*
Asema waliojenga kwenye vyanzo vya maji, maeneo ya jeshi kuhama


Na Grace Semfuko,MAELEZO

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye, amesema hakuna maeneo yatakayoachwa kwenye zoezi la uwekaji wa anwani za makazi nchini, na kwamba maeneo yote yenye migogoro sugu ya ardhi na mipaka, na ambayo mpaka sasa hayajapitiwa na zoezi hilo yatasubiri utatuzi wake.

Amesema si kwamba maeneo yenye migogoro yameachwa moja kwa moja katika zoezi hilo, bali yatapewa namba lakini hayatawekewa anwani za makazi, lengo likiwa ni kuharakisha utatuzi wa migogoro hiyo ambayo mingi ni ya muda mrefu.

Ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua na kuhamasisha mwenendo wa zoezi la uwekaji wa amwani za makazi katika Jiji la Dar es Salaam.

“Kwenye hili zoezi kuna baadhi ya maeneo kwa kweli yana migogoro ya hapa na pale, kuna mahali watu wamekaa maeneo ambayo sio rasmi mfano kwenye vyanzo vya maji, migogoro ya mipaka, katika majeshi na wananchi, wengine wamejenga kwenye maeneo ya jeshi la wananchi, sasa kuna maeneo ambayo kwa makusudi tumeamua kuacha kupeleka anwani za makazi mpaka tukamilishe kusuluhisha migogoro iliyopo, na ni vizuri wananchi wetu wakatuelewa maana wengine wanahoji mbona hapa pameachwa?, niwahakikishieni kuwa hakuna atakaeachwa” amesema Nape.

Lakini ametoa angalizo kwa wananchi wanaoishi kwenye baadhi ya maeneo kuwa, zoezi hilo halitawafikia kutokana na asili ya maeneo hayo.

"Sasa wapo ambao watarasimishwa, lakini wapo ambao watalazimika kuhama, ni vizuri maneno mengine magumu tuambiane, watu wanapokaa kwenye vyanzo vya maji hatuwezi kuwaacha, inaweza kuwa ngumu kidogo, lakini tutaweza kutumia nguvu kumwondoa mtu mmoja ili tuokoe watu wengi, na hili nalisema wazi kabisa, hatuna namna, kuna maeneo yatarasimishwa ikimpendeza Rais, lakini mengine hapana! mfano mtu anavamia eneo la jeshi tunamuachaje?” amesema Nape

Kuhusu maeneo yenye migogoro yaliyoachwa Nape anasema ni zoezi linalohitaji utatuzi kupitia Wizara mbalimbali ambazzo kwa pamoja wataweza kuitatua migogoro hiyo.

“Lakini pale ambapo kuna mgogoro mahali ambapo wananchi wanakaa maelekezo ni kwamba, pale tutatoa namba lakini hatutaweka anwani za makazi kwenye eneo hilo, lakini kitendo hicho sasa kitatumika kuharakisha utatuzi wa mgogoro uliopo maana yapo maeneo ambayo migogoro inachukua muda mrefu sana, hivyo katika kukamilisha zoezi hili, katika taarifa zetu tutaonesha kwamba hapa tumepaacha kwa sababu ya mgogoro kadhaa, na kwa sababu taarifa hizi tunampelekea Mheshimiwa Rais na migogoro hii mingi inataka utatuzi wa Wizara zaidi ya moja na sasa mwenye wizara zake Rais, hii itatupa urahisi wa kutatua migogoro hiyo kwa haraka” amesema Nape.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mhe. David Silinde amesema anwani za makazi ni muhimu katika kutambua maeneo na kuwataka wananchi kuendelea kushiriki ipasavyo katika zoezi hilo ambalo limefikia asilimia 94.89 mpaka sasa.

Nae mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makala amesema mkoa huo unaendelea kutekeleza zoezi hilo na kwamba kwa Mkoa wa Dar es Salaam, na kwamba limekuwa na mwitikio mkubwa huku akiitaja hatua hiyo kuwa imetokana na utoaji wa elimu ya kutosha kwa wananchi pamoja na kuhamasisha ipasavyo. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...