Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa akizungumza na Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya Taifa ya Biashara Elvis Ndunguru (mwenye suti ya kijivu) wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Nne ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayoendelea Mjini Geita. Benki hiyo imesema kwamba imepokea na kuanza kufanyia kazi kwa kutenga TSHs 20B maelekezo ya Waziri Mkuu ya kukopesha wachimbaji wadogo.
 

Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

SEKTA ya Madini nchini inachangia wastani wa asilimia 6.4 katika pato la taifa, hali inayoashiria umuhimu wa wake na kiashiria kinachosisitiza kuwa ipo haja kwa serikali, taasisi binafsi na wadau wa maendeleo ikiwemo mabenki kuhakikisha wanaweka nguvu ya pamoja kusaidia maendeleo ya sekta hii.

Miongoni mwa wadau wakubwa wa maendeleo nchini ni Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), miongoni mwa  taaasisi za kifedha imeonyesha dhamira ya dhati kuunga mkono uwekezaji katika sekta ya madini kwa imani ya kufikia mapinduzi ya kiuchumi kupitia madini.

Mkuu wa wilaya ya Geita, Wilson Shimo akiwakilisha viongozi wa serikali kwenye maeneo ya wachimbaji anazipongeza taasisi za fedha ikiwemo NBC kuitikia wito wa serikali na kuanza kuwasaidia wachimbaji wadogo, hali hiyo inatoa taswira ya mwelekeo rafiki kwenye sekta ya madini.

Shimo amekiri wazi benki nyingi zimeonyesha nia ya kuwakopesha wachimbaji lakini changamoto kubwa ni vigezo ndio maana hawakopesheki ingawa serikali inaendelea na mijadala kuwasaidia wachimbaji kujifunza waweze kukidhi vigezo na taasisi ziendelee kuwasaidia.

Shimo amewashauri  wachimbaji wadogo waungane na kuunda vikundi ili iwe rahisi kwao kukopesheka na kupata leseni ya uchimbaji pamoja na kuchimba katika maeneo rasmi kwani hivo itaweza kusaidia juhudi za serikali na taasisi binafsi kuzaa matunda.

Akizungumza katika viwanja vya maonyesho ya nne ya teknolojia ya madini mjini Geita, Meneja wa NBC kitengo cha biashara, Elvis Ndunguru amesema wao ni wadau wakubwa wa sekta ya madini ndio maana wameamua kudhamini maonyesho hayo.

Nduguru amesema,katika kukuza sekta ya madini NBC imeanza na madini ya dhahabu na imelenga ni kutengeneza mazingira rafiki katika mnyororo wa thamani katika biashara hiyo ambayo inahusisha wachimbaji wadogo, wafanyabiashara na watoa huduma kwenye madini na makampuni ya tafiti za madini

Aidha, kwa upande wa wachimbaji wadogo NBC imeamua kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wadogo Nchini (FEMATA) na Shirika la Kuendeleza Uchimbaji Mdogo (FADev) ambao wanatambua karibu mahitaji ya wachimbaji wadogo.

Nduguru amesema utafiti wao wa awali umebaini wachimbaji wengi wadogo hawatumii benki na kwa kuiona hilo wameanza kutoa mafunzo kuwaandaa wachimbaji waweze kuwa na sifa za kukopeseha na NBC itaanza kuchagua kama mfano wasaidiwe vifaa.

Amesema kuwa, kwa upande wa watoa huduma migodini NBC inaangalia zaidi walio na mikataba ya tenda za huduma na tayari wameshaanza kupatiwa mikopo na hadi sasa takribani makampuni 50 nchi nzima yamepatiwa mikopo unaokadiriwa kufikia bilioni 20, usio na riba na wenye mashariti nafuu. 

“Kwa wafanyabiashara tumewatengenezea mfumo ambao tunaifanya dhahabu yenyewe kama dhamana na ukiangalia mnyororo mzima tupo kuweza kusaidia kupiga hatua, lakini kwa wachimbaji kwa sasa ndio tunaaanza,”.

‘Tumeona tuanze na mafunzo kwa kuwa tuliona kuna uwazi kati ya wachimbaji wadogo na taasisi za kifedha na wengi walionekana hawapitishi pesa zao benki, na tumetenga bajeti ya kuanzia na tumeona tuanze na walau bilioni 20 kwa ajili ya wachimbaji wadogo,” amesema Elvis.

Meneja huyo wa NBC kitengo cha biashara amesema wameamua kujikita katika kukuza sekta ya madini kwa kuwa mchango wa sekta hii ni mkubwa kwenye pato la taifa na hata katika kuingiza pesa za kigeni.

“Kwa muda mrefu tulitegemea utalii, lakini toka Korona imetokea utalii umedolola na madini ndiyo yamegeuka muhimili mkubwa wa uchumi na kulipatia taifa fedha za kigeni, lakini tumevutiwa kwani serikali pia imechukua hatua stakihiki kuboresha sekta hii kwa kuamua kuanzisha masoko ya madini,” 

Hata hivyo, Amesema katika mradi wa NBC kwa kushirikiana na FADev na FEMATA wataanza kutoa mikopo ya vifaa na nyenzo zitakazowawezesha kufanya shughuli zao katika njia za kisasa zaidi ambayo itaongeza ufanisi na kipato na wapo tayari kutoa mikopo ya ununuzi wa vifaa zitakazopunguza athari ya mzingira. 

“Ukiangalia NBC ni wadau wakubwa wa mazingira, tunasisitiza wataalamu wa mazingira na wataalamu wa madini na kusaidia maeneo kama hayo, na tupo tayarii kuwezesha wachimbaji kumudu gharama ya kemikali mbadala ya zebaki ambayo ni hatari kwa mazingira na matumizi ya vyuma badala ya magogo,”

Nduguru ameeleza kuwa, kwa sasa ni mara ya nne mfululizo wanadhamini Maonyesho ya Teknolojia ya Madini mjini Geita lengo kubwa ni kutoa elimu kwa wadau wa madini hasa wachimbaji wadogo na kuhamasisha taasisi zingine kuunga mkono serikali na kupitia maonyesho hayo takribani watu 20,000 wataelimika.

Nduguru ametoa wito kwa wachimbaji kuendelea  kupata mafunzo kupitia kliniki za NBC ili ziweze kuwajengea uwezo wa utunzaji wa kumbukumbu za kifedha na biashara na waweze kukopesheka kwa urahisi na taasisi za kifedha  ziweze kuunga mkono juhudi za serikali katika kuendeleza sekta nyeti ya uchimbaji.

Akizungumzia mchango wa taasisi za kifedha ikiwemo NBC, katika kuendeleza uchimbaji mdogo, Meneja Miradi na Utafiti kutoka FADev, Evans Rubara amekiri bado wachimbaji wengi wanafanya kazi katika mazingira hatarishi kwa kutumia nyenzo duni.

Amesema, Fadev kwa kushirikiana na NBC wamejenga mfumo utakaotoa mikopo ya kufanyia kazi wachimbaji, aidha kwa kutoa vitendea kazi ama kuwasaidia wenye mgodi kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu.

Rubara amesema, kabla ya hapo wameanza kutoa elimu  ya mazingira yatakayowastahilisha kukopesheka ambapo ni lazima wapate leseni ya uchimbaji, kuwasaidia kuwa na takwimu za uzalishaji, kiuchumi na kibiashara ambayo wanaifanya kwenye soko halali.

“Jambo jingine ni kuwasaidiaa wafanye kazi katika mazingira salama, hatuwezi kuwa na sekta endelevu ikiwa wale tunaofanya nao kazi kama hawalindi afya, mazingira na hawana taarifa muhimu za uzalishaji  wala akaunti ya benki inayoeleweka,”

“Tunawasaidia wenye migodi pia wapate mafunzo jinsi ya kuweza kumudu pesa na kufanya shughuli zao kibiashara zaidi na kuwasaidia wachimbaji waweze kupata masoko ya uhakika na madini yao yanunuliwe kwa bei zinazoendana na soko la dunia,” anasisitiza Evans.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wadogo Nchini (FEMATA) amesema wanatambua changamoto wanazokutana nazo wachimbaji wadogo kuanzia nyenzo hadi mikopo na tayari wameshaweka juhudi madhubuti na kazi inaendelea kuwasaidia na wameshauriana na mabenki na wameshawasiliana na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kuishauri serikali iwekeze kuwekeza katika utafiti na wapo kwenye hatua nzuri kwani tayari wameshaanzisha vilabu vya wachimbaji.

Ameongezea katika hilo, ili sekta ya madini iweze kupiga hatua ni lazima watanzania watoe ushirikiano kwani wachimbaji inawezekana kabisa kukopesheka  kwani nchi za wenzetu wanakopesheka na wamepiga hatua na wao kama Femata wamewajenga kisaikolojia wachimbaji wadogo waweze kupokea mikopo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...