Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na   aliyekuwa mwanariadha wa Tanzania John Stephen Akhwari ambaye anakumbukwa kwa kushiriki katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 1968 nchini Mexico. Mheshimiwa Majaliwa alikutana na mwanariadha huyo wakati alipokagua mradi wa ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari ya Gehandu wilayani Mbulu, Januari 24, 2022 na alimzawadia Sh. 500,000 ikiwa ni ishara ya kutambua heshima aliyolipatia taifa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa Bashnet, Babati Vijijini akiwa katika ziara ya Mkoa wa Manyara, Januari 24, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la Msingi la ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya wilaya ya Mbulu akiwa katika ziara ya Mkoa wa Manyara, Januari 24, 2022. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere, wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Manyara,  Simon Lulu na kulia ni Mbunge wa Babati Vijijini, Flatei Masay. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Muonekano wa jengo la utawala la Halmashauri ya wilaya ya Mbulu ambalo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo hilo, Januari 24, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

**********************

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuendelea kuifungua Tanzania kwa kujenga barabara katika maeneo mbalimbali nchini ili Watanzania wazitumie katika kufanya shughuli kijamii zikiwemo biashara.

Aliyasema hayo jana (Jumatatu, Januari 24, 2022) alipozungumza na wananchi wa Dareda akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali mkoani Manyara.

Alisema kuwa Serikali ipo katika mpango wa ujenzi wa barabara za Mbulu-Hydom, Karatu-Mbulu, Hydom Mkalama-Sibiti-Meatu-Bariadi-Maswa hadi Busega

“Barabara zote hizi zinatakiwa kuwekwa lami ili mzitumie fursa hizi kufanya biashara na kusafiri kwa urahisi, leo hii tunajenga makao makuu ya Halmashauri ya Mbulu pale Dongobesh, hivyo tunajenga barabata kutoka Dongobesh kuja hapa Dareda Centre ili halmashauri ifikike kwa urahisi”

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwaondoa hofu wananchi wote waliolipia huduma ya kuunganishiwa umeme ambao bado hajapata huduma hiyo kuwa wataunganishiwa kwani tayari wakandarasi wameshapelekwa katika maeneo yao.

“Watu wote waliolipia na watakaolipia huduma ya kuunganishiwa umeme wataunganishiwa. Malengo ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote vinapata umeme ifikapo Desemba mwaka huu.”

Akizungumzia kuhusu utunzaji wa mazingira, Mheshimiwa Majaliwa aliwasisitiza Watanzania watunze mazingira na wapande miti kwa wingi ili nchi iweze kupata mvua za kutosha. “Tusiruhusu watu kuharibu mazingira tutakosa maji, pandeni miti kwa wingi ili kuliepusha Taifa kugeuka kuwa jangwa.”

Alisema katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo mito iliyokuwa ikitiririsha maji inaanza kukauka kutokana na uharibifu wa mazingira, hivyo kusababisha kupungua kwa vyanzo vya maji.

Awali, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na kuwapongeza kwa ubunifu mzuri kwani jengo lao ni la mfano. Jengo hilo hadi kukamilika linatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 6.3.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...