Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma na Kampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA), timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA SC), wamepata mwaliko wa kwenda kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa na wenzao wa Uganda, imeelezwa jijini Dar es Salaam.

Mwaliko huo umetolewa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Uganda (URA), John Musinguzi wakati akikipokea kikosi cha TRA SC kilichorejea Dar es Salaam kikitokea Morogoro katika mashindano hayo yanayofanyika kila mwaka.

Kamishna Musinguzi aliwapongeza mabingwa hao na kuwataka waendeleze ushirikiano kazini na kwenye michezo wanayoshiriki.

Alisema anafahamu mafanikio katika michezo yatasaidia pia katika kuinua maendeleo ya nchi kupitia kazi za kila siku wanazozifanya.

" Ninaona hapa mbele kuna makombe matano, ninawaalika mje Uganda tucheze mechi ya kirafiki au wao watakuja huku (Tanzania), ninawaahidi pia kule Uganda tuna kikosi imara cha soka, sina uhakika katika michezo mingine, lakini tuanze kwanza na mpira wa miguu," alisema Musinguzi.

Naye Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata aliwapongeza wachezaji wake kwa kuendeleza ubabe katika mashindano hayo na kusema wamewapa heshima kubwa taasisi hiyo.

Kidata aliwaambia ili kuhakikisha wanaendelea kufanya vizuri, ameshatenga 'fungu' la fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati wa uwanja wa michezo wanayofanya mazoezi.

Kiongozi huyo alielekeza anataka kuona hadi kufikia Juni mwakani, marekebisho hayo ya uwanja yawe yamekamilika na tayari uanze kutumika.

"Nataka uwanja ufanyiwe marekebisho makubwa na uwe wa kisasa, hatuwezi kufanyia mazoezi katika viwanja vibovu halafu tukaenda kushindana katika viwanja vizuri, tutashindwa," Kidata alisema.

Msemaji wa timu, George Gassaya, aliushukuru uongozi wa TRA kwa kuwapa ushirikiano mzuri kuanzia wakati wa maandalizi hadi walipokuwa kwenye mashindano.

Gassaya alisema umakini na kujituma kwa wachezaji wa timu hiyo ndio sababu nyingine iliyopelekea wakafanikiwa kutetea taji walilokuwa wanalishikilia la mashindano hayo.

"Tulipata muda mrefu wa mazoezi, unajua timu hii inaundwa na wachezaji kutoka mikoa yote ya Tanzania, na mpira sio kazi yetu rasmi, ila tulipata muda mzuri wa kujiandaa na hatimaye tumeibuka mabingwa," alisema Gassaya.

TRA SC iliibuka Mabingwa wa SHIMMUTA mwaka baada ya kuwafunga wenzao kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA), bao 1-0.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata akipokea kombe kutoka kwa Shomar Kamna ambaye ni Nahodha wa timu ya mpira wa miguu ya TRA SC mara baada ya kuibuka washindi wa mashindano ya SHIMMUTA yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Mkoani Morogoro

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...