Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa

 

Ndugu waandishi wa habari, habari za mchana.

 Leo ni mara yangu kwa kwanza kukutana nanyi waandishi wa habari wenzangu wa hapa Jijini Dar es Salaam tangu nilipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.

 Kabla ya kukutana nanyi hapa Dar es Salaam nimekutana na Waandishi wa Habari wenzetu wa Jijini Dodoma mara mbili na hata taarifa ya mwisho ya Msemaji Mkuu wa Serikali ambayo tunaitoa kila mwezi niliitoa Dodoma tarehe 04 Juni, 2021.

 Awali ya yote kabisa naomba kuwashukuru sana kwa ushirikiano mkubwa mlionipa katika kipindi chote cha miaka 5 na miezi 5 nilipokuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU. Kwa pamoja tulifanya mambo mengi na kwa dhati ya moyo nataka kusema kazi yangu ilikuwa nyepesi kutokana na jinsi mlivyokuwa tayari muda wote kufanya kazi za Ikulu.

 Matarajio yangu ni kuwa tutaendelea kushirikiana katika majukumu haya mapya niliyopangiwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeniteua kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali tangu Aprili 04, 2021.

 Nami nataka kuwahakikishia kuwa nipo tayari kushirikiana nanyi kuikuza sekta hii ya habari. Nitamani kuona tunashirikiana sio tu kusimamia sheria na taratibu bali kuileta, kuiheshimisha na kupandisha thamani yetu machoni mwa tunaowahudumia.

 Sasa ndugu zangu mwezi uliopita sikufanya mkutano na waandishi wa habari wa kila mwezi kwa sababu niliona tuupishe mwezi huo kwa ajili ya kupata hotuba muhimu ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipozungumza na Wahariri kuhusu siku 100 za tangu aingie madarakani.

 Kwa niaba ya Serikali naomba kuwashukuru waandishi wa habari wote kwa jinsi mlivyoshiriki ipasavyo kutoa taarifa mbalimbali na muhimu kuhusu utendaji wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha siku 100 za kwanza. Mmefanya kazi kubwa ya kuandaa Makala za magazeti, Makala za redio na televisheni, habari mbalimbali, vipindi vya majadiliano na kutangaza maudhui mbalimbali yaliyohusu utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kipindi hicho.

 Mhe. Sami Suluhu Hassan anawashukuru sana kwa jitihada hizi kubwa mnazozifanya na anawaomba muendelee kufanya hivyo kwa kuwa sote kwa pamoja tunaijenga Tanzania yet una sisi waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kuitangaza sura njema ya Tanzania ndani na nje ya mipaka yetu. Mhe. Samia Suluhu Hassan anasema anawapenda waandishi wa habari wote na anawaamini sana katika jukumu hilo, hatarajii kuona mnamzingua.

 

Leo nitakuwa na masuala kadhaa ya kuwapa taarifa kutoka Serikalini.

 

1.   Hali ya Serikali

Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan inaendelea vizuri kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba na Sheria.

 

Kwa ujumla Serikali inaendelea kutoa huduma mbalimbali za kiutawala na kimaendeleo.

 

Hali ya ulinzi na usalama ni nzuri, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha nchi ipo salama, mipaka ya nchi yetu inalindwa ipasavyo na Watanzania wanakuwa na hali ya amani na utulivu ambayo inawawezesha kufanya shughuli zao mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

 Ulipaji wa mishahara ya wafanyakazi, unaendelea kufanyika kama kawaida. Wafanyakazi wanalipwa mishahara yao kabla ya mwezi kuisha, wafanyakazi wenyewe watakuwa mashahidi mishahara wanaipata kabla ya tarehe 25 ya kila mwezi bila kukosa. Tunalipa takribani shilingi Bilioni 630 kwa mwezi.

 Pamoja na kulipa mishahara ya wafanyakazi, kama ilivyoahidi kwa mara ya kwanza mwezi Juni 2021 Serikali imetekeleza ahadi yake ya kuanza kuwalipa Madiwani moja kwa moja kutoka hazina. Katika Mwezi Juni huu Madiwani wamelipwa shilingi Bilioni 1.8, hawa ni Madiwani wote isipokuwa wale wanaotoka Majiji na baadhi ya Manispaa zenye ukusanyaji mkubwa wa mapato (yaani halmashauri ambazo zipo katika daraja la A).

 Kwa kufanya hivi Serikali imeondoa tatizo ambalo katika baadhi ya halmashauri Madiwani walikuwa wanakosa malipo ya mwezi kutokana na uwezo mdogo wa halmashauri, na kulazimika kukopwa. Sasa kila Diwani analipwa moja kwa moja kutoka hazina kiasi cha shilingi 350,000 kwa mwezi na wenyeviti wao wanalipwa shilingi 400,000.

 Serikali inaendelea kulipa madeni ya ndani ya wazabuni na watoa huduma mbalimbali na kwa kufanya hivyo mzunguko wa fedha umeendelea kuongezeka, na mzunguko wa fedha unapoongezeka maana yake vipato vya wananchi vinaongezeka na ajira zinaongezeka.

 Serikali imeendelea kugharamia miradi ya maendeleo. Kama mnavyojua tunayo miradi ya maendeleo ya kimkakati, na tunayo miradi ya maendeleo ya kawaida ikiwemo ya ujenzi wa barabara, miradi ya maji, hospitali, vituo vya afya na zahanati, ujenzi wa majengo mbalimbali, umeme, viwanja vya ndege n.k

 Katika kipindi cha robo ya nne ya mwaka 2020/2021 ambayo ni kati ya Aprili na Juni Serikali imetoa kiasi cha shilingi Trilioni 2.785 kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimali ya maendeleo. Humu ndani yake kuna miradi ya maji, barabara, madaraja, viwanja vya ndege, kununua ndege, umeme, majengo ya shule, elimu bila malipo, mikopo ya elimu ya juu, maabara, madarasa, reli, meli, nyumba, dawa na vifaa tiba na mengineyo.

 

Hali ya kichumi.

Uchumi wetu umeendelea kuwa imara.

Mfumuko wa bei kwa mwezi Juni ulikuwa 3.6% ambayo ni chini ya ukomo uliopangwa wa 5%.

 Serikali imeendelea kuimarisha viashiria vya ukuaji wa uchumi ili kufikia ukuaji wa asilimia 5.6 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 wa mwaka 2020.

 Aidha, akiba yetu ya fedha za kigeni hadi Julai 2021 ilikuwa ni Dola za Marekani Bilioni 5.5 ambazo zinatosheleza kununua bidhaa na huduma kwa takribani miezi 6.5. kiwango hiki ni zaidi ya lengo la utoshelevu la akiba ya miezi 4.5 lililowekwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

2.   Chanjo ya Uviko -19 (ugonjwa wa Korona)

Tarehe 24 Julai, 2021 nchi imepokea shehena ya kwanza ya chanjo 1,058,400 kutoka nchini Marekani. Chanjo hizi ni aina ya Johnson & Johnson (Jansen) na zimeletwa chini ya mpango wa Shirika la Afya Duniani uitwao (Covax Facility) ambao unatoa msaada wa chanjo za kukabiliana na Uviko 19 kwa nchi mbalimbali duniani hasa zinazoendelea.

Chini ya utaratibu wa mpango huu, Tanzania kama ilivyo kwa nchi zingine itapatiwa chanjo za kutosheleza asilimia 20 ya wananchi wote wa Tanzania (ukifanya hesabu utaona chanjo zitakazoletwa ni takribani dozi 11,000). Kwa hiyo chanjo 1,058,400 zilizoletwa ni sehemu ya chanjo hizi.

 Kama sote tunavyojua Mhe. Samia Suluhu Hassan juzi amezindua chanjo hizi, kwa yeye mwenyewe kuchanja na viongozi wengine kuchanja huku vyombo vya habari vikionesha zoezi hilo Mubashara.

 Kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inakamilisha taratibu za kupeleka chanjo katika vituo mbalimbali vya Mikoa yote hapa nchini. Vimeainishwa vituo 550 lakini maelekezo ya Wizara ya Afya kuwepo flexibility katika mikoa yenyewe wakiona kuna umuhimu wa kuongeza kituo basi wafanye hivyo lakini kwa kuzingatia muongozo wa utoaji wa chanjo uliowekwa na Wizara.

 Tangu zoezi limeanza mambo yanakwenda vizuri hakuna malalamiko ambayo Serikali imeyapata kutoka kwa wanaopokea chanjo hiyo. Wataalamu wetu wamezikagua chanjo zilizoletwa na wametuhakikishia kuwa chanjo hizi ni salama na zinafaa. Pamoja na viongozi wetu wao wenyewe wataalamu wanachoma chanjo kwa ajili ya kujikinga wao wenyewe na kuwakinga watu wengine.

 Serikali inawasihi Watanzania wote kufuata maelezo na miongozo inayotolewa na Wataalamu wetu.

 Kumekuwa na uchochezi na upotoshaji mwingi kwenye jamii unaoenezwa na watu wasiokuwa wataalamu katika masuala haya, upotoshaji huu kwa sehemu kubwa unafanywa kupitia mitandao ya kijamii. Natoa wito kwa vyombo vya habari, tufanye kazi zetu kwa kuzingatia weledi na kutovunja sheria za nchi yetu. Tusije tukajiingiza kwenye kuchochea uchochezi huu na kusababisha wananchi kutotumia fursa hii ya kukabiliana na ugonjwa wa korona.

 

Tunasisitiza chanjo hii ni hiari, ukiona inafaa kuchanjwa nenda kwenye vituo vilivyotengwa nchi nzima kachanje ukiona vipi hulazimishwi. Kumekuwa na watu ambao wanatumia picha na majina ya viongozi kuwatisha wananchi, naomba watu hao waache mara moja kwa sababu wanachokifanya ni uhalifu na yeyote atakayefanya uhalifu atafikiwa. Hata waliotengeneza upotoshaji kwa kutumia picha yangu wamekamatwa na watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria taratibu zikikamilika.

 

Aidha, Serikali inaendelea kusisitiza Watanzania wote kuzingatia tahadhari zote zilizotolewa na wataalamu wa afya juu ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu.

 

Msimamo wa Serikali ni kuwa shughuli za maisha yetu ya kawaida ziendelee lakini tuzingatie mwongozo ambao wataalamu wetu kupitia Wizara ya Afya wameutoa utakaotusaidia kukabiliana na maambukizi. Mwongozo huu ndio unaotutaka kuvaa barakoa, kunawa maji tiririka kwa sabuni, kutumia vitakasa mikono, kujiepusha na misongamano na pale inapobidi basi tuzingatie umbali usiopungua meta moja kutoka mtu mmoja hadi mwingine, kufanya mazoezi na pia kupimwa joto tunapoingia katika maeneo ya jumuiya.

 

Na ndugu zangu waandishi wa habari kwa kuwa nasi ni moja ya makundi yaliyokatika hatari ya kuambukizwa virusi vya korona leo Ofisi yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto tumeandaa utaratibu ambapo kwa wale watakaokuwa tayari kuchoma chanjo watachoma.

 

3.   Hali ya utoaji wa huduma za kijamii.

Serikali imeendelea kutekeleza jukumu lake la utoaji wa huduma za kijamii kama vile matibabu, maji, umeme na nyinginezo.

 

Kwa matibabu pamoja kuendelea na ujenzi wa miundombinu ikiwemo Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati katika maeneo mbalimbali. Serikali imetoa shilingi Bilioni 130 kwa ajili ya kuagiza dawa kufuatia dawa kupungua katika vituo vya kutolea tiba, na hili limekwenda sambamba na kuwalipa wazabuni ambao walisambaza dawa na kukawa na madeni (hawa wazabuni wamelipwa shilingi Bilioni 39).

 

Aidha Serikali imetoa shilingi Bilioni 14 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuzalisha mipira (gloves), vidonge vya rangi mbili, dawa za maji za watoto na vidonge vya kawaida katika eneo la Idofi, Makambako Mkoani Njombe. Hii ni hatua kubwa na muhimu kwa nchi yetu kwa sababu inatuondoa kwenye utegemezi wa dawa. Kwa kujenga kiwanda hiki pekee Serikali itaokoa shilingi Bilioni 33 ambazo zingetumika kama dawa na mipira ya mikono inayozalishwa katika kiwanda hiki ingeagizwa kutoka nje ya nchi.

 

Kwa Maji, Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji kwa Watanzania. Kama mnavyojua lengo ni kuhakikisha ifikapo 2025 Watanzania waishio mijini wanapatiwa maji kwa asilimia 95 na Vijijini kwa asilimia 85. Kwa sasa mijini maji yamewafikia wananchi kwa asilimia 86 na vijijini ni asilimia 72.3.

 

Kuna miradi ya maji ambayo imekamilika kwa asilimia 100. Baadhi yake ni;

·        Mradi wa maji ya Ziwa Victoria kwenda Tabora, Igunga na Nzega uliogharimu shilingi Bilioni 617.

·        Mradi wa maji wa Magu uliogharimu shilingi Bilioni 16.

·        Mradi wa Misungwi uliogharimu shilingi Bilioni 13.

·        Mradi wa maji wa Kagongwa – Isaka uliogharimu shilingi Bilioni 24.

·        Mradi wa maji wa Lamadi uliogharimu shilingi Bilioni 12.

·        Mradi wa maji wa Sumbawanga ambao umegharimu shilingi Bilioni 35.

Hii ni baadhi tu ya miradi.

 

Kuna miradi ya maji ambayo utekelezaji wake unaendelea.

·        Mradi mkubwa wa maji wa Arusha utakaogharimu shilingi Bilioni 520 hadi kukamilika umefikia asilimia 71.

·        Mradi wa maji wa Mgango – Kiabakari  utakaogharimu shilingi Bilioni 70 umefikia asilimia 15.

·        Mradi wa maji wa Orkesument – Simanjiro utakaogharimu shilingi Bilioni 40 umefikia asilimia 97.

·        Mradi wa maji wa Tinde – Shelui utakaogharimu shilingi Bilioni 24 umefikia asilimia 20.

·        Mradi wa Maji wa Isimani- Kilolo – Iringa utakaogharimu shilingi Bilioni 9.5 umefikia asilimia 40.

·        Na kuanzia mwezi Novemba mwaka huu 2021 tutaanza kujenga mradi wa maji wa Simiyu utakaogharimu shilingi Bilioni 444.

 

Kwa Mkoa wa Dar es Salaam kazi kubwa imefanyika kuhakikisha Mkoa huu unapata maji ya kutosha. Dhamira hii imefanikiwa kwa sehemu kubwa baada ya kukamilisha miradi ya maji ya Kisarawe, Pugu – Gongolamboto  na Mkuranga. Kazi inayoendelea sasa ni kushughulikia matatizo ya maji yaliyopo Kigamboni, Chalinze na Kibamba.

 

Lakini mwelekeo wa Serikali kwa sasa ni kutumia vyanzo vya maji vya uhakika ikiwa ni pamoja na mito na maziwa makuu yakiwemo Victoria, Nyasa na mito ya Ruvuma, Kagera, Rufiji na Kiwira. Hii itasaidia kuondoa tatizo la kujenga mradi ambao baadaye utapata changamoto ya chanzo cha maji.

 

Kwa hiyo kuna miradi mikubwa zaidi ya maji inakuja. Dhamira ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha anamtua Mama ndoo, na ameshasema kwamba kwenye eneo hili atatupia macho sana. Kwa hiyo wadau wote wa maji tujue mwelekeo huu wa Mhe. Rais na tusimzingue.

 

Kwenye umeme, Serikali imeendelea kutoa huduma ya nishati ya umeme kupitia gridi ya Taifa ambayo kwa sasa uzalishaji wake ni Megawati 1,604 kiasi ambacho ni zaidi ya mahitaji yetu ya nchi nzima ya sasa ambayo ni megawati 1,200. Sasa hivi Tanzania ukisikia mgao wa umeme basi ujue hautokani ni uhaba wa uzalishaji bali sababu zingine labda kujenga njia za umeme, kubadilisha transifoma ama kurekebisha mifumo katika maeneo mbalimbali.

 

Kuhusu upelekaji umeme vijijini kazi ya kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini inaendelea vizuri. Hadi sasa Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imeshafikisha umeme katika vijiji 10,324 kati ya vijiji vyote 12,268. Kwa hiyo vijiji vilivyobaki ni 1,944 na hivi vyote wakandarasi wapo tayari site wanapeleka umeme ili ifikapo Desemba 2022 vifikiwe na umeme na tubakiwe na kazi ya usambazaji tu.

 

MSISITIZO (Gridi ya Taifa – ningependa kueleza kidogo)

Pamoja na juhudi zilizofanyika, Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kujenga njia za umeme za gridi ya Taifa, zitakazosafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400. Tunayo miradi mikubwa ambayo kazi zinaendelea na mingine ipo mbioni kuanza.

                                i.            Tunao mradi wa ujenzi wa kujenga njia ya umeme ya kuunganisha nchi tatu Zambia, Tanzania na Kenya (ZTK).

·        Sehemu ya mradi huu imekamilika kwa asilimia 100 ambayo ni Iringa – Dodoma – Singida – Shinyanga (Kilometa 617) kwa gharama ya shilingi Bilioni 753, kulikuwa na kazi ya kuboresha kituo cha Dodoma na imekamilika pia.

·        Kinachoendelea sasa ni kujenga njia ya kuanzia Singida – Namanga – Arusha (kilometa 414) na hii ndio itaunganisha hadi Isinya nchini Kenya. Kazi hii imefikia asilimia 85 na itakamilika Desemba 2021 kwa ghama ya shilingi Bilioni 594.

                             ii.            Tunao mradi wa ujenzi wa njia ya umeme ya Iringa – Tunduma – Sumbawanga – Kigoma – Nyakanazi (Inaitwa Gridi ya Kaskazini Magharibi). Kipande cha kwanza cha Iringa – Sumbawanga kilometa 418 ujenzi utaanza Novemba mwaka huu kwa gharama ya shilingi Trilioni 1.07 na kipande cha tatu cha Kigoma – Nyakanazi (kilometa 128) ambacho ujenzi wake utagharimu shilingi Bilioni 283 unatarajiwa kuanza mwezi Septemba mwaka huu.

·        Sehemu ya njia hii pia itatumika sasa kuunganisha njia ya kwenda Zambia kukamilisha ile ZTK (Zambia, Tanzania, Kenya).

                           iii.            Tunayo miradi ya ujenzi wa njia za umeme ya kilovoti 220.

·        Tunajenga njia ya umeme ya Nyakanazi – Geita kilometa 114 kwa gharama ya shilingi Bilioni 421. Kazi hii imefikia asilimia 86.

·        Tumekamilisha ujenzi wa njia ya umeme ya Geita – Bulyakhulu kilometa 53 kwa gharama ya shilingi Bilioni 123.

·        Tumekamilisha ujenzi wa njia ya umeme ya Kurasini – Kigamboni Mkoani Dar es Salaam kilometa 14 kwa gharama ya shilingi Bilioni 290. Kazi hii imekamilika mwezi uliopita wa Juni.

 

                           iv.            Tuna mradi wa ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Rufiji (kwenye mradi wa Bwawa la umeme la Julius Nyerere) hadi Chalinze ili ukaungane na Gridi ya Taifa kilometa 167. Ujenzi huu umeanza na unatarajiwa kukamilika Aprili 2022 kwa gharama ya shilingi Bilioni 158. Mkandarasi yupo site. Kazi ni lazima ikamilike mapema kwa sababu Juni 2022 Bwawa la Julius Nyerere litakuwa linaanza kuzalisha umeme na litahitaji njia ya kuusafirisha kwenda gridi ya Taifa.

·        Kutoka hapo Chalinze tutatekeleza miradi miwili ya kujenga njia za msongo wa kilovoti 400.

Kwanza, ni kutoka Chalinze – Kinyerezi (Dar es Salaam) kilometa 115. Kazi hii itaanza Januari 2022.

Pili, ni kutoka Chalinze – Dodoma kilometa 325. Mchakato wa kupata mkandarasi kwa ajili ya kazi hii unaendelea na matarajio ni kuwa mradi huu pia uanza haraka iwezekanavyo.

 

Nimeitaja miradi hii kwa sababu nchi yetu inakwenda kuongeza uzalishaji mkubwa wa umeme kuanzia Juni 2022. Tukianza kuzalisha Megawati 2,115 pale Bwawa la Julius Nyerere nchi yetu itakuwa na zaidi ya Megawati 3,715. Umeme huu tutahitaji kuuza kwa majirani zetu, na ndio maana kuna kazi hizi kubwa zinazoendelea.

 

Kwa elimu, Serikali imeendelea kutoa elimu bila malipo kwa wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari. Katika robo ya mwisho ya mwaka 2020/21 imetoa shilingi Bilioni 62.416. Serikali pia imeendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambapo katika robo hiyo ya mwisho imetoa shilingi Bilioni 137.373.

 

Kwenye eneo la elimu ya juu, katika bajeti ya mwaka 2021/22 Serikali imepanua uwigo zaidi ambapo imeongeza fedha kutoka shilingi Bilioni 450 hadi kufikia shilingi Bilioni 570. Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mwanafunzi atakayehitaji mkopo wa elimu ya juu na anakidhi sifa apatiwe mkopo. Na haya ni mafanikio makubwa sana.

 

Lakini fedha nyingine nyingi zimetengwa kwa ajili ya kumalizia maboma ya shule, kujenga nyumba za walimu na kujenga shule moja ya sekondari ya wasichana ya masomo ya sayansi kwa kila mkoa.

 

Kwa sekta ya afya, kazi kubwa imeendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma kwa kuendeleza huduma zinazotolewa na kuanzisha huduma mpya. Kama mnavyojua Serikali inaendelea na maandali ya kutekeleza mpango bima ya afya kwa wote. Katika Bunge la Septemba mwaka huu, Serikali itawasilisha mswada wa sheria ya Bima ya Afy kwa wote ambapo katika mwaka huu wa 2021/2022 imetenga shilingi Bilioni 149.7 kwa ajili ya kuanza kuwapatia bima za afya wananchi watakaotambuliwa kuwa hawana uwezo wa kugharamia malipo ya Bima. Kwa hiyo safari hii ni safari halisi, hakuna maneno maneno. Tunataka Watanzania wote wawe na uhakika wa kupata matibabu.

 

Katika juhudi hizi hizi za kuimarisha huduma za afya, kazi kubwa imeendelea kufanyika katika kuimarisha matibabu ya kibingwa. Mnafahamu lengo la Serikali ni kuifanya Tanzania kuwa UTALII WA MATIBABU (Medicine Tourism).

Sasa katika kutimiza hili Serikali imeendelea kusambaza vifaa vya uchunguzi na tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kama ifuatavyo;

 

                                i.            Imekamilisha usimikaji wa mitambo ya kuzalisha hewa-tiba katika Hospitali za Rufaa za Mikoa 7 (Geita, Manyara, Dodoma, Dar es Salaam-Amana, Mtwara, Ruvuma-Songea, Mbeya). Mradi huo umegharimu jumla ya shilingi bilioni 8.7. Na hii ndio inayotusaidia katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya Uviko – 19, nab ado juhudi nyingine mbalimbali zinahitaji katika kuwezesha hospitali nyingine kuwa na mitambo ya kuzalisha hewa ya oksijeni.

                             ii.            Vilevile, serikali imekamilisha kufunga mashine kwa ajili ya kupasua ubongo bila kufungua kichwa (Angio Suite iliyogharimu 7.9 bilioni) katika Hospitali ya Mifupa ya MOI. Huduma zimeanza kutolewa.

                           iii.            Mtambo wa kisasa wa pili wa Cathlab na Carto 3 wenye thamani ya Shilingi bilioni 4.6 umefungwaa na kuanza kufanya kazi katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete. Mtambo huu utatumika kufanya uchunguzi na kutibu magonjwa ya moyo katika ubora wa hali ya juu sana.

                           iv.            Katika Taasisi ya Kansa ya Ocean Road yanaendelea maandalizi ya kusimika mtambo wa Pet Scan itakayogharimu shilingi Bilioni 18 na tayari 14.5 bilioni imeshatolewa.

                             v.            Serikali imenunua mashine 18 za Digital X-ray zenye thamani ya Tzs. Bilioni 5.3, mashine hizi zimepelekwa katika Hospitali za Halmashauri. Hospitali 14 za Wilaya kati ya hizo 18 ambazo ni; Mangaka, Tunduru, Mbinga, Kasulu, Nyamagana, Butiama, Makambako, Makete, Mbarari, Tukuyu, Itumba, Nkasi, Usangi, na Same zimeanza kutoa huduma, na hospitali 4 za Wilaya bado hazijafungwa kwa sababu ukarabati na ujenzi wa majengo yake bado unaendelea.

                           vi.            Pale Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza (Sekou Toure) Serikali imenunua vifaa ambavyo ni CT scan, Ultra Sound na vifaa vya mama na mtoto, upasuaji, utakasaji na incinerator. Vifaa hivi vimeshasimikwa na vinatoa huduma katika. Thamani ya vifaa tiba hivyo vyote ni Tzs. Bilioni 2.2.

                        vii.            Tunasimika mtambo wa MRI katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa (Bugando) wenye thamani shilingi bilioni 2.43.

                      viii.            Tumeshasimika CT Scan katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (Mwananyamala – Dar es Salaam) wenye thamani ya shilingi Bilioni 1.444.

                           ix.            Pia kuna vifaa vingine vyenye thamani ya shilingi Bilioni 6 ambavyo ni Fluoroscopy, Digital X-ray, ultrasound, mama na mtoto, upasuaji, utakatisaji, incinerator vinasimikwa katika hospitali 9 hapa nchini; Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma (Maweni), Bukoba, Misungwi, Musoma, Bukombe, na Chato.

Aidha, Kwa miundombinu Serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 150 kukamilisha majengo ya hospitali za Mikoa na Kikanda ambazo zimefikia hatua zifuatazo; Hospitali za Mkoa ya Njombe, Geita, Songwe umekamilika kwa zaidi ya asilimia 98. Sekou Toure-Mwanza ujenzi wake upo zaidi ya asilimia 80. Hospitali za Kikanda, Mtwara ni zaidi ya asilimia 97, Burigi/Chato umekamilika kwa asilimia 100 na Hospitali ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Meta) ipo zaidi ya asilimia 80.

Lakini pia Serikali imeajiri watumishi wa afya zaidi ya 4,127 kwa ajili ya kukabiliana na uhaba wa watumishi katika vituo vya kutolea huduma.

 

 

 

4.   Miradi ya kimkakati.

Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kama ambavyo Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwaahidi Watanzania.

 

                     i.        Ujenzi wa Reli ya Kati.

Mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge Railway – SGR) kipande cha kuanzia Dar es Salaam mpaka Morogoro (kilometa 300) ujenzi umefikia asilimia 92. Mkandarasi ameshalipwa shilingi Trilioni 2.181.

TANESCO wameshakamilisha ujenzi wa njia ya umeme kwa ajili ya kuendesha treni yenye urefu wa kilometa 160 kwa gharama ya shilingi Bilioni 73.3.

Katika kipande hiki tunatarajia Treni ya abiria ya majaribio ya kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro inatarajiwa kuanza Novemba 2021.

 

Kipande cha kuanzia Morogoro – Makutupora ya Singina (kilometa 422) kimefikia asilimia 66 na kazi inaendelea vizuri. Mkandarasi ameshalipwa shilingi Trilioni 1.218.

 

Ujenzi wa reli hii kutoka Dar es Salaam – Morogoro Makutupora utagharimu shilingi Trilioni 7.02.

·        Jambo muhimu katika utekelezaji wa miradi hii ni kuwa malipo kwa Wakandarasi yanafanyika vizuri, kila wanapoleta hati za madai ya malipo (Certificates) Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan inawalipa bila kuacha deni lolote.

·        Kwa hiyo Watanzania tuendelee kumuombea Rais wetu, tuiombee Serikali yetu kwa kuwa yale mashaka ambayo baadhi walidhani baada ya kuondokewa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Awamu ya Tano kwamba miradi ingekwama yameondoka na Mhe. Rais Samia anaendelea na miradi yote kwa kasi kubwa.

 

Kipande cha Tano cha Mwanza – Isaka (kilometa 341), Mkandarasi anaendelea na kazi ya kusafisha njia kwa ajili kujenga tuta la reli.

 

Tayari, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo ya kuanza kwa ujenzi wa kipande Tatu cha kuanzia Makutupora – Tabora na kipande cha nne cha Tabora – Isaka. Maandalizi yanaendelea ikiwa ni pamoja kupata wakandarasi wa kuanza ujenzi.

 

Pia Mhe. Rais ameagiza maandalizi yaanze kuunganisha reli hii kwenda Kigoma na pia kuunganisha reli hii kuanzia Kaliua (Tabora) hadi bandari ya Kalema (Ziwa Tanganyika). Maandalizi haya yote yanaendelea.

 

                   ii.        Bwawa la Julius Nyerere.

Ujenzi wa Bwawa la umeme la Julius Nyerere katika mto Rufiji.

Kazi inaendelea, ujenzi umefikia asilimia 56. Mradi huu unatarajiwa kukamilika Juni 2022 ambapo utatuzalishia megawati 2,115 zitakazoingia katika gridi ya Taifa.

 

Tayari Mkandarasi ameshalipwa zaidi ya shilingi Trilioni 2.5 na kila anapotoa hati ya madai (Certificate) analipwa papo hapo.

 

Kama mnavyofahamu mradi huu utaambatana na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Kuna eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji la ukubwa wa hekta 150,000.

Bwawa litakusanya maji mengi kiasi cha Meta za ujazo Bilioni 35, katika eneo la urefu wa kilometa 100. Hii itatuwezesha kuzalisha umeme hata wakati usio wa mvua.

 

Kinachoendelea hivi sasa Serikali ni maandalizi ngazi ya Wizara kuweka mpango wa kitaifa wa namna ambavyo fursa za uvuvi, utalii, kilimo na mengine yatavyotumika. Na Kamati hii ipo chini ya Makatibu Wakuu.

 

                 iii.        Ununuzi wa Ndege.

Kama wote mnavyojua Serikali imeshanunua ndege 11, ndege 9 zimewasili na ndege nyingine mbili aina Air (A220-300) zitawasili wakati wowote kuanzia sasa. Hizi ni juhudi za kulijenga shirika letu la ndege la ATCL ambalo linafanya kazi nzuri na kuleta matokeo katika ukuaji wa uchumi na kurahisisha usafiri wa anga kwa Watanzania na wageni wakiwemo watalii.

 

Japo kumekuwa na changamoto ya ugonjwa wa Uviko 19, lakini Shirika letu linaendelea kukabiliana nayo kwa kuhakikisha linafanya kazi kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu ya kuzuia maambukizi.

 

Ndani ya Tanzania ATCL ina vituo 15 inavyotua, na nje ya Tanzania kuna 7 vya kikanda. Hivi Karibuni ndege zetu zinatarajia kurejesha safari zake za Lubumbashi, Msumbuji na Johannesburg. Pia safari za Mumbai-India na Guanzhou-China zinaendelea kufanyiwa kazi ili zirejee hivi karibuni.

 

Upo mpango wa kuongeza ndege zingine 5 ukiondoa hizi 11 ambazo tayari zimeshanunuliwa. Tayari ATCL imetiliana sahihi na watengenezaji wa ndege hizo. (Kati ya ndege hizo1 masafa marefu, 2 masafa ya kati, 1 masafa mafupi na 1 ya mizigo)

 

                 iv.        Ujenzi na uendelezaji wa Jiji la Dodoma (Makao Makuu)

Kazi mbalimbali zinaendelea zikiwemo ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato utakaogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 620, ujenzi wa kilometa 112 za barabara za mzunguko (Ring Roads) utakaogharimu takribani shilingi Bilioni 500, kuna ujenzi wa majengo ya Serikali kwa ajili ya kutolea huduma katika Mji wa Serikali Mtumba, kuna ujenzi wa barabara za ndani ya Jiji la Dodoma.

 

Kuna mradi wa maji wa FARKWA, AfDB wameridhia kutoa fedha za masharti nafuu (kiasi cha shilingi Bilioni 910) kwa ajili ya kujenga Bwana na kulaza mabomba yatakayopeleka maji Chema, Dodoma Mjini, Chamwino na Bahi. Mradi huu utatekelezwa kwa awamu mbili. Kwa sasa maandalizi yanaendelea

                             v.             

 

 

5.     Ujenzi wa Miundombinu (Barabara na madaraja)

Serikali inaendelea na jukumu lake la kupanua mtandao wa barabara, kuna miradi iliyokamilika na miradi mingine inaendelea kutekelezwa. Wakandarasi wanaotekeleza miradi hii wanalipwa kulingana na wanavyozalisha hati za madai ya kazi zao.

 

Barabara.

·        Upanuzi wa barabara kuu ya Kimara – Kibaha (kilometa 19.2) umefikia 90%

·        Ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya pili (kilometa 20.3) kazi imefikia asilimia 22.

·        Ujenzi wa barabara ya Tabora – Koga - Mpanda (kilometa 356) umefikia asilimia 75.

·        Ujenzi wa barabara ya Mbinga – Mbambabay (kilometa 66) umekamilika kwa 100.

·        Ujenzi wa barabara ya Kabingo – Kasulu – Manyovu (kilometa 260.6) umefikia 7%

·        Ujenzi wa barabara ya Lusitu – Mawengi (kilometa 50) umefikia 69%

·        Ujenzi wa barabara Njombe – Moronga – Makete (kilometa 107.4) umefikia 77%

·        Ujenzi wa barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga (kilometa 112) umekamilika kwa 100%

Madaraja

·        Daraja la Tanzanite linalounganisha Coco Beach na Aga Khan Dar es Salaam (kilometa 1.03) limefikia 90%

·        Daraja la JP Magufuli linalounganisha Kigongo na Busisi katika Ziwa Victoria Mkoani Mwanza (kilometa 3.2) limefikia 28%.

·        Daraja la Wami katika mto Wami (meta 510) limefikia 51%

 

 

Lakini kupitia TARURA, mwaka huu Serikali imeamua kuja na mpango maalum kabisa wa kukabiliana na hali mbaya ya barabara. Kwa kutenga shilingi Bilioni kwa kila jimbo kwa ajili ya barabara. Sasa itakuwa ni uamuzi wa jimbo husika kutumia fedha hizo kujenga barabara ya lami ya kilometa 2 au kujenga barabara za changarawe za urefu wa kilometa 20.

 

 

6.   Kuvutia uwekezaji, kuboresha mazingira ya kufanya biashara.

Kufuatia maelekezo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyetaka kuongeza jitihada za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, hatua madhubuti zimechukuliwa kuhakikisha vikwazo mbalimbali vinaondolewa. Miongozi mwake ni kutekeleza ule mpango wa kuvutia wawekezaji uitwao Blue Print.

 

Ukusanyaji wa kodi wa maguvu na kutisha walipa kodi umedhibitiwa na sasa walipa kodi wanalipa kodi zao kwa amani na hali inaonesha kuwa nzuri.

 

Mhe. Rais yeye mwenyewe amekutana na viongozi wa taasisi ya sekta binafsi (TPSF) na kuzungumza nao na amekuwa akiambatana nao katika safari zake alizozifanya nchini Kenya na Burundi. Matokeo ni mazuri sana, na wafanyabiashara na wawekezaji wengi wanakuja kuwekeza hapa Tanzania.

 

 

7.   Kuhusu Sensa ya Watu na Makazi.

Kama mnavyojua, nchi yetu hufanya Sensa ya watu na Makazi kila baada ya miaka 10. Sensa inafanyika kwa lengo la kupata idadi ya watu na Makazi ili takwimu hizo zitumike katika kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi.

 

Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yanaendelea na Sensa ya Majaribio inatarajiwa kufanyika Agosti 2021.

 

Tumeandaa Mkakati wa Mawasiliano kwa ajili ya kutoa elimu na taarifa mbalimbali kwa jamii. Kwa sehemu kubwa mkakati huu utatuhusisha sisi Waandishi wa Habari, niwaombe Waandishi wa Habari wenzangu tutoe ushirikiano katika jukumu hili. Kutakuwa na vipindi, Makala, majarida na kazi nyingine mbalimbali za uandishi na utangazaji, naomba tujitoe kufanya jukumu hili lenye maslahi makubwa kwa Taifa letu.

 

Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (OCGS) tutakuwa tayari muda wote kushirikiana na Vyombo vya Habari na Waandishi wa Habari kufanikisha jukumu hili muhimu.

 

8.   Hali ya ukusanyaji wa mapato.

Kama mtakumbuka, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipoingia madarakani aliagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iachane na ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mabavu ikiwemo kutumia vikosi kazi na vitisho dhidi ya walipa kodi. Utekelezaji wa maelekezo hayo umefanyika na kumekuwa na hisia miongoni mwa jamii kuwa pengine hatua hii ingeshusha mapato kwa kiasi kikubwa na kuathiri utendaji kazi wa Serikali.

 

Nataka kuwahakikishia kuwa hali ya ukusanyaji wa mapato ni nzuri. Katika robo ya mwisho ya mwaka 2020/2021 yaani kuanzia Aprili hadi Juni 2021 hali ya ukusanyaji wa mapato ilikuwa wastani wa Shilingi Trilioni 4.41 sawa na wastani wa shilingi Trilioni 1.51 kwa mwezi. Na mwezi Juni ambao ni mwezi wa mwisho wa mwaka makusanyo yalipanda hadi kufikia shilingi Trilioni 1.85.

 

Serikali inawashukuru na kuwapongeza Watanzania wote kwa kulipa kodi na inawasihi kuendelea kufanya hivyo kwa kuwa kodi hizi ndizo zinajenga barabara, zinanunua dawa hospitali na katika vituo vyote vya tiba, inagharamia elimu bila malipo katika shule za msingi na Sekondari na ndio inapeleka maji na umeme vijijini.

 

9.   Hali ya Ukusanyaji wa Mapato katika Halmshauri.

Halmashauri zetu zimeendelea kukusanya mapato ambayo pia hutumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Katika mwaka 2020/2021 halmashauri zimekusanya shulingi Bilioni 757 ambayo ni asilimia 93 ya malengo ya kukusanya shilingi Bilioni 815. Fedha hizo ni ongezeko la shilingi Bilioni 40 ikilinganishwa na mwaka 2019/2020.

 

Serikali imeshatoa maelekezo kwa halmashauri zote ambazo mapato yake ni chini ya shilingi Bilioni 5 kuhakikisha asilimia 40 ya mapato hayo yanaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi, na kwa halmashauri ambazo mapato yake yanazidi shilingi Bilioni 5 kuhakikisha asilimia 60 ya mapato yake yanaelekezwa katika miradi ya maendeleo.

 

10.               Kuhusu Tozo ya miamala ya simu.

Natambua kuwa jambo hili ndilo limetawala vinywa vya Watanzania wengine. Serikali imesikia madai ya wananchi na baada ya Mhe. Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo ya kufanyiwa kazi kwa madai hayo kwa Mawaziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile, Mawaziri hawa wamekutana na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanyia kazi jambo hili.

 

Ndugu zangu waandishi wa habari napenda kuwajulisha kuwa jana Jumamosi Waheshimiwa Mawaziri wamekutana na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kwa ajili ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais.

 

Baada ya kupokea taarifa hiyo Mhe. Waziri Mkuu ametoa maelekezo mengine ya kuboresha zaidi taarifa ya Waheshimiwa Mawaziri ili hatimaye madai ya wananchi ya zingatiwe na miradi ya wananchi ambayo inapaswa kutekelezwa kutokana na fedha zilizopangwa kukusanywa katika tozo hizo itekelezwe.

 

Napenda kusisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha inaongeza nguvu katika kukabiliana na matatizo ya hali mbaya za barabara hasa vijijini, kujenga vituo vya afya, hospitali, zahanati, kupeleka maji na huduma nyingine za kijamii.

 

11.               Sekta ya Madini.

Serikali imeendelea kusimamia vizuri sekta ya madini ambayo imepiga hatua kubwa katika miaka mitano iliyopita. Kama mnavyojua katika kipindi hicho mapato ya madini yamepanda kutoka shilingi Bilioni 191 kwa mwaka hadi kufikia shilingi Bilioni 584 katika mwaka uliopita wa 2020/2021.

 

Sitaki kurudia mambo mengi ambayo yamefanyika katika sekta hii lakini naomba niwajulishe kuwa katika mwezi Juni uliopita nchi yetu imeandika historia nyingine kubwa katika sekta ya madini kwa kutoa leseni kubwa mbili za migodi ya madini.

 

Tumetoa leseni kubwa ya mgodi wa madini wa Nyanzaga uliopo Sengerema Mkoani Mwanza na tumetoa leseni kubwa ya madini adimu (Rare Earth Elements) kule Songwe.

 

Zinaitwa leseni kubwa kwa sababu uwekezaji kwenye kila mgodi ni zaidi ya Dola za Marekani Milioni 100 (sawa na zaidi ya shilingi Trilioni 2.3). Migodi hii kila mmoja utaajiri zaidi ya watu 1,000.

 

Kwenye ule mgodi mkubwa wa Songwe pia kutakuwa na mradi mwingine wa kujenga kiwanda cha kusafisha hayo madini adimu (rare earth elements) hiki nacho kitajengwa hapa hapa Tanzania na kinatarajiwa kuongeza mahitaji ya tindikali ambayo inatumika katika usafishaji. Kwa hiyo wazalishaji wa tindikali dili hilo limekuja kazi kwenu.

 

Lakini mkumbuke sheria yetu ya madini inaipa Serikali umiliki wa asilimia 16 ya migodi hii na bado itakusanya kodi na tozo mbalimbali. Ndio maana tunasema huu ni ushindi mwingine mkubwa katika sekta ya madini.

 

 

12.               Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Kuna kazi kubwa inaendeleza mkongo wa Taifa.

Kama mnavyojua mkongo wetu wenye urefu wa kilometa 8,319 umeunganishwa katika Mikoa yote, na sasa kazi inayoendelea ni ya kuunganisha wilaya zote.

 

Tumefanikiwa kufikisha huduma za mkongo wetu katika nchi zinazotuzunguka ambazo ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia, Malawi na sasa tunaekea kupeleka mkongo katika nchi za Msumbiji na Kongo.

 

Kwa kutambua umuhimu huu katika bajeti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, safari hii Serikali imeongeza bajeti katika Wizara hii ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutoka shilingi Bilioni 15 hadi Bilioni 240.

 

Tunataka kujikita zaidi katika eneo hili ambalo lina fursa nyingi za kutuletea mapato na kuzalisha ajira kwa Watanzania wengi. Kwa hivi sasa kazi kubwa inayoendelea kuendelea kuboresha mazingira kwa kupunguza urasimu, na jana mmeona TCRA imezindua mfumo wa kidijitali kwa ajili ya kuchakata maombi ya leseni. Mfumo huu utapunguza muda wa kuomba leseni kubwa na sasa leseni kubwa itapatikana ndani ya siku 45 na leseni ndogo itakuchukua siku zisizozidi 5.

 

13.               Usafiri wa anga.

Serikali imeendelea kuimarisha usafiri wa anga kwa kuchukua hatua kadhaa wa kadhaa za kukamilisha miundombinu ikiwemo viwanja vya ndege 11 vinavyojengwa na kukarabatiwa. Katika robo ya mwisho iliyopita shilingi Bilioni 8.6 zimetolewa katika eneo hili na kazi zinaendelea kukamilishwa.

 

Serikali imelipa fedha za ununuzi wa ndege kiasi cha shilingi Bilioni 38.437 moja kati ya ndege 3 zilizonunuliwa mmeiona jana imepokelewa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na ile ndege inaitwa De Havilland Canada – 8 (DHC-8). Ndege hizo haziitwi tena Bombardier Dash 8 Q400 kwa sababu kiwanda hicho sasa kimeuzwa kwa mmiliki mwingine.

 

Lakini ndege nyingine 2 za aina ya Airbus (A220-300) hizo zitafika wakati wowote kabla ya kuisha kwa mwaka huu. Mambo ni moto…….

 

 

 

14.                Sekta ya Kilimo.

Juhudi mbalimbali zinaendelea. Mojawapo kwa sasa ni kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa bei ya mbolea, tayari Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imechukua hatua ya kukutana na wafanyabiashara wa mbolea. Moja kati ya hatua ilizochukua ni kuondoa utaratibu wa watu wachache kuagiza mbolea na badala yake imeruhusu muagizaji wa mbolea yeyoye kuleta mbolea ilimradi iwe bora kwa uthibitisho wa Mamlaka yetu ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) na Shirika la Viwango (TBS).

 

Lakini tungependa wananchi wajue kuwa kupanda kwa bei ya mbolea kunakotokea sasa kwa sehemu kubwa kumesababishwa na kupanda kwa bidhaa hiyo katika masoko ya dunia. Tangu kulipuka kwa ugonjwa wa Korona ziko baadhi ya nchi ambazo ziliamua kujifungia (Lockdown) na zikaacha kuzalisha mazao ya kilimo. Matokeo yake ni kuwa hata viwanda vilisitisha uzalishaji wa mbolea. Sasa baada ya kuondoa lockdown wakulima wamerudi mashambani mahitaji ya mbolea yamepanda ghafla na mbolea imepanda bei.

 

Matarajio yetu ni kuwa hatua ambazo zimechukuliwa na Wizara ya Kilimo kuondoa urasimu na ucheleweshaji wa mbolea pale bandarini zitasaidia kupunguza bei.

 

Habari njema katika eneo hili ni kuwa mwekezaji Aliko Dangote yule aliyejenga kiwanda cha Saruji kule Mtwara ambako amewekeza zaidi ya Dola za Marekani Milioni 770 (Sawa na zaidi ya Trilioni 1.7) ameahidi kujenga kiwanda cha kuzalisha mbolea, na pia kuna wawekezaji kutoka Burundi (Kampuni ya Intracom) wameahidi kujenga kiwanda cha kuzalisha mbolea bila kutumia kemikali Jijini Dodoma kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha tani laki 5 kwa mwaka. Na ukichanganya na mbolea yetu ya Minjingu, mambo yatakaa sawa.

 

15.               Katika Sekta ya Michezo.

Tunafanya vizuri katika michezo.

 

Juzi wote mmeona timu yetu Taifa ya vijana chini ya miaka 23 imeibuka mabingwa wa CECAFA 2021 kule Ethiopia. Timu hii inarejea mchana hu una Mhe. Innocent Bashungwa Waziri wetu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amewaandalia vijana chakula cha mchana ambacho atakula nao na kuwapa neno la pongezi.

 

Tumeanza kuondokana na ombaomba katika kuendeleza michezo, Serikali ya Awamu ya 6 imeanza kutoa fedha kupitia mfuko wa maendeleo ya michezo uliopo BMT. Kuna fedha ambazo huenda hazina kutoka michezo ya kubashiri, sasa Serikali imekubali asilimia 5 ya fedha hizo zipelekwe kwenye mfuko wa kuendeleza michezo.

 

Pia Serikali imeondoa VAT katika nyasi bandia, ili kuondoa gharama kubwa katika nyasi na hivyo kuchochea uboreshaji wa miundombinu ya michezo.

 

Serikali imefufua michuano ya UMITASHUMITA na UMISETA, ambayo mwaka huu imefanyika Kitaifa Mkoani Mtwara. Na Wizara yenye dhamana ya Michezo imeamua kunogesha mashindano haya kwa kuwahusisha wasanii na wote mmeona jinsi mambo yalivyokuwa kule Mtwara.

 

Tumeunda kamati ya Kitaifa ya kurudisha TAIFA CUP na imeanza kazi tayari. Tunataraji michuano hii itafanyika mwaka huu.

16.                       ..

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...