Na. Paschal Dotto-MAELEZO

Waziri wa Habari, Mwasiliano na Teknolojia  ya Habari, Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na kufanya kazi na vyombo vya habari katika kutangaza  mambo mbalimbali yanayofanywa na Serikali kwa watanzania.

Akizungumza katika Mkutano wake na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini, Waziri Dkt.  Kijaji amesema lengo la Serikali ni kujenga uimara wa vyombo hivyo ili viweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika kuwaelimisha, kuburudisha na kutangaza mandeleo ya nchi kwa wananchi.

“Ndugu Wahariri lengo la Mkutano huu  ni kujitambulisha kwenu kwani tangu niteuliwe, Jambo hili ni muhimu hususan baada ya Mhe. Rais kuamua kwamba tasnia ya Habari sasa isimamiwe na Wizara yangu na kuunda Wizara Mpya yaani Wizara ya Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, kwa hiyo ndugu wahariri ninaomba ushirikiano katika kukuza hii tasnia”, Alisema Dkt. Kijaji.

 Dkt Kijaji alisema kuwa ushirikiano wa Vyombo vya Habari na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ni  tunatimiza takwa la kisheria   Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inatamka kuwa kila mtu yuko huru kutoa  maoni na kutoa mawazo yake,  kutafuta, kupokea na kutoa habari kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi.

Aidha Dkt. Kijaji alivishukuru Vyombo vya Habari nchini kwa kuendelea kuelimisha na kutoa  ushirikiano katika changamoto kubwa ya UVIKO 19, ambapo aliwataka waendelee kufanya kazi kwa weledi ili wananchi wapate elimu na kuchukua maamuzi sahihi ya kuchanja na kujikinga na madhara ya janga hilo.

Katika hatua nyingine Dkt. Kijaji alisema kuwa ushirikiano wa Vyombo vya habari na Serikali kupitia Wizara yake ni moja na nguzo muhimu katika kuendeleza sekta hiyo kwani ni sekta ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo inafanya wananchi kupata taarifa ya utekelezaji wa miradi na mambo mbalimbali ya Serikali, lakini pia inaonyesha wadau wa maendeleo nini Serikali inafanya.

 “Pamoja na juhudi kubwa mnayoifanya, naendelea kuwaomba ushirikiano mkubwa kutoka kwenu ili tuweze kuindeleza sekta ya habari hapa nchini na kutangaza masuala muhimu na mazuri yanayofanywa na Nchi yetu ikiwa ni pamoja na miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali, Wadau wa Maendelo na Wananchi wetu kwa ujumla wao”Alisema Dkt Kijaji.

 

Kuelekea Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru, Dkt. Kijaji alieleza umuhimu wa vyombo vya Habari katika kuelezea nchi ilikotoka, ilipo na inapokwenda, ambapo kuelekea siku hiyo ya  tarehe 9 Disemba 2021, vyombo vya habari vinatakiwa kueleza maendeleo na mambo mbalimbali yaliyofanyika tangu uhuru

Aliongeza kuwa kutokana na umuhimu wa sherehe hizo, Watanzania wote hawana budi  kujivunia miaka 60 ya Uhuru  wakiwa na amani na maendeleo katika  sekta mbalimbali ikiwepo tasnia ya habari.

“Naomba nitumie fursa hii kuwaomba wanatasnia ya habari kushiriki kikamilifu katika kutangaza shughuli zote zinazohusu Uhuru wa nchi yetu kama sehemu muhimu ya kutoa elimu kwa Watanzania na dunia kwa ujumla. Umoja wetu katika jambo hili utasaidia sana kuelimisha wananchi”, Alisema Dkt. Kijaji.

Akijibu Swali lililoibuliwa na Wahariri, kuhusu Maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Kijaji alisema kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kufunguliwa kwa media mbalimbali zikiwemo zile za magazeti na online za Wizara inalifanyia kazi agizo hilo na atahakikisha anapata ufumbuzi hivi punde.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainabu Chaula amevitaka vyombo vya Habari kufanya kazi kwa weledi na kwa kufuata sheria kwani kwa kufanya hivyo tasnia itakua na kuwa na watalaam zaidi.

“ Waandishi wa Habari, tukifanya kazi kwa weledi hakuna kuvutana na fujo haziwezi kutokea, tukifanya kazi zinazotuhusu hakuna vurugu yeyote kwa hiyo tufanye kazi kwa kufuata sheria na kutumia taarifa vizuri ili kutoa taarifa za kuaminika”,

Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji akieleza jambo kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini umuhimu wa vyombo vya habari katika kujenga taifa na kuketa ustawi  wakati wa kikao chake na wahariri hao kilichofanyika leo Oktoba 25, 2021 Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari leo Oktoba 25, 2021 Jijini Dar es Salaam kuhusu mikakati ya wizara hiyo katika kuimarisha ushirikiano na vyombo vya habari hapa nchini.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jimmy Yonazi akieleza jambo wakati wa kikao cha pamoja kati ya Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji leo leo Oktoba 25, 2021 Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa akieleza kwa wahariri kuhusu utayari wa Idara ya Habari kuendeleza ushirikiano uliopo na vyombo vya habari hapa nchini kwa maslahi ya Taifa.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Bw. Deodatus Balile akieleza kufurahishwa kwake na namna Wizara ya Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ilivyoanza kushughulikia masuala ya sekta ya Habari hapa nchini ili kukuza zaidi sekta hiyo na kuongeza ustawi wa Taifa.
Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji akiwa kwenye picha ya pamoja na wahariri wa vyombo vya habari hapa nchini mara baada ya kikao chake na wahariri ha oleo Jijini Dar es Salaam 

Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakifuatilia hotuba ya Waziri wa  Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji wakati wa kikoa chake na wahariri hao leo Oktoba 25, 2021 Jijini Dar es Salaam.

 

(Picha zote na Idara ya Habari MAELEZO)


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...