Riyadh, Saudi Arabia

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Mhe. Abdulaziz bin Salman Al Saud ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya kikazi nchini humo. Katika kikao hicho, Waziri Makamba alijadiliana masuala mbalimbali yahusuyo nishati na Waziri mwenzake na pia aliwasilisha ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Serikali ya Saudi Arabia.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Waziri Makamba alisema “tumekuja nchini Saudi Arabia tukiwa na ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ninayo furaha kusema kuwa ujumbe huo umefika kama ilivyokusudiwa”. Aidha, Waziri Makamba aliongeza kuwa Tanzania na Saudi Arabia zina mahusiano mazuri ya muda mrefu na sasa nchi hizi mbili zinakusudia kuendeleza mahusiano kwa kuongeza ushirikiano katika sekta ya nishati.  

“Katika kuthibitisha hilo siku za hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia alitembelea Tanzania na pia Mfalme wa Saudi, Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud amemualika Rais wetu, Mhe. Samia Suluhu Hassan kuzuru Saudi Arabia” alieleza zaidi Waziri Makamba.

Waziri Makamba, katika ziara hiyo ameambatana na Kamishna wa Petroli na Gesi, Ndg. Michael Mjinja na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio. Ziara hiyo pia imelenga kuanzisha uhusiano wa kibiashara, kubadilishana ujuzi na teknolojia katika sekta ya mafuta na gesi. Ikumbukwe kuwa Saudi Arabia ni mzalishaji mkubwa wa mafuta duniani na hivyo mahusiano na Tanzania yanaweza kufungua fursa mbalimbali katika eneo hilo.

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akiagana na mwenyeji wake, Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia Mhe. Abdulaziz bin Salman Al Saud mara baada ya kumaliza mazungumzo yao. Wengine pichani ni Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Balozi Ali J. Mwadini (nyuma ya Waziri Makamba), Kamishna wa Petroli na Gesi, Ndg. Michael Mjinja (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio (kushoto)

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akizungumza na mwenyeji wake, Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia Mhe. Abdulaziz bin Salman Al Saud. 

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akiongozana na mwenyeji wake ambaye ni Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Mhe. Abdulaziz bin Salman Al Saud mara baada ya kumaliza kikao chao kilicholenga kudumisha uhusiano katika sekta ya nishati na kuwasilisha ujumbe wa Rais Samia kwa Serikali ya Saudi Arabia. 

 Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akiteta jambo na mwenyeji wake ambaye ni Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Mhe. Abdulaziz bin Salman Al Saud. Wengine pichani ni Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Balozi Ali J. Mwadini (wa pili kushoto) na Katibu wa Waziri Makamba, Ndg. Dunford Mpelumbe (wa kwanza kushoto)

 

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...