RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 27 Septemba, 2021 amewapatia zawadi ya viwanja wachezaji wa Timu ya Taifa ya Wanawake ya mpira wa miguu ya Twiga Stars na kuwapongeza kwa kubeba kombe la COSAFA Women’s Championship nchini Afrika Kusini.

Hafla ya kuwapongeza wachezaji hao, ambayo iliambatana na chakula cha mchana, imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Baraza la Michezo Tanzania (BMT).

Aidha, katika hafla hiyo Mhe. Rais Samia amewapongeza washindi sita (06) wa mashindano ya urembo na utanashati kwa viziwi barani Afrika, timu za Cricket za wanawake na wanaume kwa kushika nafasi ya tatu katika mashindano ya Cricket Afrika na timu ya Taifa ya Karate kwa kutwaa medali nyingi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mhe. Rais Samia amehusisha mafanikio ya timu za Taifa na uwekezaji ambao Serikali imeanza kuufanya katika kugharamia timu za taifa.

Mhe. Rais Samia amesema alikuwa akiwafuatilia kwa karibu Twiga Stars wakati wote wa mashindano hayo ya COSAFA na kwamba amevutiwa na kiwango walichokionyesha kuanzia mchezo wa kwanza hadi fainali na kuongeza kwamba timu hiyo ya Twiga Stars imeonyesha ushujaa mkubwa na majina yao yataandikwa katika historia ya michezo ya nchi yetu.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amewaomba mawakala wa wachezaji wa mpira wa miguu wawasaidie wachezaji wa Twiga Stars ili waweze kupata nafasi ya kucheza soka la kimataifa nje ya nchi ili kuwainua na kuisadia timu yetu ya Taifa ya Wanawake iweze kuwa na uzoefu mchanganyiko, na kuwaasa wachezaji hao kudumisha nidhamu kwasababu ndio msingi mkuu wa mafanikio.

Sambamba na pongezi hizo kwa Twiga Stars, Mhe. Rais Samia amempongeza Kocha Mkuu wa timu hiyo Bakari Shime kwa kazi kubwa aliyoifanya na kuahidi kuangalia namna bora ya kusaidia kuihudumia Twiga Stars na kutatua changamoto zinazoukabili mchezo wa mpira wa miguu.

Wakati huohuo, Mhe. Rais Samia amesema mabadiliko aliyoyafanya hivi karibuni katika muundo wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo yalikuwa na lengo la kuleta ufanisi katika masuala ya utamaduni, sanaa na michezo ili mchango wa sekta hizo katika kukuza ajira uweze kuonekana.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Samia aliwaombea dua timu ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 20 (Tanzanite) ambao wanawania nafasi ya kucheza Kombe la Dunia chini ya miaka 20 mwezi Juni mwakani nchini Costa Rica.

Jackson Msangula
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...