Na Mwandishi wetu, Roma
Jukwaa la kwanza la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia limefanyika Jijini Roma kwa mafanikio makubwa, Italia na kuwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji zaidi ya 250 kutoka nchi zote mbili hasa katika kipindi hiki cha Uviko 19.

Pamoja na mambo mengine, jukwaa hilo limewawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kujadili fursa, uwezekano wa ubia, changamoto zinazokabili mazingira ya biashara na njia ya kuboresha mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Italia ambapo limendaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kwa kushirikiana na Kituo cha Taifa cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Taifa ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA). 
Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya ambapo Prof. Manya amewaeleza wawekezaji na wfanyabiashara kutoka Italia kuwa Tanzania kwa sasa imejikita kuwekeza katika miundombinu wezeshi ya uwekezaji, na kwamba hilo ndilo jambo ambalo Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Rais  Samia ameliweka suala la uwekezaji kama kipaumbele katika kuhakikisha kuwa wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi wanawekeza fedha na mitaji yao ili kukuza biashara na ajira kwa watanzania na kuwezesha uchumi wa Tanzania kusonga mbele.

“Tanzania inathamini uwekezaji na sasa inapiga hatua kwa kuweka miundombinu wezeshi pia Tanzania kama nchi tunamshukuru Mungu kwamba lengo la njozi yetu na maono yetu ya Tanzania Development Vision (2020-2025) imeweza kufikia malengo yake miaka mitano kabla muda uliokuwa umepangwa. Ambapo lengo kubwa lilikuwa ni kuifanya Tanzania kwenda katika viwango vikubwa vya kiuchumi na mwaka 2020 Tanzania ilitangazwa na Benki ya Dunia kuingia katika Uchumi wa kati,” amesema Prof. Manya.

Kadhalika, Prof. Manya ameongeza kuwa katika miaka mitano inayokuja Tanzania inapoelekea kumaliza njozi yake, inatamani kuendelea kukuza uchumi na ikiwezekana ihame katika uchumi wa kati na kuhamia uchumi wa juu……na ndiyo maana imejikita kuwekeza katika miundombinu ya reli ya kati itakayotumika kusafirisha mizigo kwa umeme, ujenzi wa bwawa kubwa linaloweza kuzalisha umeme wa kutosha pamoja na barabara za kusafiri kutoka mashariki kwenda magharibi na kaskazini kwenda kusini.

Ameongeza kuwa Tanzania inajivunia kuwa na hali ya amani na utulivu na katika nchi za ukanda wa maziwa makuu Tanzania inajivunia kuwa na siasa safi yenye utulivu na amani ndani yake.
“Mfano tumeona mwekezaji aliyewekeza katika kilimo cha Pareto ameshuhudia kwa kusema kuwa Tanzania ni nchi ya amani na utlivu na kuwasihi Waitaliano kuja kuwekeza Tanzania,” ameongeza Prof. Manya.

Kupitia jukwaa hili, tunaamini kuwa litachagiza chachu ya uwekezaji zaidi nchini Tanzania na kukuza biashara kati ya Tanzania na Italia.

Mwitikio ni mkubwa na wameonesha utayari wa kuja kuwekeza zaidi Tanzania pamoja na kukuza biashara miongoni mwetu na tumewahahakikishia kuwa Tanzania ni sehemu salama na yenye mazingira mazuri ya Uwekezaji na wameahidi kuwekeza zaidi Tanzania.
Nae Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo amesema kuwa kufanyika kwa Jukwaa la biashara na uwekezaji lengo lake kubwa ni kuwavutia wafanyabiashara na wewekezaji wa sekta mbalimbali kutoka Italia kuwekeza zaidi Tanzania ili kukuza uchumi wa pande zote mbili.

“Mwitikio ni mkubwa sana na tumeitikiwa na Serikali ya Italia vizuri sana pamoja na jumuiya za Italia za kibishara na pia kwa upande wa Tanzania pia mwitikio ni mkubwa pia,” amesema Balozi Kombo.

Mwenyekiti wa Chama Wawekezaji wa Hoteli Zanzibar, Bw. Paulo Rosso amewasihi wawekezaji kutoka Italia kuwekeza kwa wingi Tanzania kwa kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ni tulivu na salama.
“Tanzania ni sehemu salama kuwekeza, ni nchi ya amani, tulivu kwa uwekezaji, karibuni sana kuwekeza Tanzania,” amesema Bw. Rosso.

Katika Jukwaa hilo, Kampuni mbalimbali za Kiitaliano zimeonesha nia ya kuwekeza Tanzania ambazo ni pamoja na Kampuni ya utengenezaji Magari Ferari ambayo imeonesha utayari wa kuwekeza katika Gereji nchini Tanzania na Shirikisho la Uwekezaji katika Uchumi wa Buluu kutoka Italia pia limeonesha nia ya kuwekeza Tanzania.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...