Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Lusajo Kafuko akizungumza na wamiliki na walezi katika vituo vya makuzi na malezi kwa watoto wachanga na watoto wadogo, mafunzo hayo yametolewa wilayani Mkuranga mkoani pwani.
KATIKA kuhakikisha watoto wanapata huduma za malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali kadiri ya taratibu za serikali Shirika la Anjita Child Development Foundation kwa kushirikiana na serikali limeendelea kutoa mafunzo kwa wamiliki na walezi wa vituo vya kulelea watoto wadogo na watoto wachanga mchana.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Mkuranga Mkoani Pwani, Meneja Mradi wa Shirika la Anjia, Janeth Malela amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia uboreshaji wa huduma kwa watoto vituoni ikiwepo wamiliki kuendelea kufanya usajili wa vituo, kwani kwa kufanya hivyo kunaongezea thamani vituo hivyo na kuvifanya vitambulike rasmi kisheria.
Janeth amesema, watoto kuwepo katika vituo hivyo kunasaidia ulinzi na usalama wa watoto, kuwepo kwa ujifunzaji wa awali kwa watoto na wazazi /walezi wanapata muda wa kufanya shughuli za kiuchumi.
Amefafanua pia, program ya 'mafunzo kwa wote' yamewalenga wamiliki na walezi wote katika mikoa ya Rukwa, Pwani, Mtwara, Lindi, Kagera, Arusha, Kilimanjaro, Njombe na Ruvuma. Ambapo kwa awamu ya kwanza yamefanyika Rukwa, Pwani na Mtwara, na kwa mwaka wa fedha 2022/ 2023 mikoa iliyobakiwa itatekelezwa.
Akizungumzia kuhusu serikali imejipangaje kuhusiana na huduma vituoni, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Lusajo Kafuko amewaasa wamiliki wa vituo vya Malezi na makuzi kuvisajili Serikalini ili watambulike na shughuli zao zitambulike Serikalini.
Amesema usajili wa vituo hivyo ni bure kwani sheria ya mtoto namba 21 ya Mwaka 2009 kifungu cha 147 mpaka 152 na kanuni za watoto imetoa ufafanuai kuhusu vituo vya kulelea watoto wadogo na watoto wachanga mchana na imeeleza taratibu za kufuata wakati wa kufungua vituo vya makuzi na malezi kuwa na vigezo vinavyohitajika.
Amesema kuwa wilaya ya Mkuranga inavituo 123 vinavyojulikana na ustawi wa jamii kati ya hivyo vimesajiliwa vituo 21.Hivyo ni vema kwa kila anaeanzisha asajili kwanza kwaajili ya kumlinda mtoto.
Kwa upande wa Mwakilishi wa wamiliki Eva John, amelishukuru shirika la Anjita na serikali kwa utoaji wa mafunzo yaliyokuwa ya vitendo zaidi na kusaidia uundaji wa umoja wa wamiliki wa day care centers -mkuranga na kutuelekeza vyuo vya malezi vinavyotambulika na serikali ambapo itasaidia kuongeza ujuzi kwa wamiliki na walezi.
Eva amesema, jitihada zote za Anjita na serikali zimesaidia kuongeza uelewa kwao na kuanza kufanya mabadiliko chanya ya kutoa huduma za vituo kwa watoto na kuwepo na umoja huo utawasaidia kujadiliana na kupeana uzoefu katika eneo la huduma vituoni.
Eva amesisitiza pia serikali na wadau wasichoke waendelee na jitihada hizo na ikiwezekana hadi kwa wazazi/walezi yawafikie ingawaje pia wao kama wamiliki na walezi vituoni watasaidia kutoa elimu ya malezi kwa wazazi/ walezi katika vituo.
Mratibu, Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto kutoka shirika la Anjita Child Development Foundation, Yasinta Mlay akitoa maelekezo kwa makundi wakati wa mafunzo ya Malezi na makuzi kwa watoto yaliyofanyika wilayani Mkuranga mKoani Pwani Novemba 20,2021.
Walezi wakifundishwa baadhi ya michezo ya watoto inayofuata sheria wakati wa mafunzo ya malezi na makuzi kwa wamiliki na walezi wa watoto wachanga na watoto wadogo.
Makundi ya wanaopewa mafunzo kwa watoto wachanga na watoto wadogo wakiendelea kufanya kazi walizopewa na mtoa mafunzo.
Mmpoja wa walezi wa watoto akitoa moja ya mchezo wa kumpongeza mtoto ambapo amefanya vizuri (Mpasho) wakati wa mafunzo kwa walezi na wamiliki wa vituo vya malezi kwa watoto wachanga na watoto wadogo mchana.
Mazoezi yakiendelea kwa walezi na wamiliki wa vituo vya malezi na makuzi kwa watoto katika mafunzo yaliyofanyika wilayani Mkuranga Mkoani Pwani Novemba 20,2021.
Wawasilishaji wa makundi wakiwasilisha majibu ya maswali waliyopewa na Mkufunzi wao wakati wa mafunzo yaliyofanyika wilayani Mkuranga Mkoani Pwani Novemba 20,2021.
Picha mbalimbali katika makundi ya wamiliki na walezi wa watoto wachanga na watoto wadogo wakati wa mafunzo yaliyofanyika wilayani Mkuranga Mkoani Pwani Novemba 20,2021.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...