Na Mwandishi Wetu,Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama ameishauri jamii kutambua uwezo na mchango wa watu wenye Ulemavu mahali popote walipo ili kuinua ustawi na maisha yao na kuwafanya watambue kuwa wanamchango zaidi katika maendeleo ya jamii zao na Taifa kwa ujumla.

Mhagama amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wadau kuhusu Masuala ya Utoaji wa Huduma kwa watu wenye ulemavu uliofadhiliwa  na Foundation for Civil Society (FCS) ukilenga kupitia na kutoa maoni ya kukamilisha mwongozo wa kukuza ujumuishwaji na kuimarisha huduma kwa watu wenye ulemavu kilichofanyika tarehe 16 Septemba, 2021 katika Hoteli ya Royal Village Jijini Dodoma.

Amesema upo umuhimu wa kutambua uwezo na mchango wa Watu Wenye Ulemavu mahali popote walipo na Serikali kwa kushirikiana na Wadau mballimbali ina wajibu wa kuweka mikakati thabiti ya kuwaendeleza na kuwahakikishia ustawi na mahitaji yao ya kimsingi, ikiwemo ulinzi na usalama.

“Kuwa mlemavu sio kushindwa kufanya kitu chochote, ningependa jamii itambue vipaji na uwezo mkubwa walionao watu wenye ulemavu katika kufanya mambo makubwa kuliko wasio na ulemavu, hivyo kujumuishwa kwa kundi hilo katika nyanja zote za kijamii, kisiasa na kiuchumi ni kuinua ustawi na maisha yao na kuwafanya wawe na mchango zaidi katika maendeleo ya jamii zao na Taifa kwa ujumla,” alisema Waziri Mhagama

Amesema Tanzania ni nchi yenye demokrasia imara inayojengwa kwa kufuata misingi thabiti ya kuheshimu, kutambua na kuthamini utu, usawa na haki kwa watu wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote, ambapo kila mtu na kila mwananchi, wakiwemo Watu Wenye Ulemavu, wana haki sawa ya Kikatiba na Kisheria.

"Katika kushiriki kikamilifu katika mambo muhimu yanayomhusu yeye mwenyewe na jamii nzima kwa ujumla, ikiwemo kupata mahitaji ya Msingi na kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo yake binafsi, jamii na nchi kwa ujumla,"amesema.

Ameongeza Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inatambua na kuheshimu michango ya kila mdau kwa kuzingatia muhimu wake katika suala la ujumuishaji na uimarishaji wa utoaji na upatikanaji wa huduma bora wenye mahitaji maalum.

Pia mwongozo umelenga kurekebisha mitizamo, mienendo na vitendo vyote visivyolinda na vinavyonyima haki na nafasi kwa Watu Wenye Ulemavu kushiriki kwenye maamuzi na utekelezaji wa masuala muhimu ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Aidha, Tofauti na Miongozo mingine ya awali, Mwongozo huo unakusudiwa kuwa wa muda mrefu unaoweka na kutoa Dira na mwelekeo wa Vipaumbele muhimu vya Kitaifa katika Ujumuishwaji, Utoaji na Upatikanaji wa Huduma Bora kwa Watu Wenye Ulemavu nchini.

“Haya yote yanafanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi thabiti wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuhakikisha nchi inakuwa na Jamii Jumuishi inayozingatia Haki, Usalama, Usawa na Huduma Bora kwa Watu Wenye Ulemavu,”amesema.

Kwa upande wa Naibu Waziri anayeshughulikia masuala ya Wenye Ulemavu Ummy Nderiananga mesema kwamba ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanakuwa na ustawi, Serikali imeamua kufufua vyuo vya watu wenye ulemavu ili kuwajengea uwezo wa kujikimu kiuchumi na kuondokana na dhana ya utegemezi.

“Tulikuwa na vyuo viwili vya Sabasaba na Yombo vinavyofanya kazi na sasa tuna Luanzari mkoani Tabora na serikali inafanya ukarabati wa vyuo vya Tanga na Mtwara na tupo mwishoni katika mwongozo wa uboreshaji wa miundombinu kwa watu wenye ulemavu na kama serikali tutapata muda wa kuzungumza na wadau tuwe na dira ya pamoja,” ameeleza Naibu Waziri Ummy.

Aidha Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), Ernest Kimaya aliishukuru Serikali pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea kuunga mkono watu wenye ulemavu katika nyanja mbalimbali na ushirikishwaji katika sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti mwaka 2022.

“Tunaishukuru Serikali kwa kusimamia suala la ajira kwa watu wenye ulemavu sekta ya elimu kwani tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa wengi walioomba nafasi ya ualimu nafasi zilipotangazwa siyo kwa upendeleo ni kwa kufuata vigezo.Tunashukuru watu wenye ulemavu kuhusishwa kataika maandalzii ya sensa ya watu na makazi."

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la CBM International, Nesia akitoa neno la shukuran kwa mgeni rasmi mara baada ya kuhutubia katika mkutano wa Wadau kuhusu masuala ya utoaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu uliofanyika Septemba Jijini Dodoma.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Ummy Nderiananga akieleza mikakati ya Serikali katika kuhudumia watu wenye ulemavu wakati wa mkutano huo.

 Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la CBM International, Nesia akitoa neno la shukuran kwa mgeni rasmi mara baada ya kuhutubia katika mkutano wa Wadau kuhusu masuala ya utoaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu uliofanyika Septemba Jijini Dodoma.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...