SERIKALI imesema kuwa zaidi ya Watumishi wa Umma 180,000 wamepandishwa madaraja ambapo Wilaya ya Nkasi iliyopo mkoani Rukwa imenufaika na promosheni kwa watumishi wake 837 kuwa miongoni mwa waliopandishwa madaraja huku watumishi zaidi ya 40 wakibadilishiwa kada zao za utumishi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi wakati akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ambapo pia amesisitiza viongozi wa kiserikali na kisiasa kuacha tabia ya kuwadhalilisha watumishi wa umma pindi wanapokosea na badala yake wafuate taratibu za kumuajibisha mtumishi pindi anapokosea.

Ndejembi amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejikita katika kuwaboreshea maisha watumishi wa umma huku akiwataka kufanya kazi kwa bidii na kuwa wabunifu kazini.

Amesema kuwa Ofisi ya Rais Utumishi itaendelea kutetea haki za watumishi wa umma usiku na mchana na kwamba hakuna haki ya mtumishi yeyote itakayopotea iwe ni kulipwa malimbikizo ya mishahara, kupandishwa madaraja au kubadilishiwa kada.

" Rais Samia ameweka kipaumbele kabisa katika kutatua changamoto zenu watumishi, Ndio maana katika kipindi kifupi alichoingia amefanya mambo makubwa kwa haraka ikiwemo upandishwaji wa madaraja ambapo hapa Nkasi pekee zaidi ya Watumishi 837 wamepandishwa na watumishi zaidi ya 40 wamebadilishiwa kada, Haya ni mambo ambayo kwa muda mrefu mlikua hamjayapata.

Kwa upendo wa Rais Samia kwetu watumishi hebu chapeni kazi kwa ubunifu, simamieni rasilimali fedha, simamieni rasilimali watu mnaowaongoza, ukiteuliwa kuwa Mkuu wa Idara tenga muda wa kuwasikiliza walio chini yako, wafuateni hadi katika ngazi ya kata msiishie kukaa maofisini tu, fanyeni kazi ya kumsaidia Rais wetu,"Amesema Naibu Waziri Ndejembi.

Naibu Waziri Ndejembi pia ametoa wito kwa baadhi ya viongozi kuacha kuwafokea na kuwadhalilisha watumishi wa umma hadharani pindi wanapokosea badala yake wafuate utaratibu wa kumuajibisha mtumishi anapokosea kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizowekwa kwenye utumishi wa umma.

"Mtumishi wa umma anapokosea siyo busara kumfokea na kumdhalilisha hadharani, waiteni faragha muwaeleze wapi walipokosea, siyo vema kumfokea mtumishi mbele za watu tena wale anaowahudumia au kuwasimamia, tunataka watumishi wa umma waheshimiwe," Amesema Ndejembi.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi iliyopo mkoani Rukwa.
Watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi wakati alipofika kuzungumza nao.
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Peter Lijualikali akizungumza katika mkutano wa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, Aide Kenani akizungumza katika mkutano wa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...