*****************

Na. John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe. Innocent Bashungwa amesema Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa mashindano ya dunia mchezo wa soka kwa wenye ulemavu (WAF) baada ya kumalizika mashindano ya dunia ya mchezo huo Oktoba , 2022 nchini Uturuki.

Mhe. Bashungwa ameyasema hayo leo Disemba 3, 2021 alipoambatana na Katibu Mkuu wa Wizara yake, Dkt. Hassan Abbasi, Mkurugenzi wa Michezo Yusuph Omary na Kaimu Katibu wa Baraza la Michezo la Taifa, Neema Msitha wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka la Bara la Afrika kwa wenye Ulemavu jijini Dar es Salaam ambao pamoja na mambo mengine una lengo la kuwachagua viongozi wakuu wa Shirikisho hilo.

Aidha, ametoa wito kwa mkutano huo wa ngazi ya juu kabisa Afrika kufikiria kuyaleta mashindano hayo kutokana na mazingira wezeshi na utashi mkubwa wa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Amewataka kutumia mashindano haya kuelimisha dunia kupinga ubaguzi na mila potofu za kuwatenga na kuwabagua wenye ulemavu kwa kuwa ni binadamu sawa na wengine na kwamba wanauwezo sawa na wengine.

Ametumia tukio hilo muhimu kukaribisha mataifa yote ya Afrika kuja kutembelea kilele cha Afrika; Mlima Kilimanjaro na vivutio mbalimbali vya utalii ikiwa ni pamoja na utalii wa baharini katika kisiwa cha Zanzibar.

Naye Makamu wa pili wa Shirikisho la soka dunia kwa wenye ulemavu ( WAF) Mateus Wildack ametuma salamu za pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu kwa uongozi mahiri wa kuiletea Tanzania maendeleo ya haraka na kuwashirikisha kikamilifu wenye ulemavu na kuwapa kipaumbele kwenye maendeleo hayo ikiwa ni pamoja na eneo la michezo ambayo imefanya vizuri sana.

Ameisifia Serikali kwa uratibu makini iliyofanya kwenye mashindano hayo yaliyofanyika kwa siku saba jijini Dar es Salaam na kuelezea kuwa yamefanyika kitaalam.

Rais wa Shirikisho hilo wa Afrika ( FAAF) Mchungaji Richard Nii Adesah amepongeza Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na uwezeshaji iliyotoa katika kipindi chote cha mashindano ambapo amesema mkutano huo utasaidia kuleta mabadiliko makubwa kwenye michezo ya walemavu katika Bara la Afrika.

Aidha amewataka mataifa yote ya Afrika kutokubali kugawanywa na kitu chochote kutokana na umoja imara uliojengeka baina ya nchi zote kutokana na mashindano hayo ya Afrika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...