MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kukosekana usawa katika upatikanaji huduma kwa Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi kunachangia kuendelea kuwepo maradhi ya Ukimwi nchini na watu kuendelea kupata maambukizi mapya ya maradhi hayo.

Mhe. Othman ameyasema hayo leo huko Kidimni Wilaya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja alipozungumza katika kilele cha Maadhimisho ya kitaifa Zanzibar ya Siku ya Ukimwi Duniani, ambapo Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Tuweke usawa kumaliza Ukimwi na Majanga mengine”.

Amefahamisha kwamba bila ya serikali na Jamii kwa jumla kufanya jitihada maalum za pamoja katika kuhakikisha watu wote wanapata huduma sawa, nchi na dunia kwa jumla itashindwa kutimiza lengo lililowekwa kimataifa la kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030.

Amesema kwamba hivi sasa dunia imeweka msisitizo wa kuhakikisha kwamba mataifa yote yanakuwa kitu kimoja na kuungana katika uumarishaji wa upatikanaji huduma za afya kwa kuzingatia upatikanaji wa rasilimali za afya za kutosha kwa wote.

Hata hivyo, Mhe. Makamu amesema takwimu zinaonesha kwamba Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika kupunguza maambukizo mapya ya maradhi ya Ukimwi kutoka kesi 366 mwaka 2010 kesi 177 mwaka huu wa 2021, jambo ambalo ni la kupongezwa ingwa kwa kuzidi kuchukua tahadhari za kuendelea kujinginga na maambukizo mapya hasa kwa vile Zanzibar kijiografia ni nchi ndogo.

Pia , Mhe. Othman alitahadfharisha jamii kwamba pamoja na mafanikio hayo, hali ya maambuzikizi Zanzibar sio nzuri kwa upande wa makundi maalum na kwamba yanahitaji kupewa kipaumbele kutokana na makundi hayo kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Amefahamisha kwamba takwimu zinaonesha kuwa watu wanaotumia madawa ya kulevya kwa kujidunga sindano ni asilimia 48 tu ndio wanaojitambua kuwa wanaishi na virusi vya Ukimwi, huku wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja wakiwa ni asilimia 60 tu ndio wanaojitambua kuwa wanaishi na Virusi vya maradhi hayo, wakati wanawake wanaofanya biashara ya kujiuza miili yao ni asilimia 73 ndio wanaojitambua kwamba wanaishi na Virusi vya maradhi hayo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe. Rashid Hadid Rashid, amesema kwamba pamoja na Takwimu kitaifa kuonesha kupungua, lakini hali ya maambukizi ya Ukwimwi katika Mkoa huo hasa wilaya ya Kati Unguja sio nzuri kwa kuwa wilaya hiyo inaongoza kwa kuwa na maambukizi mapya kutokana na kuwepo viashiria na vishawishi vingi vinavyochochea kasi ya ongezeko la maradhi hayo.

Amesema kwamba Wilaya hiyo inaviashiria vingi hatarishi ikiwemo upigaji wa ngoma holela za muda mrefu, mikusanyiko ya usiku , baa nyingi za kuuzia pombe na kuwepo vitendo vya kujamiiana kiholela na kwamba kunahitajika juhudi kubwa za kupunguza vitendo hivyo ili kudhibiti kasi ya Ukimwi Mkoani humo.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Dk. Saada Mkuya Salum, amesema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Tume ya Ukimwi Zanzibar na wadau mbali mbali inafanyia mapitio Sera na Mikatati ya kupambana na maradhi hayo ikiwa ni jitihada za kuongeza kasi ya mapambano ya maradhi ya ukimwi Zanzibar.

Amefahamisha kwamba Wilaya ya Kati ni eneo lenye kasi ya maambukizo mapya ya Ukimwi kutokana na kuwepo vichecheo vingi vya maambukizo hayo, hivyo jitihada maalum zinahitajika ili kuinusuru jamii isiendelee kuambukizwa maradhi hayo.

Naye Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Matifa la Kupambana na Ukimwi Duniani (UNAIDS) Zanzibar Dk.Gorge Loy, ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada kubwa inazochukua katika kupambana na maradhi ya Ukimwi na kutaka hatua zaidi za pamoja ziendelee kuchukuliwa ili kuzidisha kasi ya mapambano na kupata mafanikio zaidi dhidi ya maradhi hayo.

Hata hivyo, amesema kwamba katika kupambana na tatizo hilo, hivi sasa Duniani kunahitajika juhudi zaidi za pamoja za kuleta mageuzi na mabadiliko ya mifumo ya kisera na kuweka misingi ya usawa katika kulinda haki ya kila mtu ili na kuweza kupambana na changamoto zinazojiri katika mapambano dhidi ya Ukimwi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...