Makamu wa Rais na Mwenyekiti Mkazi, Equinor Tanzania AS, Unni Merethe Skolstad Fjaer akizungumza jambo wakati wa kikao kati ya Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na viongozi wa makampuni ya Shell na Equinor kilicholenga kuwaongezea uelewa wajumbe wa bodi hiyo kuhusu utekelezaji wa mradi wa kubadili gesi asilia kuwa kimiminika (LNG). Kikao hicho kimefanyika leo, Oktoba 25, 2021 jijini Dar es Salaam. Picha na Janeth Mesomapya
Na Janeth Mesomapya

BODI ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imekutana na kufanya kikao na viongozi wa makampuni ya Shell na Equinor ambao ni wabia wakuu (pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kwa niaba ya Serikali) wa utekelezaji wa mradi wa kubadili gesi asilia kuwa kimiminika (LNG).

Kikao hicho kilichofanyika leo, Oktoba 25, 2021 jijini Dar es Salaam kililenga kujadili namna bora ya utekelezaji wa mradi huo wa LNG ambao kwasasa hatua inayofuata ni ya kuanza kwa Majadiliano ya Mkataba wa Nchi Hodhi (HGA) baina ya serikali na wabia wa mradi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi hiyo Profesa Gasper Mhinzi, kikao hiki kilikuwa na nia ya kuwaongezea uelewa wajumbe wa bodi kuhusiana na mradi na manufaa yatakayotokana na utekelezaji wake.

“Katika kikao hiki makampuni haya yamefanya mawasilisho mbalimbali yaliyokuwa na lengo la kutanua uelewa kwa wajumbe wa bodi na jinsi utakavyokuwa na manufaa kwa pande zote mbili yaani serikali ya Tanzania na wawekezaji,” alisema.

Profesa Mhinzi aliongeza kuwa kikao hiki hakikuwa cha kufanya maamuzi yoyote bali kilijikita katika kuulewa mradi kwa undani ili kuboresha utekelezaji wake.

Naye Makamu wa Rais na Mwenyekiti Mkazi wa Shell, Jared Keuhl ameeleza kuwa ni muhimu kwa wadau wote yaani Serikali na wabia wa mradi kushirikiana na kuhakikisha katika hatua hizi za mwisho za maandalizi ya mradi kunakuwa na uwazi wa kutosha katika maamuzi yanayofanyika.

“Japokuwa hatua tuliyopo inaelekea ukingoni ni vizuri kila kitu kifanyike kwa ufasaha na uwazi mkubwa katika kipindi chote, na japokuwa majadiliano haya ni ya kuangalia maslahi ya pande zote mbili tunatamani yawe majadiliano ya ushirikiano,” aliongeza Keuhl.

Kikao hiki ni mwendelezo wa maandalizi ya majadiliano ya HGA baina ya Serikali na wabia wa mradi wa LNG yanayotarajiwa kuanza rasmi Novemba 8, 2021.

Mradi wa LNG ambao utasimamiwa na PURA unakadiriwa kuwa wa thamani ya takriban Dola za Marekani bilioni 30. Unatarajiwa kutengeneza ajira 6,000 za moja kwa moja na zaidi ya 15,000 zisizo za moja kwa moja kwa Watanzania.
Makamu wa Rais na Mwenyekiti Mkazi wa kampuni ya Shell Tanzania, Jared Keuhl akizungumza jambo wakati wa kikao kati ya Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na viongozi wa makampuni ya Shell na Equinor kilicholenga kuwaongezea uelewa wajumbe wa bodi hiyo kuhusu utekelezaji wa mradi wa kubadili gesi asilia kuwa kimiminika (LNG). Kikao hicho kimefanyika leo, Oktoba 25, 2021 jijini Dar es Salaam. Picha na Janeth Mesomapya.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi Charles Sangweni ambaye pia ni Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka hiyo, akizungumza jambo wakati wa kikao kati ya Bodi hiyo na viongozi wa makampuni ya Shell na Equinor kilicholenga kuwaongezea uelewa wajumbe wa bodi kuhusu utekelezaji wa mradi wa kubadili gesi asilia kuwa kimiminika (LNG). Kikao hicho kimefanyika leo, Oktoba 25, 2021 jijini Dar es Salaam. Picha na Janeth Mesomapya.
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na viongozi wa makampuni ya Shell na Equinor wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kikao kilicholenga kuwaongezea uelewa wajumbe wa bodi hiyo kuhusu utekelezaji wa mradi wa kubadili gesi asilia kuwa kimiminika (LNG). Kikao hicho kimefanyika leo, Oktoba 25, 2021 jijini Dar es Salaam. Picha na Janeth Mesomapya.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...