Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab amefungua warsha kwa maafisa wa Serikali wanaoshiriki zoezi la uwekaji gharama katika mpango mkakati elekezi wa maendeleo wa kanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Africa SADC – RISDP ( Regional Indicative Strategic Development Plan 2020 - 2030).

Warsha hiyo inayoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni mratibu wa masuala ya kikanda kitaifa imeanza leo tarehe 15 hadi 22 Septemba, 2021 mjini Morogoro. Pia imehudhuriwa na maafisa kutoka wizara zinazosimamia sekta za vipaumbele zilizoainishwa katika Mkataba wa SADC wa mwaka 1992.

Sekta hizo ni pamoja na; Amani, Usalama na Utawala Bora; Maendeleo ya Viwanda na Mtangamano wa Masoko; Maendeleo ya Miundombinu katika kusaidia Mtangamano wa Kikanda; Maendeleo ya Jamii na Watu; Jinsia, Vijana, Mazingira na Mabadiliko ya Tabia nchi na Usimamizi wa hatari ya Maafa; na Usimamizi wa kimkakati wa Mpango Mkakati Elekezi wa Maendeleo wa Kanda.

“Nimeelezwa kuwa Warsha hii inajumuisha sekta mbalimbali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa zile zinazohusika moja kwa moja na utekelezaji wa itifaki na sera mbalimbali za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika. Ni faraja kuona mpo katika ari kubwa kwa ajili ya kuikamilisha kazi hii muhimu, hivyo mkaweke mbele maslahi ya Taifa wakati wa kupanga gharama kwenye maeneo husika.” Alisema Balozi Fatma

Lengo kuu la mpango huu ni kuimarisha ushirikiano katika Kanda kwa ajili ya kuharakisha juhudi za kupunguza umaskini na hatimaye kufikia malengo ya maendeleo ya kiuchumi na yasiyo ya kiuchumi. Mpango huu mpya umekuja baada ya ule wa awali wa mwaka 2015 – 2020 kumalizika muda wake. Kimsingi mpango huu mpya umetokana na Dira ya SADC ya mwaka 2020 - 2030 (Vision 2050)

Kadhalika, Balozi Fatma alitumia fursa hiyo kuwashukuru Shirika la Ujerumani (GIZ) kwa kukubali kufadhili shughuli hii na akawaahidi kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano kwenye programu na miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini na kikanda.

Zoezi hili linafanyika kufuatia maelekezo ya Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Mendeleo kusini mwa Africa (SADC) uliofanyika mwezi Agosti 2021 Lilongwe, Malawi. Mkutano huo ulizitaka nchi wanachama kukamilisha zoezi hilo na kuwasilisha maoni yao kwa Sekretarieti ya SADC kabla ya tarehe 30 Septemba 2021.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akizungumza wakati wa Hafla ya Ufunguzi wa Warsha ya Kitaifa ya Uwekaji Gharama katika mkakati elekezi wa maendeleo wa kanda ya SADC - RISDP 2020 -2030 inayofanyika kuanzia tarehe 15 hadi 22 Septemba 2021 mjini Morogoro

Mshauri Elekezi ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika, Dkt. Tumaini Katunzi akifuatilia hotuba ya ufunguzi.

Balozi Fatma akiteta jambo na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola na Afisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Khalifa Kondo.
Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Joshua Mponera akielezea ratiba ya warsha kwa washiriki wakati wa ufunguzi.
Washiriki wakifuatilia ufunguzi wa warsha hiyo.

Washiriki wakifuatilia ufunguzi wa warsha.

Washiriki wakifuatilia ufunguzi wa warsha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...