Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

USIKU wa Ijumaa Kikosi cha Wananchi, Yanga SC kinaondoka na Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania, Ndege aina ya Airbus A 220-300 kuelekea nchini Nigeria kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa pili wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United FC ya nchini humo, mchezo utakaopigwa mjini Port Harcout kwenye dimba la Yakubu Gowon.

Yanga SC ikiwa na ‘slogan’ yake ya NO RETREAT, NO SURRENDER, inaondoka na msafara wa watu takriban 60 wakiwemo Wachezaji 22, Benchi la Ufundi watu 10 pamoja na Viongozi wa Klabu, Mashabiki watakaosafiri kwa ajili ya kushangilia siku ya Jumapili Septemba 19, 2021 katika mchezo huo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Klabu hiyo, Haji Manara amesema wanaenda nchini Nigeria kwa lengo la kupata matokeo licha ya kukubali kukabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Wanigeria hao, Rivers United ambao watakuwa nyumbani katika mchezo huo.

“Tunajua tutakuwa ugenini katika mchezo wetu wa mkondo wa pili, tunajua tutakutana na visa na mikasa, na kwa vyovyote utakuwa mchezo mgumu. Tayari baadhi ya Viongozi wetu akiwemo Senzo Mbatha wametangulia tangu Jumatatu kuweka mazingira sawa sehemu ambayo tutafikia”.

“Hatuendi kinyonge Nigeria, tunaenda kupigana vita ya dakika 90 tunaamini tutashinda siku ya Jumapili. Tumeona mchezo wa Benjamin Mkapa takwimu zilikuwa upande wetu tuliongoza kwa kiasi kikubwa, kikubwa Wanayanga watuombee dua”, ameeleza Manara.

Kuelekea mchezo huo, Manara amesema watawakosa Wachezaji wao Sita, wakiwemo Mabeki David Brayson, Yassin Mustapha na Kiungo Mshambuliaji Balama Mapinduzi ambao bado ni majeruhi. Pia Yanga SC itaendelea kuwakosa Wachezaji wake Khalid Aucho, Djuma Shabani na Fiston Mayele ambao Hati zao za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) hazijafika.

Hata hivyo, Manara amethibitisha kuwa Wachezaji hao wa kigeni ambao wamekosa ITC hadi sasa, watakuwepo kwenye Ligi za nyumbani wakianza na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba SC, Septemba 25, 2021 katika dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Yanga SC inaondoka nchini Nigeria ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wake wa mkondo wa kwanza nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya Rivers United FC, bao hilo likifungwa na Mchezaji wa timu hiyo, Moses Omoduemuke.



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...