Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

PAZIA la Ligi Kuu Soka Tanzania Bara msimu wa 2021-2022 rasmi limefunguliwa kwa nyasi za viwanja mbalimbali nchini kuwaka moto huku vikishuhudiwa vicheko na vilio kwa timu zinashiriki Ligi hiyo, kuanza kwa ushindi na nyingine kupoteza.

Katika mchezo wa kwanza majira ya Saa 8 mchana ilishuhudiwa wageni wa Ligi hiyo, Mbeya Kwanza FC kutoka mkoani Mbeya wakipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wa Ligi hiyo Mtibwa Sugar katika uwanja wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani. Bao la Mbeya kwanza lilifungwa na Mchezaji, William Edgar katika dakika ya 49 akiweka rekodi ya kufunga bao la kwanza msimu huu.

Mchezo mwengine majira ya Saa 10 jioni, uliwakutanisha Namungo FC dhidi ya Geita Gold FC waliopanda Ligi Kuu msimu huu. Namungo waliwaadhibu Wachimba Madini wenzao wa Geita na kuondoka na ushindi wa bao 2-0 katika dimba la nyumbani kwa sasa, dimba la Ilulu lililopo mkoani Lindi. Mabao ya Namungo FC yalifungwa na Wachezaji, Shiza Kichuya dakika ya 14 na Reliant Lusajo dakika ya 81 ya mchezo huo.

Mchezo wa tatu, Wagosi wa Kaya, Coastal Union FC wenyeji wa uwanja wa CCM Mkwakwani mkoani Tanga wakilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC kutoka Chamazi, Dar es Salaam. Azam FC walianza kupata bao katika mchezo huo likifungwa na Beki Daniel Amoah dakika ya 49 na bao la kusawazisha la Coastal likifungwa na Hance Masoud dakika ya 90 ya mchezo.

Simba SC watakuwa ugenini Musoma uwanja wa Karume wakicheza na Biashara United Mara siku ya Jumanne wakati Yanga SC wakishuka siku ya Jumatano dhidi ya Kagera Sugar kwenye uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...