Yabainisha matokeo ya sensa yatasaidia katika kufikia uchumi wa bluu na kuimarisha usalama wa vyombo hivyo.

Na Chalila Kibuda,Michuzi Tv, Bagamoyo 

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kuanza kufanya sensa ya vyombo vidogo vya usafiri majini kwenye  maziwa, mito pamoja na bahari ili kujenga kanzidata ya vyombo vidogo vya usafiri na hivyo kuwezesha kupanga mipango ya maendeleo na kuimarisha usalama  katika sekta hiyo.

 Sensa hiyo itashirikisha  Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) pamoja na Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambapo sensa hiyo itaanza Oktoba Mosi hadi Oktoba 30 mwaka huu.

Akizungumza wakati wa semina ya siku mbili yenye lengo la kuwajengea uwezo maafisa uvuvi na maafisa wa TASAC, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TASAC ambaye ni  Mkurugenzi Udhibiti Uchumi wa Shirika hilo  Nahson Sigalla amesema sensa hiyo ya nchi nzima pamoja na mambo mengine imelenga kuinua maendeleo ya sekta hiyo kusaidia katika utungaji sera na udhibiti.

Amesema sensa hiyo pia itasaidia kuimarisha usalama kwa kulinda uhai na mali za watumiaji na wamiliki  wa vyombo hivyo nchini kote.

Sigalla amesema sensa ya vyombo hivyo itakayofanywa katika maeneo ya bahari, maziwa na mito itasaidia kutambua idadi ya vyombo hivyo na majukumu yake na baadae taarifa zake kuwekwa katika kanzidata maalumu.

"Tanzania inatekeleza uchumi wa bluu unaohusisha masuala yote ya uchumi wa bahari, kanzidata tunayoijenga  kupitia sensa hii itatuwezesha kubaini hatua za  kuchukua kufanikisha maendeleo na kutatua changamoto zinazokabili sekta hiyo" amesema Sigalla.

Aidha, amesema kwa kuzingatia utaratibu uliopo, sensa hiyo itavishirikisha vyombo vidogo vyenye urefu usiozidi urefu wa mita 24 au uwezo wa kubeba mizigo isiyozidi tani 50 katika maeneo yote ya ukanda wa bahari, maziwa na mito ambako huduma ya usafiri huo hutolewa.

Amesema pamoja na kusaidia kupanga mipango  ya kimaendeleo, sensa  ya vyombo hivyo pia itawasaidia wataalamu wa vyuo vya elimu ya juu  kufanya tafiti mbalimbali ikiwemo namna vyombo hivyo vinavyosaidia katika ukuaji wa maendeleo nchini na dhamira ya Serikali ya kukuza uchumi wa bluu.

Sigalla alisema dhima nyingine ya sensa hiyo imetokana na mahitaji ya upatikanaji wa taarifa kwa ajili ya kusaidia ukuaji wa maendeleo ya sekta hiyo muhimu kwa uchumi.

Mmoja wa walengwa wa mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa Uvuvi kutoka Mkoa wa Kagera Maengo Nchimani amesema matarajio mafunzo hayo yatawasaidia  kufanikisha malengo yaliyokusudiwa huku akiamini ujio wake ni muhimu katika kuharakisha maendeleo ya taifa. 

Nchimani amesema  kumekuwepo na vyombo vingi vinavyotoa huduma ya usafiri na ubebaji wa mizigo katika mito, maziwa na bahari huku akiwataka wamiliki wa vyombo hivyo kutoa ushirikiano wa dhati sensa itakapoanza.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Nahson Sigalla akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufunga mafunzo ya maafisa  uvuvi kwa ajili ya Sensa itakayoanza hivi karibuni kwa nchi nzima kwa vyombo vidogo vya majini.

Mshiriki wa Mafunzo Afisa Uvuvi Maengo Nchimani akizungumza kuhusiana  na mafunzo hayo namna watavyochukua sensa hiyo kwa kwa kisasa

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...