Na Englibert Kayombo – Dodoma.

Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) leo limetoa taarifa ya matokeo ya mtihani wa kabla ya utarajali kwa wanafunzi waliokuwa wanatarajia kuanza mafunzo hayo kwa vitendo katika vituo vya kutolea huduma nchini.

Akitoa taarifa hiyo leo Jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Baraza la Madaktari Tanganyika Prof. David Ngassapa amesema mnamo Tarehe 13 Oktoba, 2021 Baraza lilitahini watarajali watarajiwa kutoka katika vyuo mbalimbali Nchini vipatavyo tisa (9) na Wanafunzi kutoka nje ya Nchi ambapo jumla ya wanafunzi 1242 Waliojiandikisha kufanya Mtihani.

“Jumla ya wanafunzi waliojiandikisha kufanya mtihani walikua 1242 na waliofanya mtihani walikua jumla 1,198, ambapo 1161 walikua Wahitimu wa Udaktari, 36 wahitimu wa Udaktari wa Meno na mmoja (1) Mhitimu wa Fiziotherapia ambapo walifanya mtihani huo katika vituo vitano ambavyo ni Dar es Salaam (680), Kilimanjaro (182), Dodoma (106), Mbeya (79) na Mwanza (151).” amesema Prof. Ngassapa

Ameendelea kwa kusema kuwa wahitimu wa Udaktari waliofaulu wako 845 ambao ni 72.8% waliofeli ni 316 ambao ni 27.2%, wahitimu wa Udaktari wa Meno waliofaulu ni 28 (77.8%) na waliofeli ni 8 ambao ni 22.7%, upande wa Fiziotherapia alikua mmoja na alifeli.

Prof. Ngassapa amesisitiza kuwa hakuna mwanafunzi ambaye amefeli na akafaulishwa kama ambavyo imekua ikidaiwa na baadhi ya watahiniwa wa mtihani.

Aidha Prof. Ngassapa amsema Baraza kwa kuzingatia changamoto walizopitia watarajali watarajiwa na baada ya kupokea maombi mbalimbali limeridhia kuruhusu kufanyika kwa mtihani maalum ambao utafanyika tarehe 8 .12. 2021.

“Mtihani huu awali ulilenga wale tu waliokutana na changamoto wakati wa kufanya usajili lakini walikua na vigezo vya kufanya mtihani, kwa kuwa mtihani huo maalumu ulishapangwa kuwepo na kuna watahiniwa waliokwisha leta maombi ya kurudia mtihani baada ya matokeo, Baraza limeridhia kuwaruhusu nao kufanya kwa marudio ya mtihani huo” amefafanua Prof. Ngassapa.

Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) lililo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto limeundwa na Sheria ya Udaktari, Udaktari wa Meno na Afya shirikishi sura Na. 152, kifungu cha 4 cha Sheria na linaratibu maombi ya watarajali na kuwapa usajili wa awali (Provision Registration) kwa ajili ya kuwapangia katika vituo vya utarajali kama sheria inavyo elekeza na kisha usajili kamili wakisha maliza na kufaulu mtihani wa baada ya utarajali.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...