fedha uliopita na kuweka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2021/2022 uliofanyika jijini Dodoma Julai 23, 2021. Kulia waliokaa ni Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Emmanuel Bulayi na Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Amos Zephania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...