Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MTU Wangu ngoja nikwambie kitu,iko hivi mtaani kwangu na hata kwako tunashuhudia makundi ya rika mbalimbali ambavyo wanavuta bangi kila kukicha.Unashangaa?

Kibaya zaidi wanaotumia wenyewe wanajidanganya tu, oooh bangi bwana inakufanya uwe na nguvu, oooh sijui ukivuta utakuwa unalima sana!! Uongo mtupu na wala usikubali kudanganywa.Bangi mbaya na haifai kwa jamii, huo ndio ukweli.

Sasa iko hivi najua wengi tunazungumzia bangi lakini wakati wengine hawajui bangi nini ? Inatokana na nini? Madhara yake je, kweli inakupa nguvu?

Ngoja tuanze,na bangi ni nini? Tuliza akili bro,kuwa makini mshikaji wangu, mwana ujue nataka kuongea na wewe,acha kuzingua bwana.Tega sikio na sikiliza kwa makini...ndio nakwambia na weka kichwani.Eeh nilikuwa nataka kueleza bangi ni nini? Jibu ni kwamba bangi ni aina ya dawa ya kulevya inayotokana na mmea unaoitwa "Cannabis Sativa" ambavyo hustawi na kutumika kwa wingi hapa nchini na duniani kote.

Bangi huathiri ubongo na kuvuruga utendaji wa milango ya fahamu hivyo kubadilisha tunavyotafsiri uhalisia wa vitu.Majani na maua ya mmea huo hukaushwa na kutumiwa kama kilevi peke yake au kwa kuchanganywa na dawa nyingine.

Mara nyingi bangi imekuwa ni kati ya dawa ya awali kutumiwa ambapo watumiaji wengi huanza matumizi wakiwa na umri mdogo,hivyo kuwa katika hatari zaidi ya kuathirika kiafya.Aidha watumiaji wengi wa bangi huishia kutumia dawa nyingine hapo baadaye kama heroin na cocaine.

Hivyo bangi hutumika kama njia ya kuingia katika matumizi ya dawa nyingine za kulevya.Majina mengine ya bangi yanayotumika mitaani ni kama msuba,dope,nyasi,majani,mche,kitu,blanti,mboga, sigara kubwa, ndumu,msokoto na ganja.Ila mshikaji wangu jamaa wanaotumia hii kitu wajanja sana, wana majina mengi sana, wengine wanaita cha Arusha,ujue hiyo ndio ile bangi ambayo wavutaji wanaona iko Super, dah! Jamaa hawa noma sana.

Hata hivyo iko hivi bangi huweza kupatikana katika hali tatu,bangi ya majani yaliyokaushwa ambayo hupatikana na kutumika zaidi.Bangi iliyosindikwa hufahamika pia kama charas au hushish na hupatikana kwa kiasi kidogo hapa nchini.Mafuta ya bangi huwa na kiasi kikubwa zaidi cha kemikali ya THC na hupatikana kwa kiasi kidogo zaidi.

Mmea wa bangi una kemikali zipatazo 400 ambapo tetrahydrocannabinol ( THC) ndiyo kemikali inayoathiri ubongo ikipatikana kwa asilimia tano hadi 22 kwenye mmea huo.Bangi iliyosindikwa huwa na kiasi kikubwa cha THC inayofikia asilimia 20 ikilinganishwa na bangi ya majani iliyokaushwa.

Kiasi kikubwa cha bangi iliyosindikwa huzalishwa kwa kutumia maua na vikonyo vya bangi katika nchi za Morocco,Lebanoni na Afghanistan .Bangi ya mafuta ambayo watumiaji huchanganya na vyakula vingine huwa na kiasi kikubwa cha THC kinachofikia asilimia 60 .

Ngoja nikupe darasa, iko hivi mbegu na matawi ya bangi huwa na kiasi kidogo sana cha THC .Kiasi cha THC kimekuwa kikiongezeka kutokana na kukua kwa teknolojia katika uzalishaji wa bangi,aidha kemikali ya THC hukaa mwilini mwa mtumiaji kwa muda mrefu hadi mwezi mmoja kwa kujishikiza kwenye kuta za seli za ubongo ikilinganishwa na aina nyingine ya dawa za kulevya.

Halafu bwana ngoja nikueleze bangi inamadhara mengi,yaani mengi kweli.Ngoja nikwambie tu baadhi ya madhara ya bangi kwanza kabisa huamsha magonjwa ya akili hususani sonona, uvutaji wa bangi huzalisha lami na kemikali mbalimbali kwenye mapafu na kusababisha kikohozi sugu,kukosa pumzi,vidonda vya koo pumu pamoja na saratani.

Pia bangi huingilia utendaji kazi wa milango ya fahamu na humfanya mtumiaji awe kwenye hali ya njozi ambapo ataona na kusikia vitu tofauti na uhalisia hasa rangi na sauti .Hali hiyo huweza kusababisha ajali,uharibifu wa mali pamoja na kushusha ufanisi wa kazi.

Baadhi ya watumiaji hupata wasiwasi mkubwa mara wavutapo na kuwahisi vibaya watu wengine na huweza kujidhuru mwenyewe au kumdhuru mtu bila hatia.

Lakini ndugu yangu bangi hupunguza uwezo wa kufikiri na kukumbuka.Kwa wanafunzi na vijana matumizi ya bangi hufanya washindwe kukumbuka wanachojifunza,kushindwa kutulia ili wajifunze ,kupunguza uwezo wa akili na kupoteza ari ya kujifunza na hivyo kupata matokeo yasiyoridhisha.

Ikumbukwe kuwa bangi haiongezi ufanisi na tija kazini ,kwenye kilimo au masomo.Dunia ya mtumiaji hubadilika kutoelewa muda na mahali alipo na huwa mgomvi sana,bangi huaribu uwezo wa kumudu uendeshaji mitambo na hupunguza usikivu.

Halafu naona hapa kuna watu wanaona mimi mtalaamu, nikwambi mshikaji wangu utalaamu wangu ni kuandika tu ili unayesoma ujumbe ukufikie.Msema kweli mpenzi wa Mungu na mimi napenda kuwa karibu na Mungu wangu, kwanza naye hapendi watumiaji dawa za kulevya.Kwa hiyo nachotaka kueleza haya niliyoandika ni kwa msaada wa vipeperushi viivyoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.

Pili nimeandika baada ya kupata darasa la kutosha kutoka kwa Kamishina Msaidizi wa Kitengo cha Kinga na Huduma za Jamii wa Mamlaka hiyo Moza Makumbuli .Ujue Mamlaka pamoja na mambo mengine imejikita katika kutoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya.

Hivyo wameamua kuandaa darasa(mafunzo) kwa ajili ya waandishi wa habari ,lengo ni kutujengea uwezo ambao utawezesha kutumia kalamu na maandishi yake kuendelea kuelimisha umma.Mafunzo haya yanaendelea kwa waandishi wa habari hasa wanaoripoti kupitia mitandao ya kijamii.

Kama hutajali naomba nihitimishe kwa kueleza hivi na hiyo ni kwa mujibu wa Kamishina Moza , ni kwamba Taifa linaingia gharama kukabiliana na matumizi pamoja na kilimo haramu cha bangi kwa kutoa tiba ya maradhi ya akili yanayotokana na bangi, kuteketeza mashamba,kudhibiti biashara ya bangi na kuwatunza wahalifu wanaojihusisha na bangi.

Hivi naomba kuuliza hadi hapo ujaelewa tu? Maana naona wengine wameanza kulalamika eti nimeandika sana! Ndio nimeandika kwani madhara yake hujui?

Leo nimefurahishwa na mfano mmoja uliotolewa na Florance Khambi ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DCEA aliuliza hivi ukiambiwa kuna njia mbili,njia moja kuna walevi na njia nyingine kuna wavuta bangi, utapita njia ipi kati ya hizo?

Nilicheka lakini nikaona angalau nipite njia ya Walevu, najua hawanaga shida, kwa wavuta bangi njia yao visu nje nje, kukabwa ni jambo la kawaida.Usicheke ndugu yangu.Halafu nisikuchoshe wala usinichoshe.Alamsiki.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...