Na John Walter-Manyara


Serikali Mkoani Manyara imesema inatarajia kutoa elimu ya chanjo nyumba kwa nyumba na kuwahamasisha watumishi wa afya na ndugu wanaoleta wagonjwa Hospitali ili wawe mstari wa mbele kuchanjwa na kuwa mfano kwa wananchi wengine.

Msimamo huo wa serikali umetolewa Mjini Babati na Mratibu wa chanjo Mkoani hapa Suleiman Manoza wakati akieleza mikakati ya mkoa juu ya utoaji wa chanjo ya Uviko-19 katika kikao kazi cha tathimini ya utekelezaji wa mpango shirikishi."Watoa huduma 666 wanaendelea kupewa elimu kila wilaya ili watoe chanjo kwa wananchi," alisema Manoza

Aidha alisema katika mpango wao wataimarisha huduma ya mkoba kwa kutembea nyumba kwa nyumba ili kusaidia kuleta matokeo chanya.

Mratibu huyo wa chanjo alisema ili mkoa ufikie asilimia 60 ya watu waliochanjwa mwaka 2022 wameiomba wizara ya afya kuwapatia Chanjo ya Janssen ambayo inatolewa mara moja itakayowafaa wananchi wa mkoa huo hasa wafugaji ili kuwasaidia kuepuka kuchanjwa mara mbili kitu ambacho kinaweza kusababisha wengine wakakimbia au chanjo ikaisha muda wake.

Vile vile alisema watawahamasisha wafanyakazi wa afya wakachanjwe ili iwe rahisi kwenda vijijini kuhamasisha watu ambao hawajachanja.

Akitoa taarifa ya chanjo mganga mkuu wa mkoa wa Manyara Dk. Damas Kayera alisema mkoa huo ulipewa dozi 15,000 na zote zimeisha.Dk. Kayera alifafanua kuwa serikali kwa awamu ya pili imeshaleta chanjo ya Sinopharm ambapo wanatarajia kuchanja dozi 570,000 ambazo zimeletwa.

Alisema kwa siku wanachanja watu 60 hivyo hawaridhiki na kasi hiyo ndio maana wamekutana kuweka mikakati ya kuwavusha.

Mtaalamu huyo wa afya alisema kwa kasi wanayoenda nayo wasipoongeza nguvu wanaweza kutumia miaka miwili kumaliza dozi mpya waliyopewa.Mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere akifungua kikao kazi hicho alisema hadi kufika mwezi Oktoba mwaka huu walikuwa wameshachanja watu zaidi 13,000 mkoa mzima.Makongoro aliwaomba wataalam wa afya, viongozi na wananchi kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha chanjo hiyo.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa huo Carolina Mthapula aliwasihi wataalam kwenda kuboresha taarifa zao na kuongeza nguvu ya uhamasishaji.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...