WAZIRI MKUU, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema Serikali imetoa maelekezo kwa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kuwasaidia wawekezaji pamoja na wafanyabiashara wadogo ili wafanye vizuri katika shughuli zao kwa kuwa kuna faida kubwa kwa Taifa.

“Haya ni maelekezo thabiti ya Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa ni lazima sekta zote zinazohusika na uwekezaji, ziendelee kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Novemba 27, 2021) alipotembelea kiwanda cha maji cha Tukuyu Springs Water Limited, Kilichopo katika Kijiji cha Kibisi, Kata ya Kyimo, Wilayani Rungwe Mkoani Mbeya.

Mheshimiwa Majaliwa amesema, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) itaendelea kuboresha mazingira bora ya uwekezaji na kushughulikia changamoto zinazowakabili pamoja na kutoa fursa kwa wawekezaji wazawa.

“Serikali inaendelea kuboresha miundombinu yote muhimu kwa wawekezaji ikiwemo, kuweka mfumo rahisi wa kuwapatia wawekezaji ardhi, kuboresha miundombinu ya barabara, nishati na maji”

Amesema uwekezaji hasa wa wazawa umekuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania kwani wanaelewa mazingira halisi ya maeneo wanayowekeza huku akipongeza kitendo cha kiwanda hicho cha Tukuyu Springs Water Limited kuwawezesha wakazi wanaozunguka eneo la kiwanda kupata huduma ya maji safi na salama pamoja na kuwasaidia kuunganishiwa huduma ya umeme.

Waziri Mkuu pia amewahakikishia wawekezaji kuwa Watanzania wengi sasa wana elimu ya kutosha na utaalam wa kuajiriwa na wanaaminika katika maeneo yao ya kazi na hilo limedhihirishwa na muwekezaji wa kiwanda hicho kwa kuajiri asilimia 100 ya Watanzania na kazi zinafanywa vizuri na kiwanda hicho kimepata mafanikio.

Awali akitoa taarifa ya uwekezaji Meneja Mkuu wa kiwanda hicho Godfrey Ng'wanang’walu ameishukuru Serikali kwa mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa kwa wawekezaji wazawa na ameahidi kuendelea kuwekeza zaidi na kutoa ajira kwa Watanzania “Kwa sasa kiwanda kiko katika hatua ya upanuzi ili kuongeza uzalishaji”.

“Uwekezaji huu ni matunda ya mazingira bora yaliyotengenezwa na nchi yetu, tumekuwa na mafanikio katika kipindi chote cha uzalishaji na tumeweza kulipa kodi kwa uaminifu mkubwa, katika kipindi chote tumepata ushirikiano kutoka kwa viongozi wa Mkoa na Wilaya, sisi tutaendelea kuwekeza zaidi”.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...