Meneja wa Kitengo cha Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Muungano Saguya akizungumza katika kikao kati ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma leo tarehe 21 Sept 2021 akiwa katika ziara ya siku tano mkoani Dodoma. 
(PICHA ZOTE NA HASSAN MABUYE WIZARA YA ARDHI)

Na Munir Shemweta, KONDOA

 

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limesema limeanza kufanya ukarabati wa nyumba zake katika maeneo mbalimbali nchini ili ziwe katika ubora.

 

Hayo yalibainishwa leo tarehe 21 Sept 2021 wilayani Kondoa mkoani Dodoma na Meneja wa Kitengo cha Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa Muungano Saguya  Dodoma wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa huo.

 

"Shirika letu la NHC lilianzishwa mwaka 1964 na sasa tumeanza kuzifanyia ukarabati  nyumba zetu katika maeneo mbalimbali zikiwemo zile za Dar es Salaam ambapo kuna asilimia 60 ya nyumba zote za shirika" alisema Saguya

 

Kwa mujibu wa Saguya, NHC ina takriban nyumba 18,000 nchi nzima zinazotumika kwa shughuli za biashara na makazi na ukarabati unaofanyika utasaidia nyumba hizo kuwa na ubora na muonekano mzuri wa kuvutia.

 

Hata hivyo, Meneja  huyo wa Kitengo cha Habari na uhusiano NHC aliongeza kuwa, pamoja na ukarabati wa nyumba zake unaoendelea  shirika la NHC linadai takriban shilingi  bilioni 26 kutoka kwa wapangaji wake na kuwataka wote wanaodaiwa kuhakikisha wanalipa madeni yao kwa wakati ili fedha hizo zitumike kuendesha miradi mingine ya Shirika.

 

Saguya alibainisha kwa kusema, Shirika la Nyumba la Taifa, kwa sasa linaendelea na miradi yake ya ujenzi wa nyumba za kuuza na zile za kupangisha kwenye mkoa wa Dodoma na sasa linakamilisha mradi wa nyumba 300 eneo la Iyumbu na nyumba 100 eneo la Chamwino.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema, katika kuwezesha ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kabla kuanza ujenzi shirika la  nyumba linatakiwa kufanya mawasiliano na taasisi kama TARURA, Maji na TANESCO ili   kusaidia uwezeshaji miundo mbinu katika eneo la mradi.

 

Alibainisha kuwa, NHC kwa sasa inajenga nyumba kwa wanaohitaji kulingana na chaguo la mteja hivyo ni fursa kwa halmashauri kulitumia shirika katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...