Pichani Matthew Luhanga ( kulia) na Mark Mwandosya wakiwa maprofesa wa uhandisi, Chuo Kuu cha Dar es SalaamNimeombwa na familia ya Matthew Laban Pimpa Thompson Alfred Luhanga niongee
machache kwa niaba yao kama ni njia ya kutoa shukrani kwa kadamnasi hii na wote mliohusika kwa njia mbalimbali kuifariji familia katika kipindi hiki kigumu. Ni kweli nimeombwa lakini nami pia nilitaa iwe hivyo, ili nitumie nafasi hii, ukumbi huu, mahala hapa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili niweze kumuaga ndugu na rafiki wa karibu, profesa mwenzangu wa teknolojia ya umeme, elektroniki na mawasiliano, mwanafunzi mwenzangu, mhandisi mwenzangu, mwandishi mwenzangu na Jirani yangu. Nafanya hivyo kwa niaba ya familia yangu, mke wangu Lucy, vijana wetu; Max, Sekela na Emmanuel, na ukoo wote wa Mwandosya na wa Magombe, walio hai na waliotutangulia mbele ya haki.

Nimezoea kutoa mihadhara  kama mwalimu hapa, na kwenye vyuo vikuu vingine. Kama mtumishi wa umma nimehutubia mikutano mbalimbali, na maeneo mbali mbali nchini na duniani kote. Nakiri kwamba hakuna uzoefu unaokutayarisha kutoa salaam za kuomboleza na shukrani, hasa pale ambapo anayekutoka alikuwa mtu wa karibu sana. Nitajitahidi, na nikiazima maneno ya Mark Anthony alipotoa salaam zake katika maziko ya Juliasi Kaisari, “Ndugu wanazuoni naomba masikio yenu”, nikimaanisha, “naomba mnivumilie”.

Aliyesoma wasifu wa Matthew amefanya kazi nzuri sana na  kwa umahiri mkubwa. Amenirahisishia kazi yangu. Amejibu swali kuu linaloulizwa na litaendelea kuulizwa, “Profesa Matthew Luhanga alikuwa nani hasa?” Lakini wengi pia wameniuliza, "Profesa Mwandosya, ukaribu wako na Profesa Luhanga umeanzia wapi?" Maelezo yangu ni mafupi, na yatajikita katika yale mambo ambayo hayaandikwi katika wasifu, lakini ambayo kwayo yametufanya mimi na yeye, na familia zetu kuwa karibu. Ni mchanganyiko wa bahati, hatima na matukio ambayo sio rahisi kujua chanzo chake. Wakati mwingine nadiriki kusema ni ya kiroho zaidi.

Niliingia darasa la tisa (kidato cha kwanza) Shule ya Sekondari ya Serikali Malangali mwaka 1965, wanafunzi wa kidato cha kwanza tukiitwa Mugya. Hapo nilimkuta Matthew akiwa darasa la 10 (kidato cha pili). Hawa vijana wa kidato cha pili walituendesha vilivyo, mithili ya magaidi. Hata hivyo Matthew alikuwa mstaarabu katika kundi hilo. Tukajenga urafiki kwa sababu mbili. Mosi, wote tulikuwa tunatoka Mbeya mjini, na pili tulikuwa na uwezo mkubwa wa masomo yote ikiwa ni pamoja na somo la hisabati. Kuhusu hisabati, yeye, akiwa kidato cha pili, na mimi nikiwa kidato cha kwanza, tulikuwa tunawasaidia wanafunzi wa kidato cha tatu katika somo la hisabati, ikiwa ni pamoja na somo la hisabati ziada (additional mathematics).

Mwaka juzi,  Ambangile Mwakilembe, mmoja wa walimu wetu wa Malangali alikuja kunitembelea kijijini, Lufilyo, Busokelo. Akanikumbusha jinsi Matthew na mimi tulivyoweza kugundua makosa katika kitabu cha hisabati cha Durell na kupelekea masahihisho katika makala zilizofuata. Na nakumbuka siku moja, Matthew akiwa kidato cha nne na mimi cha tatu, Mwalimu Mkuu, Alexander Thobias Mabele, marehemu baba ya mwenzetu Profesa Robert Mabele, akaitisha mkutuno wa wanafunzi na walimu. Akasema alikuwa na neno moja tu, nalo ni kwamba Malangali ilikuwa na bahati ya kuwa na wanafunzi wawili wenye vipaji vya hali ya juu. Kila mtu akatega masikio Mwalimu Mabele angesema nini. “Na wanafunzi hao ni Matthew Luhanga na Mark Mwandosya”. Akafunga mkutano akituacha na butwaa. Lakini mimi nilihisi alimlenga zaidi Matthew.

Alipomaliza kidato cha nne, Matthew akachaguliwa kwenda Chuo cha Ufundi cha Dar es Salaam (DarTech) ili yeye na wenzake waanzishe kidato cha tano, mchepuo wa Hisabati, Hisabati, Fizikia (Pure Mathematics, Applied Mathematics, Physics-PMM), mchepuo ambao ulilenga katika kutayarisha vijana kwenda vyuo vikuu kusomea uhandisi. Nilimkuta Matthew DarTech mwaka 1969 nilipochaguliwa kuingia hapo kuchukua mchepuo huo wa PMM. Alipomaliza kidato cha sita, Matthew alijiunga na Chuo Kikuu cha California Polytechnic kusomea shahada ya kwanza ya uhandisi umeme, na elektroniki na kufuzu kwa kiwango cha juu kabisa (suma cum laude). Akaendelea hapo hapo na kupata shahada ya uzamili (Masters). Nami nilipohitimu kidato cha sita, nikapata udhamini wa kwenda kusomea uhandisi umeme, Chuo Kikuu cha Aston, Uingereza. Nilipofuzu na kupata shahada ya kwanza, daraja la kwanza (first class honours), nikaenda Chuo Kikuu cha Birmingham moja kwa moja kufanya utafiti na kuhitimu shahada ya uzamivu (udaktari wa falsafa) katika fani ya umeme na teknolojia ya elektroniki baada ya miaka miwili na nusu.

Aliporudi kutoka Marekani, Matthew akawa mkufunzi DarTech, kama sharti la ufadhili wake kwenda Marekani lilivyomtaka. Nami nilipomaliza masomo yangu nikaja kuwa mhadhiri, idara ya umeme, kitivo cha uhandisi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Akiwa DarTech, na mimi nikiwa UDSM, mimi na Lucy tulipofunga ndoa, Matthew na mkewe Stephania (sasa ni marehemu na apumzike kwa amani) ndio waliosimamia ndoa yetu. Hatukuwa na magari ya binafsi enzi hizo. Tulipanda UDA kutoka hapa Chuo Kikuu kwenda kufunga ndoa. Tukapanda UDA tena baada ya kufunga ndoa kwenda kwa akina Matthew hapo DarTech kwa ajili ya chakula cha mchana. Baada ya hapo sisi tukarudi Barabara ya Kileleni Namba 25. Gharama za harusi hazikuzidi shilingi mia tano.

Ilikuwaje Matthew akaja kuwa mhadhiri, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam? Kuna wakati nilikaimu kama Mkuu wa Idara ya Umeme, Kitivo cha Uhandisi. Moja ya majukumu yangu ilikuwa ni kutafuta na kuwashawishi watu wenye uwezo  wajiunge na idara kama wahadhiri. Nilipomshauri Matthew, na alipokubali, ndipo nilipomuendea Profesa Awadhi Sadiki Mawenya, aliyekuwa Mtanzania wa kwanza kuwa Mkuu wa Kitivo Cha Uhandisi, na kumwomba akubali tuanze mchakato wa kumhamsha Matthew kutoka DarTech kuja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.  Profesa Mawenya akakubali kuchukua jukumu hilo na akaomba ridhaa ya Ndugu Ibrahim Kaduma, aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Naye akakubali. Wizara ya Elimu walionesha ugumu kumruhusu ahamie Chuo Kikuu. Nikachukua jukumu la kumwona aliyekuwa Waziri wa Elimu, nadhani alikuwa Mheshiwa Nicholas Kuhanga. Waziri akamuagiza Katibu Mkuu atoe kibali husika mara moja. Na kama wahenga walivyosema, yaliyofuata sasa ni historia.

Baada ya Malangali na DarTech kama wanafunzi, tukaja kukutana tena Kitivo cha Uhandisi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama wahadhiri. Tukakutana tena Marekani mwaka 1983 yeye akiwa Chuo Kikuu cha Columbia, New York, akisomea shahada ya uzamivu, na mimi nikiwa ‘sabathical leave’ Chuo Kikuu cha Princeton, New Jersey. Tuliporudi kutoka Marekani, baada ya muda mfupi mimi nikateuliwa kuwa Kamishna wa Nishati na Petroli, baadaye Katibu Mkuu, halafu Waziri na baadaye  Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya mwanzilishi. Yeye akaendelea na utumishi wa Chuo Kikuu. Akateuliwa kuwa Afisa Mkuu Taaluma na baadaye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Tukiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na hata baada ya mimi kuazimwa na hatimaye kuhamia serikalini, kwa pamoja tumetoa machapisho kadhaa yaliyotoka katika majarida ya kutaaluma humu nchini na nje ya nchi. Nilikuwa napitia wasifu wake nikaishia machapisho 75 na vitabu nane.  Vinne kati ya hivyo vitabu nane, tumeandika pamoja katika fani za uhandisi, nishati na mazingira, hususan mabadiliko ya tabianchi. Suala la mabadiliko ya tabia nchi sasa linazungumzwa sana duniani. Sisi tulilifanyia utafiti miaka 30 iliyopita!

Matthew na mimi tulianza uandishi wa pamoja zamani. Mwaka 1970 tuliandika makala kuhusu umuhimu wa Tanzania kuwa na wahandisi wanawake. Makala hiyo ilichapishwa na The Standard, gazeti la serikali chini ya kichwa 'Why No Women Engineer?' Makala hiyo ilitoka tarehe 10 Julai 1970, ikawa makala bora ya wiki na tukapata zawadi ya shilingi 10. Chapisho la pamoja ni la hivi majuzi. Miezi michache iliyopita yeye na mimi tukiwa waandishi wenza, tumechapisha andiko kuhusu, “Blockchain: A Disruptive and Transformative Technology of the Fourth Industrial Revolution”, andiko ambalo limechapishwa na jarida la kitaaluma la Shule ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (University of Dares Salaam Business Management Review).

Profesa Luhanga ndiye aliyeishauri Idara ya Umeme, Kitivo cha Uhandisi ianzishe Kigoda cha Kiprofesa cha Usimamizi wa Nishati na Teknolojia, kigoda cha kwanza kuanzishwa UDSM ambacho nilibahatika kukikalia. Kilipoanzishwa kigoda cha teknolojia na usimamizi wa mawasiliano, Profesa Luhanga akawa profesa wa kigoda hicho. Profesa Luhanga ndiye aliyewezesha kupatikana kwa eneo linalotumika na Chuo cha Teknolojia za Habari na Mawasiliano cha UDSM, kilicho Kijitonyama, baada ya aliyekuwa Waziri mwenye dhamana ya sekta ya mawasiliano (jina nalihifadhi), kumshauri aiombe serikali ili UDSM ipewe eneo hilo.

Lakini Profesa Luhanga atakumbukwa zaidi kwa kubuni na kutekeleza kimkakati, na kwa ufanisi na mkubwa, Mageuzi ya Kitaasisi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (University of Dar es Salaam Institutional Transformation Programme). Mpango huo uliongeza ufanisi katika utendaji kazi, ulipanua wigo na kuongeza udahili wa wanafunzi. Ulileta matumizi bora ya majengo na kuongeza miondombinu; na ulifanikiwa kuleta uwiano mzuri wa kijinsia katika udahili. Wote tumeshuhudia matokeo chanya ya mabadiliko hayo.

Moja ya mambo ambayo hayajulikani sana ni kwamba Profesa Luhanga alikuwa, pamoja na Profesa Mawenya, Ndugu Enock Kamuzora, Mhandisi Salema, Ndugu Ibrahim Kaduma na sisi wengine, tulianzisha kikundi cha kubuni mbinu na mikakati ya kuzuia rushwa katika sekta ya uhandisi na ujenzi (FACEIT-Front Against Corruption in Engineering in Tanzania). Hii ilikuwa hata kabla ya Tume ya Warioba.

Mambo mengine yalikuwa si rahisi kuyaelewa yalivyotokea. Baruany Elijah Luhanga, kaka yake Matthew, ambaye alituchemsha sana tukiwa ’mugya’ Malangali, ndiye aliyenikaribisha Uingereza akiwa Mwanafunzi wa uhandisi wa elektroniki Chuo Kikuu cha Liverpool, Uingereza, mimi nilipokwenda Aston. Tukaja kukutana tena yeye akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, mimi nikiwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini. Jambo ambalo lilistaajabisha familia zetu ni pale ambapo mama yao akina Luhanga, Mama Edith Talina Nyaukandawire, na baba yetu sisi, Mzee Isaac Mwandosya, walipofariki siku moja hapa Dar es Salaam mwaka1995. Tukawa na misiba miwili na misafara miwili ya kwenda kuzika huko Mbeya.

Nilipokuwa nafundisha 'Control Theory EE441', kipindi kilikuwa cha dakika 50. Ikifika dakika 40 baadhi ya wanafunzi walikuwa wanaanza kupiga miayo. Nikiwauliza, “Kwanini?” Wanasema, “Njaa Profesa”. Nisingependa baadhi yenu muanze kupiga miayo.

Hivyo basi, nimalizie kama nilivyoanza, na kama nilivyoombwa, kwa kuwashukuru wote mliokuja kumsindikiza ndugu yetu Profesa Matthew Luhanga, au, Uncle Matthew, kama watoto wetu wanavyomfahamu. Tunawashukuru madaktari, wauguzi na wengine wote waliomhudumia Uncle Matthew hapa nchini na huko India.

Tunatambua na kuheshimu uwakilishi wa serikali kati yetu. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amewakilishwa na Profesa Kitila Mkumbo, profesa mwenzetu na Waziri wa Viwanda na Biashara. Uwepo wa Profesa Mdoe kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia umetupa faraja.

Tunamshukuru Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Mheshimiwa Jaji Damian Lubuva, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Profesa William Anangisye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ndugu Nicholas Kuhanga, ambaye amewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, aliyemfuata Profesa Luhanga kama Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, uongozi wote na jumuiya ya Chuo Kikuu kwa kumuaga Profesa Luhanga kwa heshima anayostahili. Tunawashukuru pia Chuo Kikuu cha Mzumbe, ambako Matthew alikuwa Mwenyekiti wa Baraza. Chuo hicho kimemuaga Profesa Luhanga vilivyo. Tunamshukuru Mheshimiwa Dr Ali Mohamed Shein, Mkuu wa Chuo na Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; Mheshmiwa  Barnabas Samata Jaji Mkuu Mstaafu, aliyekuwa Mkuu wa Chuo; Profesa Lughano Kusiluka, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu; na jumuiya ya Chuo Kikuu cha Mzumbe.  Chuo Kikuu cha Mzumbe, tunawashukuru sana kwa kuchangia jeneza, gharama za kaburi na nyinginezo. Tunamshukuru pia Mheshimiwa Joseph Sinde Warioba, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Uongozi na jumuiya za Chuo Kikuu cha Ardhi, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili na vyuo vingine.  Natambua pia uwepo wa Profesa Anna Tibaijuka aliyekuwa Mbunge mwenzangu na Waziri mwenzangu, na aliyekuwa Mkuu wa shirika la HABITAT la Umoja wa Mataifa.

Mwisho, lakini sio kwa umuhimu, tunamshukuru Baba Padri Dr Rev. Joseph Mosha, Baba Paroko wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wana parokia wote kwa kuongoza misa ya maziko ya Profesa Luhanga. Asante sana.

Tunazishukuru taasisi na wale wote mliochangia kwa hali na mali katika msiba huu ambao hatima yake ni maziko ya yule ambaye wenzetu wa Kenya wanamwita ‘Mwendazake’ yatakayofanyika kesho jumanne tarehe 21 Septemba 2021 katika makaburi ya Kondo, Tegeta.

Profesa Luhanga ameacha mke, Columba Namkamba, na watoto watatu; Edith, Thompson, na Jeremiah. Ameacha pia wajukuu wawili, Miriam na Abigaeli. Aidha Matthew na familia yake wamelea watoto na wajukuu wengi wa ndugu zao.

Sisi tumekuwa majirani na familia ya Matthew pale Tegeta, Kadenge, aliyekuwa mhudumu wetu, ilikuwa akimuona Profesa Luhanga anaingia nyumbani kwake alikuwa ananitaarifu, "Profesa Luhanga amefika. Ameingia nyumbani kwake na madigrii yake", akimaanisha amebeba vitabu. Watoto na wajukuu, yatumieni madigrii ya Profesa Luhanga.

Hatujaja kumlilia Matthew. Hapana. Tunasherehekea maisha ya mtu mwenye kipaji na uwezo mkubwa, aliyekuwa mpenda watu na mcheshi, aliyejaliwa busara, hekima, na nidhamu ya hali ya juu, na mzalendo aliyetoa mchango mkubwa kitaaluma na katika maendeleo ya elimu.

Nahitimisha kwa kusema kwamba pamoja na sifa zote, Profesa Luhanga alikuwa binadamu. Lazima katka maisha yake atakuwa amewakwaza baadhi yenu. Kwa hayo tunaomba, tena kwa unyenyekevu mkuu, mumsamehe.

Raha ya Milele Umpe ee Bwana, na Mwanga wa Milele Umwangazie. Apumzike kwa Amani.

Asanteni sana. Mbarikiwe sana.

Mark Mwandosya
Jumanne 21 Septemba 2021
 
Kwaheri Profesa Matthew Laban Pimpa Luhanga

Nimeombwa na familia ya Matthew Laban Pimpa Thompson Alfred Luhanga niongee

Mambo mengine yalikuwa si rahisi kuyaelewa yalivyotokea. Baruany Elijah Luhanga, kaka yake Matthew, ambaye alituchemsha sana tukiwa ’mugya’ Malangali, ndiye aliyenikaribisha Uingereza akiwa Mwanafunzi wa uhandisi wa elektroniki Chuo Kikuu cha Liverpool, Uingereza, mimi nilipokwenda Aston. Tukaja kukutana tena yeye akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, mimi nikiwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini. Jambo ambalo lilistaajabisha familia zetu ni pale ambapo mama yao akina Luhanga, Mama Edith Talina Nyamkandawire, na baba yetu sisi, Mzee Isaac Mwandosya, walipofariki siku moja hapa Dar es Salaam mwaka1995. Tukawa na misiba miwili na misafara miwili ya kwenda kuzika huko Mbeya.

Nilipokuwa nafundisha 'Control Theory EE441', kipindi kilikuwa cha dakika 50. Ikifika dakika 40 baadhi ya wanafunzi walikuwa wanaanza kupiga miayo. Nikiwauliza, “Kwanini?” Wanasema, “Njaa Profesa”. Nisingependa baadhi yenu muanze kupiga miayo.

Hivyo basi, nimalizie kama nilivyoanza, na kama nilivyoombwa, kwa kuwashukuru wote mliokuja kumsindikiza ndugu yetu Profesa Matthew Luhanga, au, Uncle Matthew, kama watoto wetu wanavyomfahamu. Tunawashukuru madaktari, wauguzi na wengine wote waliomhudumia Uncle Matthew hapa nchini na huko India.

Tunatambua na kuheshimu uwakilishi wa serikali kati yetu. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amewakilishwa na Profesa Kitila Mkumbo, profesa mwenzetu na Waziri wa Viwanda na Biashara. Uwepo wa Profesa Mdoe kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia umetupa faraja.

Tunamshukuru Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Mheshimiwa Jaji Damian Lubuva, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Profesa William Anangisye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ndugu Nicholas Kuhanga, ambaye amewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, aliyemfuata Profesa Luhanga kama Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, uongozi wote na jumuiya ya Chuo Kikuu kwa kumuaga Profesa Luhanga kwa heshima anayostahili. Tunawashukuru pia Chuo Kikuu cha Mzumbe, ambako Matthew alikuwa Mwenyekiti wa Baraza. Chuo hicho kimemuaga Profesa Luhanga vilivyo. Tunamshukuru Mheshimiwa Dr Ali Mohamed Shein, Mkuu wa Chuo na Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; Mheshmiwa  Barnabas Samata Jaji Mkuu Mstaafu, aliyekuwa Mkuu wa Chuo; Profesa Lughano Kusiluka, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu; na jumuiya ya Chuo Kikuu cha Mzumbe.  Chuo Kikuu cha Mzumbe, tunawashukuru sana kwa kuchangia jeneza, gharama za kaburi na nyinginezo. Tunamshukuru pia Mheshimiwa Joseph Sinde Warioba, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Uongozi na jumuiya za Chuo Kikuu cha Ardhi, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili na vyuo vingine.  Natambua pia uwepo wa Profesa Anna Tibaijuka aliyekuwa Mbunge mwenzangu na Waziri mwenzangu, na aliyekuwa Mkuu wa shirika la HABITAT la Umoja wa Mataifa.

Mwisho, lakini sio kwa umuhimu, tunamshukuru Baba Padri Dr Rev. Joseph Mosha, Baba Paroko wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wana parokia wote kwa kuongoza misa ya maziko ya Profesa Luhanga. Asante sana.

Tunazishukuru taasisi na wale wote mliochangia kwa hali na mali katika msiba huu ambao hatima yake ni maziko ya yule ambaye wenzetu wa Kenya wanamwita ‘Mwendazake’ yatakayofanyika kesho jumanne tarehe 21 Septemba 2021 katika makaburi ya Kondo, Tegeta.

Profesa Luhanga ameacha mke, Columba Namkamba, na watoto watatu; Edith, Thompson, na Jeremiah. Ameacha pia wajukuu wawili, Miriam na Abigaeli. Aidha Matthew na familia yake wamelea watoto na wajukuu wengi wa ndugu zao.

Sisi tumekuwa majirani na familia ya Matthew pale Tegeta, Kadenge, aliyekuwa mhudumu wetu, ilikuwa akimuona Profesa Luhanga anaingia nyumbani kwake alikuwa ananitaarifu, "Profesa Luhanga amefika. Ameingia nyumbani kwake na madigrii yake", akimaanisha amebeba vitabu. Watoto na wajukuu, yatumieni madigrii ya Profesa Luhanga.

Hatujaja kumlilia Matthew. Hapana. Tunasherehekea maisha ya mtu mwenye kipaji na uwezo mkubwa, aliyekuwa mpenda watu na mcheshi, aliyejaliwa busara, hekima, na nidhamu ya hali ya juu, na mzalendo aliyetoa mchango mkubwa kitaaluma na katika maendeleo ya elimu.

Nahitimisha kwa kusema kwamba pamoja na sifa zote, Profesa Luhanga alikuwa binadamu. Lazima katka maisha yake atakuwa amewakwaza baadhi yenu. Kwa hayo tunaomba, tena kwa unyenyekevu mkuu, mumsamehe.

Raha ya Milele Umpe ee Bwana, na Mwanga wa Milele Umwangazie. Apumzike kwa Amani.

Asanteni sana. Mbarikiwe sana.

Mark Mwandosya
Jumanne 21 Septemba 2021

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...