Na Mbaraka Kambona,

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kwa kushirikiana na Serikali wamesema kuna haja ya kuchukua hatua za haraka za kudhibiti kusambaa kwa mmea wa Gugu Kongwa ambao umeonesha kuathiri kwa kiasi kikubwa maeneo ya malisho  yaliyopo Wilayani Kongwa na Mkoani Singida.

Hayo yalibainishwa na Wataalamu hao walipokutana na wadau wengine wa Sekta ya mifugo jijini Dodoma Oktoba 22, 2021 kuwasilisha  matokeo ya awali ya utafiti waliofanya kujua tabia za ukuaji na usambaaji wa mmea huo ili kutafuta njia fungamanishi za kupunguza au kutokomeza kabisa mmea huo ujulikanao Gugu Kongwa.

Akiongea katika Mkutano huo, Mtafiti Kiongozi kutoka SUA, Dkt. Selemani Ismail alisema utafiti wa Gugu Kongwa ulilenga kujua tabia ya ukuaji wake na  kwa kiasi gani mmea huo unaoathiri malisho ya Mifugo umesambaa.

"Utafiti wa awali tulioufanya kwa miaka miwili (2)  ulilenga kutafuta njia shirikishi za kupunguza au kuangamiza kabisa mmea huo wa Gugu Kongwa ambao usambaaji wake umekuawa na athari kubwa katika maeneo mengi ya malisho hususan katika maeneo ya Kanda ya Kati na Mkoa wa Manyara," alisema Dkt. Ismail

Dkt. Ismail aliendelea kusema kuwa katika kutafuta njia ya kudhibiti Gugu Kongwa walifanya utafiti na kupata mmea unaoitwa Melia ambao umeonesha ufanisi katika kutokomeza usambaaji wa Gugu Kongwa.

"Utafiti wetu tuliufanya Wilayani Kongwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) na Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa ili kutokomeza mmea huo na kulinda malisho kwani likiachwa liendelee kusambaa athari zake ni kubwa sana kwa malisho ya mifugo," aliongeza

Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Kejeri Gillah alisema kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine inajipanga kuhakikisha matokeo hayo ya utafiti yanakwenda kufanyiwa kazi.

"Tumeona athari kubwa za gugu hili vamizi katika maeneo yetu ya malisho na hivyo ni muhimu kulidhibiti mapema ili lisisababishe uhaba wa malisho na kupunguza tija katika uzalishaji," alisema Dkt. Gillah

Naye, Meneja wa Mfuko wa Kuendeleza Sayansi na Teknolojia kutoka COSTECH, Ntufye Mwakigonja alisema anaimani kuwa utafiti huo utatatua changamoto hiyo inayokabili malisho nchini huku akiongeza kuwa  wao kama COSTECH wataendelea kushirikiana na watafiti hao ili kuhakikisha matokeo hayo yanafanyiwa kazi kwa manufaa ya Sekta ya mifugo nchini.

Aidha, Wadau wa Sekta ya Mifugo waliohudhuria mkutano huo walisema kuwa pamoja na kuwepo  changamoto zinazosababishwa na mmea huo katika malisho ya mifugo, watafiti hao waendelee kufanya utafiti kuangalia mtizamo chanya ambao unaweza kusaidia jamii kutumia faida zinazoweza kupatikana zitokanazo na Gugu Kongwa.

 

Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Prof. Antony Sangeda akiwasilisha sehemu ya utafiti wa Gugu Kongwa kwa Wadau wa Sekta ya Mifugo katika Mkutano wa uwasilishaji wa Utafiti huo uliofanyika juzi jijini Dodoma 


Mkurugenzi Mkuu, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI), Prof. Erick Komba akitoa maoni yake  katika Mkutano wa uwasilishaji wa utafiti wa awali kuhusu Gugu Kongwa uliofanyika juzi jijini Dodoma

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...