Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Jenista Mhagama akitoa taarifa yake Kwa umma kuhusu mwelekeo wa mifumo ya utendaji kazi katika Utumishi wa umma. Waziri Jenista anatoa taarifa hiyo alipokua akizungumza na Watendaji wa Wizara hiyo katika Ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Kiserikali Mtumba jijini Dodoma.
Baadhi ya Watendaji katika Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora wakimsikiliza Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Jenista Mhagama alipokua akizungumza nao leo jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Jenista Mhagama akizungumza na Watendaji wa Wizara hiyo leo katika Ofisi za Wizara Mtumba jijini Dodoma.


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Jenista Mhagama amewataka Watendaji Wakuu wote wa Taasisi za Umma kufanya maandalizi na kusimamia utekelezaji wa mfumo mpya wa upimaji utendaji kazi kwa watumishi wa umma na taasisi zake (Opras).

Agizo hilo amelitoa leo katika Ofisi za Wizara hizo zilizopo Mji wa Kiserikali Mtumba jijini Dodoma wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Wizara hiyo kuhusu mwelekeo wa mifumo ya utendaji kazi katika Utumishi wa Umma.

Waziri Mhagama amesema kuwa Wizara yake imefanyia kazi agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa kwao wakati wa kikao chake na Mawaziri na Manaibu Waziri ambapo alieleza bayana kutoridhishwa na namna ambavyo mfumo huo wa 'OPRAS' unavyofanya kazi.

Katika kikao hicho na Mawaziri na Manaibu Waziri, Rais Samia alisema kuwa upimaji utendaji kazi kupitia OPRAS hauakisi hali halisi ya utendaji kazi kwa watumishi hali inayoleta hisia za kupendeleana au kuoneana. Pia matokeo ya upimaji utendaji kazi hayatumiki ipasavyo katika kufanya maamuzi ya kiutumishi.

Waziri Mhagama amesema katika kuendelea kutumia mfumo huo wa OPRAS uzoefu inaonesha kuwa mfumo huo ulioanzishwa mwaka 2004 una mapungufu hivyo kuamua kuchukua hatua za haraka za kuwaelekeza wataalamu wake kumaliza changamoto hiyo kwa kuja na mfumo mpya ambao utaanza kufanya kazi Julai 1, 2022.

" Katika kutekeleza agizo la Rais Samia tayari Ofisi yangu imechukua hatua kadhaa ikiwemo kuja na mfumo wa Kielektroniki ambao utakua na manufaa Kwa watumishi ikiwa ni pamoja na kuwarahisishia uandaaji wa mikataba ya kazi kwa kuwa na malengo na shabaha za kila mtumishi zitawekwa katika mfumo Rafiki na kupunguza matumizi ya karatasi.

Mfumo huu unategemewa kuanza kutumika Julai 1, 2022, hivyo niwatake Watendaji Wakuu wote wa Taasisi za Umma kufanya maandalizi na kusimamia utekelezaji wa mfumo huu kikamilifu  Kwa kuzingatia maelekezo yatakayotolewa na Katibu Mkuu (Utumishi), Pia wahakikishe wanatenga bajeti kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa mfumo huu kwenye taasisi zao," Amesema Waziri Mhagama.

Amesema kuwa mfumo mwingine ni mfumo wa uwazi wa kupima utendaji kazi wa taasisi ambapo unajulikana kama mfumo wa mikataba ya utendaji kazi katika ngazi ya Taasisi na ulianza rasmi mwaka 2018.

Amesema mfumo huu pia umefanyiwa kazi ili uwe wa Kielektroniki ni wa makubaliano ya kimaandishi kati ya Serikali na Taasisi za Umma kuhusu malengo ambayo Taasisi husika inatekeleza katika kipindi cha mwaka mmoja.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...