Benki inayoongoza nchini Tanzania, NMB, imeendeleza ufanisi wake kiutendaji katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2021.  Faida baada ya kodi ya mapato imeongezeka kwa asilimia 43 na kufikia shilingi bilioni 134 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 94 ya kipindi kilichoishia June 2020. Ufanisi huu mkubwa umetokana na ongezeko la biashara na miamala, udhibiti wa gharama za uendeshaji na ubora wa mikopo inayotolewa.

Mapato ya Benki yameongezeka kwa asilimia 20 hadi kufikia shilingi bilioni 463 katika kipindi kilichomalizikia mwezi Juni 2021 ikilinganishwa na shilingi bilioni 387 zilizopatikana kipindi kama hicho mwaka jana. Mapato haya yamechangiwa na ongezeko la mikopo kwa wateja na uwekezaji kwenye hati fungani za Serikali.

Vilevile mapato yasiyotokana na riba yameongezeka kwa asilimia 17 hadi kufikia shilingi bilioni 140 ikilinganishwa na shilingi 119 ya kipindi kama hicho mwaka 2020. Ongezeko la mapato yasiyo ya riba yalichangiwa na ongezeko la miamala ya kibenki kutokana na hudumu nzuri zinazotolewa na benki, mahusiano mazuri na wateja, na uwekezaji katika mifumo ya kidigitali.

Pia benki ya NMB imeendeleza ufanisi bora wa kiuendeshaji, sanjari na malengo makuu ya kimkakati pamoja na viwango elekezi vya ufanisi vilivyowekwa na msimamizi wa mabenki, yaani Benki Kuu ya Tanzania.  Katika kipindi hiki cha nusu ya kwanza mwaka 2021, uwiano wa matumizi yasiyo ya riba na mapato halisi umeimarika mpaka asilimia 47, kutoka asilimia 56 katika kipindi kama hiki mwaka jana. Uwiano huu wa asilimia 47, uko ndani ya kiwango cha juu cha asilimia 55 kilichowekwa na Benki Kuu ya Tanzania.

Benki itaendelea kutilia mkazo uimarishaji wa ufanisi huku ikiboresha sana uwekezaji katika teknolojia na vipaumbele vya kimkakati ili kuendeleza utoaji wa huduma bora kwa wateja.

Pia katika kipindi hiki cha nusu ya mwaka 2021, ubora wa mali za NMB uliimarika kutokana na mikakati thabiti ya kuimarisha mikopo ya benki. Katika kipindi hiki, uwiano wa mikopo chechefu uliimarika hadi asilimia 4.3 kutoka asilimia 6.9 katika kipindi kama hiki mwaka jana, ikiwa ndani ya kiwango cha juu ya asilimia 5 kilichowekwa na Benki Kuu ya Tanzania.

Benki ya NMB imeendelea kuimarisha mizania yake ikiwa na ukuaji endelevu hivyo kuonesha kwa jinsi gani benki imeweka misingi bora na imara ya uhusiano wake na wateja. Mikopo ilikuwa kwa asilimia 11 hadi kufikia shilingi trilioni 4.2 kufikia mwisho wa mwezi Juni 2021 ukilinganisha na shilingi trilioni 4 katika kipindi kama hiki mwaka jana.

Amana za wateja zilikua kwa asilimia 8 hadi kufikia shilingi trilioni 5.8 ikilinganishwa na shilingi trilioni 5.5 katika kipindi kama hiki mwaka jana, hii ikionesha mazingira mazuri yaliyowekwa na benki katika uhusiano wake na wateja. Katika kipindi hiki mali za benki zimeongezeka kwa asilimia 6 hadi kufikia shilingi trilioni 7.6 ukilinganisha na shilingi trilioni 7.2 katika kipindi kama hiki mwaka jana.

Akizungumzia mafanikio haya makubwa yaliyopatikana, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna amesema, “Tunajivunia ufanisi bora na uimara wa benki yetu ya NMB. Mafanikio haya makubwa ya nusu ya mwaka 2021 ni kielelezo cha imani kubwa ya wananchi na wateja kwa benki yao ya NMB, ufanisi wa wafanyakazi wa benki ya NMB, utekelezaji bora na usimamizi mzuri wa mpango mkakati wa benki”.  

Aliongeza kusema kuwa, “Tunazidi kujikita katika misingi imara ambayo tumeshaijenga ikiwa ni pamoja na mizania bora ya benki, mtaji mkubwa, matawi mengi, uwezo mkubwa kidijitali, na wafanyakazi bora ili kuweza kusukuma mbele biashara yetu ya benki.

Tukiangalia mbele tunahamasika tukiona  fursa mbalimbali zilizo mbele yetu kutokana na kuzidi kuimarika kwa uchumi wa dunia hasa baada ya madhara makubwa yaliyosababishwa na ugonjwa wa UVIKO-19 pamoja na hatua stahiki zinazochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania kuimarisha sekta ya kibenki”.

Aidha, bi Ruth alimalizia kwa kusema “Tutaendelea kuweka mkazo katika kuwahudumia wateja wetu kwa ufanisi na kutoa huduma bora ili kuhakikisha benki inaendelea  kuleta mafanikio kwa wawekezaji wake na pia kuwajibika katika jamii inayotuzunguka.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...