WAZIRI wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano na Mbunge wa Jimbo la Kigamboni Dkt. Faustine Ndugulile ameipongeza Familia ya Liginiku Millinga na mkewe Upendo Ngoda kwa kujitoa na kuanzisha kituo cha kulea watoto watokao katika mazingira magumu kijulikanacho kama Jerusalem Home of Orphanage na kutoa huduma muhimu za afya, lishe bora, malazi na elimu na kuwataka wadau wa maendeleo na wafadhili kuunga mkono jitihada hizo ili kituo hicho kiweze kufikia malengo ya kupanua huduma ya kulea watoto yatima 100 ifikapo 2024.


Akizungumza leo katika kituo hicho kilichopo Kibada,  Mkoani Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja wa makao ya kituo hicho cha malezi, Ndugulile amesema familia hiyo imejitoa kwa dhati bila wafadhili kwa kuhakikisha mazingira ya malezi kwa watoto ni safi na salama.

Waziri Ndugulile amesema haki za msingi kwa watoto zinazosimamiwa na wizara ya Afya kwa watoto hasa zile tano ambazo ni muhimu kuzizingatia na amejiridhisha uwepo wa haki hizo mara baada ya kutembelea, kukagua na kuzungumza na watoto hao.

"Haki tano kwa watoto ni haki ya kuishi, haki ya kuendelezwa kielimu, haki kulindwa, haki ya kushirikishwa pamoja na haki ya kutobaguliwa kwa namna yoyote ile....Baada ya kutembelea katika maeneo wanayoishi watoto hawa na kuzungumza nao nimejiridhisha kuwa haki zote hizi zinatekelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu." Amesema Waziri Ndugulile.

Amesema kuwa kituo cha Jerusalem kimekuwa kikizingatia haki za watoto hao na kutoa malezi bora kwa ujenzi wa taifa imara la baadaye na kuwataka watanzania na wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada hizo ili kukiwezesha kituo hicho kulea watoto wengi zaidi katika mazingira salama zaidi.

Kwa upande wake mwanzilishi na Mama mlezi wa kituo hicho Upendo Ngoda amesema, kituo hicho kinalea watoto 16 wenye umri wa kuanzia siku moja hadi miaka 6 na wamekuwa wakipambana na changamoto  zilizopo na kuwajibika katika kuhakikisha wanawajenga watoto hao katika misingi imara.

Bi. Upendo amesema, jamii na marafiki wa Jerusalem wamekuwa sehemu kubwa ya kushiriki katika kuhakikisha watoto hao wanapata huduma zote muhimu ikiwemo afya bora, bima za afya pamoja na elimu bora.

Vilevile amesema katika huduma hiyo ya malezi hadi sasa wamefanikiwa kuwaunganisha watoto wanne na familia zao.

Kuhusiana na changamoto zinazokikabili kituo hicho bi. Upendo amesema hakuna chanzo cha kudumu cha mapato wala wafadhili  bali kituo hicho kinalelewa na jamii na marafiki pamoja na ufinyu wa eneo la kutolea huduma hiyo hali inayopelekea kushindwa kuwachukuwa watoto wengi zaidi kwa kuwa uwezo wa kituo ni kubeba watoto 18 pekee.

Awali baba mlezi wa kituo hicho na Mbunge ya jimbo la Bumbuli January Makamba aliipongeza familia hiyo kwa kujitoa na kuwatunza watoto hao kwa misingi ya mahitaji ya kimwili na kiroho na kuwataka watanzania na wadau mbalimbali kushiriki katika kuhakikisha watoto ambao ndio hazina ya kesho wanaishi katika mazingira bora na kupata mahitaji muhimu.












 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...