WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Ofisi ya Rais-TAMISEMI ihakikishe inasimamia ujenzi wa majengo ya ofisi za halmashauri ya wilaya ya Kigoma unafanyika kwenye Kata ya Mahembe kama ilivyopendekezwa katika vikao vya Baraza la Madiwani si katika Kata ya Kamala linalopendekezwa na watalamu.

Ametoa agizo hilo leo (Ijimaa, Septemba 17, 2021) mara baada ya kusimamishwa na wakazi wa kata hiyo ambao wamedai maamuzi ya madiwani yamebadilishwa na kusisitiza kuwa kama sababu ni eneo kutofaa kwa ujenzi wa majengo ya ghorofa wabadilishe ramani Ili yajengwe majengo ya kawaida.

Wananchi hao ambao waliwasilisha malalamiko yao kupitia mabango walimueleza Waziri Mkuu kwamba hawaridhishwi na maamuzi ya Serikali ya kuhamishia ujenzi wa ofisi za halmashauri katika Kata ya Kamala wakati Baraza la Madiwani lilishatoa maamuzi kupitia vikao rasmi.

Baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Waziri Mkuu alimtaka Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Rashid Mchata atoe ufafanuzi juu la suala hilo ambapo kiongozi huyo amekiri kuwa ni kweli ujenzi ulipendekezwa ufanyike katika eneo hilo ila uamuzi wa kubadilisha ulitokana na ushauri wa wataalamu ambao walisema eneo hilo halifai kujengwa majengo ya ghorofa kama ramani inavyoonesha.

Waziri Mkuu amesema kwamba “Kama eneo hili halifai kujengwa ghorofa ni lazima mjenge majengo ya ghorofa? Wananchi wanahitaji majengo ya kutolea huduma. Unajua maamuzi ya eneo la ujenzi yameamuliwa na wananchi kupitia Baraza la Madiwani, hivyo yazingatiwe huko msiende kujenga.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema “Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ipo makini na haiwezi kuwaangusha, halmashauri itajengwa katika eneo lililochaguliwa na vikao vya Baraza la Madiwani na kama wataalamu watasema eneo hilo halifai kujengwa majengo ya chini waende kuhamisha kijiji maana patakuwa hapafai kwa makazi.”

Naye, Mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini Assa Makanika amesema Baraza la Madiwani lilipendekeza kuwa ujenzi wa jengi la halmashauti ijengwe katika eneo hilo na alishangaa kusikia ujenzi huo ukihamishiwa katika eneo linguine, ameomba maombi ya wananchi yasikilizwe.

Pia, Diwani wa Kata ya Mahembe, Mamisho Seif alisema Baraza la Madiwani lilifanya vikao na kupiga kura kuamua eneo ambalo zitajengwa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma ambapo kata ya Mahembe ilichaguliwa kati ya kata sita zilizopendekezwa.

“Jambo la kusikitisha ni kitendo cha wataalamu kufanya mabadiliko ya eneo la ujenzi na kuhamishia katika Kata ya Kamala. Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaomba maamuzi ya Baraza la Madiwani yafuatwe.”

Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mahembe alisema baada ya kupekea taarifa kwamba eneo lao limechaguliwa kujengwa ofisi za halmashauri walitoa bure eneo la ukubwa wa ekari 25 kwa Serikali ili liweze kutumia kwa ajili ya ujenzi huo.

Aliongeza kuwa wakati wakisubiri ofisi hizo zijengwe walitoa majengo ya shule ya msingi yatumike kama ofisi na wao kuamua kujenga shule nyingine, hivyo wanashangazwa na taarifa za kuhamishwa kwa makao makuu ya halmashauri yao, ambapo waliiomba Serikali iingilie kati suala hilo.

Kwa upande wake, Naibu wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, David Silinde amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba wamepokea maelekezo na watasimamia utekelezaji wa mapendekezo ya Baraza la Madiwani na Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma zitajengwa katika eneo hilo na si lazima yajengwe maghorofa.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuzungumzia juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita za kuendeleza zao la mchikichi nchini na kuwataka wakazi wa mkoa huo kuachana na kilimo cha mazoea na badala yake wasikilize ushauri wa unaotolewa na wataalamu ili kujiongea tija.

Akiwa katika Gereza la Kwitanga ambalo ni miongoni mwa maeneo maalumu kwa ajili ya kilimo cha mchikichi, Mheshimiwa Majaliwa amesema muitikio wa taasisi na wakazi katika kilimo hicho umetafsiri wazi mafanikio katika safari ya kuifanya Tanzania kujitolesha kwa mafuta ya kula na kuwa kitovu cha zao hilo katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema miche ya michikichi kwa sasa inatolewa bure, hivyo wsananchi wachangamkie fursa hiyo kwa kuongeza ukubwa wa mashamba na hatimaye kuipunguzia Serikali matumizi ya fedha nyingi za kigeni zinazotumika katika kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameisisitiza Serikali iwasaidie wananchi wanaotaka kulima zao la michikichi kwa kuwapa elimu kuanzia hatua za awali za utayarishaji wa mashamba, upatikanaji wa mbegu, pembejeo hadi upatikanaji wa masoko. “Suala la masoko la zao hili msiwe na shaka soko la uhakika lipo hapa hapa nchini.”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...