Na farida Mangube, Kilosa.

KAMATI za Maliasili za vijiji vinavyojihusisha na uhifadhi na uvunaji misitu kwa njia endelevu wilayani Kilosa mkoani Morogoro zimeagizwa zisikubali kuyumbishwa na viongozi kinyume na taratibu.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kitunduweta kata ya Muhenda baada ya kufanya ziara ya kuangalia shughuli za uhifadhi na uvunaji endelevu unaondelea katika misitu uliopo katika kata hiyo Mkuu wa wilaya hiyo, Alhaj Majid Mwanga alisema kumekuwa na vitendo vya baadhi ya viongozi wa vijiji na kata kuingilia kamati za maliasili hali ambayo inaondoa ufanisi wa kamati hizo

“Nina taarifa kuwa Katibu wa Kamati ya Maliasili Kitunduweta anataka kujiuzulu kwa sababu ya viongozi wanaingilia majukumu yenu, mimi nipo na nyie kazeni mguu na kama itatokea tena anawapa maagizo nipeni taarifa nitamshughulikia,” alisema.Mkuu wa Wilaya hiyo.

Ameongeza kuwa kamati za maliasili katika vijiji vyenye misitu zipo kisheria hivyo zinapaswa kuheshimiwa ili zifanye kazi kwa weledi na uaminifu kwani kinyume chake watachangia upotevu wa rasilimali misitu.

Aidha Mwanga alisema kamati hiyo imefanya kazi nzuri ya kulinda misitu katika kijiji hicho hivyo inapaswa kuungwa mkono ili kuhakikisha sumu hii ya kuhifadhi misitu inafika kila mahali wilayani Kilosa.

Mkuu huyo wa wilaya alisema uwekezaji uliofanywa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usisimamizi wa Misutu Tanzania (MJUMITA) kupitia ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC) unapaswa kuungwa mkono kwa kuhakikisha misitu inakuwa endelevu.

kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilosa Wilfred Sumari, alisema halmashauri itawapa ushirikiano wananchi wote ambao wanasimamia rasilimali misitu kwa kuwa ni muhimu kwa maendeleo na uchumi.

Sumari aliongeza kuwa hali ya uharibifu wa misitu katika maeneo ambayo hayana miradi ni mbaya hivyo kuwataka wananchi wote kuwa mabalozi wa uhifadhi ili misitu kuwa endelevu.

Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilosa, Kisena Mabuba alisema halmashauri haitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa mtumishi yoyote ambaye atabainika kushiriki kuhujumu rasilimali misitu ambayo ni muhimu kwa nchi.

“Yamesemwa mengi na wananchi ofisi yangu itafuatilia iwapo itabaini ushiriki wa mtumishi wa umma haitasita kuchukua hatua ili kuhakikisha misitu inakuna salama,” alisema.

Mabuba aliwaagiza makatibu tarafa na watendaji wa kata, vijiji na vitongoji kuhakikisha wanatatua changamoto zilizopo katika ngazi zao hasa katika eneo hilo la uhifadhi wa misitu hali ambayo itachangia rasilimali hiyo kuwa endelevu.

Katibu wa Kamati ya Maliasili Kijiji cha Kitunduweta, Leoti Msoloka alisema hali ya uhifadhi katika kijiji chao ni nzuri huku akitoa rai kwa watendaji wa vijiji kuacha kuingilia majuku yao hali inayowakatisha tamaa kulinda rasilimali hiyo adimu.

Msoloka alisema changamoto kubwa katika uhifadhi wa misitu ni moto na mifugo jambo ambalo linawakatisha tamaa hasa ikizingatiwa kuwa wapo viongozi wanatajwa kushiriki.

kwa upande wao wanufaika wa Mradi wa Usimamizi Shiriki wa Misitu ya Jamii (USMJ), kupitia uchomaji mkaa, Kulangwa Ganda alisema ujio wa mradi huo umeweza kubadilisha maisha yake na kijiji kwa ujumla.

Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo alisema ushiriki wa halmashauri katika uhifadhi utaongeza motisha kwa wananchi wanaozungukwa na rasilimali hiyo kuipenda na kuitunza.

“Sisi TFCG tulichokifanya ni kuleta mtoto na kumlea hadi amekuwa hivi sasa tumeshatoa mguu mmoja nje mwaka 2022 tunatoa wa pili imani yetu ni kuona baada ya kutoka kabisa mtoto huyu anahudumia familia yake mwenyewe bila kutegemea mtu mwingine,” alisema

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Alhaji Majid Mwanga akitoa maelezo na maelekezo kwa Kamati ya Maliasili na viongozi wa Kijiji cha Kitunduweta, kata ya Muhenda kuhusu kuongeza juhudi za kulinda na kuhifadhi Msitu wa Matalawe, kulia kwa DC ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Wilfred Sumari na kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Kisena Mabuba (Picha na Mpiga Picha wetu).


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilosa, Kisena Mabuba akijibu maswali ya baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kitunduweta kata ya Muhenda wilayani humo.Kulia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), Revocatus Njau na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaji Majid Mwanga.


Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG), Emmanuel Lyimo akitoa ufafanuzi kuhusu Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ta Mkaa Tanzania mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Alhaji Majid Mwanga na wananchi wa kijiji cha Kitunduweta kata ya Muhenda.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...