Na Edwin Moshi, Makete.


Ofisi ya Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Njombe Balozi Dkt. Pindi Chana kwa kushirikiana na Wakala wa Vipimo hapa nchini (WMA), wameendesha mafunzo ya matumizi sahihi ya vipimo yaliyofanyika wilayani Makete Mkoani hapo kwa lengo la kuhakikisha jamii inapata uelewa wa kutosha kuhusu matumizi sahihi ya vipimo

Mafunzo hayo yamefanyika Septemba 23, 2021 na kuhusisha viongozi na baadhi ya wananchi wakiwemo wakulima na wajasiriamali kutoka kata za wilaya ya Makete ambapo pamoja na mambo mengine limegusiwa suala la kuwepo kwa vifungashio nchi nzima vya mazao kama viazi ili kuepukana na rumbesa ambayo imetajwa kumnyonya mkulima

Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo, Mgeni rasmi katika mafunzo hayo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Makete Mh. Festo Sanga amesema serikali ina nia ya dhati ya kuleta matumizi sahihi ya vipimo kwenye kila eneo linalotakiwa kwa kuwa ina lengo la kuhakikisha kunakuwa na usawa baina ya muuzaji na mnunuzi ama mkulima na mfanyabishara

Amesema wakala wa vipimo watakapotoa mizani kwa ajili ya kupima mazao ya wakulima, mizani hizo ziende kwenye kila kijiji na wananchi washirikishwe ili kuona mizani hizo zinakaa wapi ili kusiwe na migogoro ya kuwafanya wauzaji kusafirisha mazao yao umbali mrefu kufuata huduma hiyo

“Kwa Afrika nzima na nchi hizi zinazotuzunguka ni Tanzania peke yake inayouza Viazi kwa kukadiria, wapo wafanyabiashara wanakuja kununua viazi kwa kukadiria lakini wanayapeleka kwenye nchi zao na kuyauza kwa vipimo, gunia alilolinunua hapa nchini akienda kuliuza nchini mwake anakuta ni gunia moja na nusu, anauza bei ya gunia moja na nusu alilolinunua huku kwetu bei ya gunia moja, hivyo yeye anapata faida na mkulima ananyonywa” amesema Mbunge Sanga

Naye Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Njombe Mh. Balozi Dkt Pindi Chana amesema suala la vipimo limetajwa katika ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya 2020 – 2025, ambapo takwimu zinaonesha vipimo sahihi visipozingatiwa serikali inakosa mapato na wananchi wake wakiwemo wakulima wananyonywa na kutofaidika na kilimo chao

Mbunge huyo amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa vipimo sahihi (mizani) ambapo itasaidia mkulima kuuza mazao yake na kupata fedha anazostahili huku pia mnunuzi akinunua kwa bei ya uhakika ambapo itasaidia serikali kukusanya ushuru sahihi pamoja na kuepusha uharibifu wa barabara ambao unatokana na magari kupakia mazao yenye uzito uliopitiliza uwezo wa barabara

“Ndugu zangu huu ndio muda wa kuondokana na kuuza na kupima kwa kutumia makopo, vikapu, madebe n.k, tukitumia vipimo sahihi kila mtu atapata anachostahili, barabara zetu hazitaharibika kwa kupakia mizigo kupita kiasi, halmashauri itakusanya mapato mengi na wakulima watapata fedha stahili ya mazao yao” amesema Mbunge Balozi Dkt. Pindi Chana

Jasel Mwamwala ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Njombe amekiri kuwepo kwa vipimo visivyo sahihi katia mkoa wa Njombe hivyo kuiomba serikali kuhakikisha vinapatikana vifungashio vya usawa mmoja nchi nzima ili kuwaokoa wakulima

Naye Hawa Kada ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Makete amewataka washiriki wa mafunzo hayo kwenda kuitoa elimu waliyoipata kwa wananchi wenzao ili mafunzo hayo yakawe na tija iliyokusudiwa

Meneja wa wakala wa vipimo mkoa wa Njombe Henry Msambila amesema kwa mikakati ambayo inapangwa, rumbesa itafutika kabisa huku akiiasa jamii kuona umuhimu wa kutumia vipimo sahihi na kuachana na makopo na ndoo

Amesema matumizi sahihi ya vipimo yanachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi, huku akikiri kuwepo kwa mafundi wachache wa mizani katika mkoa wa Njombe kitendo kinachochangia gharama za utengenezaji wa mizani kuwa juu hivyo kutoa rai kwa wanamakete wanaopenda kuwa mafundi kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwasiliana na ofisi ya wakala wa vipimo mkoa wa Njombe

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakiwemo wakulima na wajasiriamali wamezungumzia umuhimu wanaouona katika suala la vipimo sahihi ambapo Bw. Andrea Sanga ameshukuru kwa mafunzo hayo ambapo amekiri kuuona mwanga katika matumizi sahihi ya vipimo yatakavyoinua uchumi wa wakulima na taifa kwa ujumla.

Meneja wa wakala wa vipimo Mkoa wa Njombe Henry Msambila akizungumzia umuhimu wa matumizi ya vipimo sahihi
Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Njombe Balozi Dkt Pindi Chana akifafanua jambo kwenye mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya vipimo
Mbunge wa jimbo la Makete Mh. Festo Sanga ambaye ni mgeni rasmi katika mafunzo hayo akielezea namna wanavyoshirikiana na serikali ili suala la matumizi ya vipimo sahihi lifanikiwe
Baadhi ya washiriki wakifuatilia mafunzo hayo
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...