JUMLA ya Shule 12 kutoka Wilaya ya kisarawe zimenufaika na elimu ya unawaji mikono inayolenga kuwakinga na magonjwa mbalimbali ya maambukizi ikiwemo Uviko-19 iliyotolewa na taasisi isiyo ya Kiserikali  Environmental Conservation Community of Tanzania (ECCT) inayojihusisha na utoaji wa elimu ya Usafi na Utunzaji wa Mazingira. 

Mradi huo unaotekelezwa na taasisi hiyo chini ya Ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Japan International Cooperation Agency (JICA) unatarajiwa kuwafikia wanafunzi zaidi ya 5817 kutoka Shule nne za Sekondari na nane za Msingi za wilayani humo.

Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu ulioenda sambamba na ugawaji wa vifaa kwa ajili ya unawaji mikono wakati wa kilele cha siku ya unawaji mikono Duniani mwishoni mwa wiki iliyopita, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kisarawe Wanchoke Chinchibela aliipongeza ECCT kwa kuichagua wilaya hiyo kutekeleza mradi huo.

Alisema Tanzania kama ilivyo nchi zingine Duniani bado inakabiliwa na janga la ugonjwa wa Uviko-19 hivyo matumaini yao elimu ya unawaji mikono kwa wanafunzi wa Shule za wilaya hiyo itasaidia mapambano dhidi ya ugonjwa huo na mengine ya kuambukiza.

Chinchibela ambaye pia ni Afisa Maendeleo wa wilaya hiyo, alisema Serikali ya wilaya hiyo na wana  jamii nzima wa Kisarawe wamepokea jambo hilo kwa mikono miwili wakiamini kuwa elimu itakayoendelea kutolewa itakuwa chachu kwa wananchi katika mapambano dhidi ya magonjwa mbalimbali ya kuambukiza.

" Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kisarawe, nichukie nafasi hii adhimu kuwashukuru ECCT kwa upendo wao wa kuichagua wilaya yetu kuwa miongoni mwa wanufaika wa mradi huu, imetupa faraja na zaidi tunaamini elimu hii itakuwa chachu ya mabadiriko" alisema Chinchibela

Kwa upande wake Mkurugenzi wa ECCT, Bi.Lucky Michael alisema mradi huo ulioanza kutekelezwa Mei 21 Mwaka huu na unatarajia kutamatika Februari mwakani 2022, lengo lake ni kupunguza maambukizi ya magonjwa ya mlipuko kwa kuielimisha jamii ya wanafunzi na wananchi juu ya unawaji wa mikono na usafi kwa ujumla.

Alisema katika kulitekeleza hilo, ECCT imekuwa ikishirikiana vizuri na JICA, uongozi wa Wilaya ya Kisarawe na wadau wengine wa kimaendeleo ili kufikia adhma ya Serikali kuwa na jamii yenye afya njema.

Alizitaja Shule nufaika kupitia mradi huo kuwa ni  Manerumango,Chanzige,Kibuta na Masaki ambazo ni za Serikali na kwa upande wa shule za Msingi Shule zilizopo katika mradi huo ni  Chanzige 'A na B', Kibasila, Masaki, Chan'gombe 'A na B' Madugike na Kibuta.

Aidha aliushukuru uongozi wa Wilaya hiyo kwa kuupokea vyema mradi huo akiamini kuwa utasaidia mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko na hivyo kuiweka salama jamii nzima ya wana Kisarawe.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...