NA  YEREMIAS  NGERANGERA…NAMTUMBO

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Dkt Julius Kenneth Ningu aliyasema hayo wakati wa kupokea mabomba ya chuma (steel pipe) kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji uliosimama kwa miaka mitano toka 2017 mpaka 2022.

Dkt Ningu alifafanua sababu ya mradi huo kuchelewa ni kutokana na kuchelewa kutengenezwa kwa mabomba ya chuma yaliyotakiwa kutumika katika kutekeleza mradi huo .

Aidha Dkt Ningu alidai kitendo cha serikali kusimamia utengenezaji na kusimamia upatikanaji wa mabomba hayo ya chuma kutamaliza kilio cha muda mrefu cha wananchi wa kijiji cha Kumbara na Litola ambao mara kwa mara walikuwa wakiilalamikia serikali kwa kutokamilisha mradi huo wa maji.

Meneja wa RUWASA wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma David Mkondya alisema mkataba wa mradi wa  maji Litola –Kumbara ulisainiwa tarehe 12 oktoba 2013 na utekelezaji wake ulianza tarehe 30 junuari 2017 na ulitarajiwa kukamilika tarehe 5  Desemba 2019 chini ya mkandarasi ajulikanaye kwa jina la Vibe International company LTD.

Hata hivyo Mkondya katika taarifa yake kwa mkuu wa wilaya huyo alitaja kazi zilizofanyika katika mradi huo kuwa ni ujenzi wa matenki mawili yenye  ujazo wa lita 100,000 na lita 75,000,ujenzi wa chanzo cha kukusanyia maji,uchimbaji na ulazaji wa mtandao wa mabomba ya usambazaji maji , ujenzi wa vituo 32 vya kuchotea maji katika kijiji cha Litola na Kumbara.

Mkondya pia alitaja kazi ambazo hazijafanyika kuwa ni pamoja na ununuzi na ulazaji wa bomba kuu kutoka katika chanzo mita 7000 na ujenzi wa chemba katika bomba kuu katika chanzo baada ya kulaza mabomba ya chuma.

Mwenyekiti wa bodi ya maji katika kijiji cha Kumbara na Litola Bosco Rabanus Gingo aliishukuru serikali kwa kusimamia uagizaji na usimamiaji wa utengenezaji wa mabomba ya chuma kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji wa kijiji cha Litola na Kumbara.

Bwana Gingo alidai tatizo kubwa la kusimama kwa mradi huo lilikuwa utengenezaji wa mabomba ya chuma hivyo kuwasili kwa mabomba hayo kumewafanya wananchi waamini kuwa serikali yao inawajali wananchi wake alisema mwenyekiti huyo.

Diwani wa kata ya Litola Paulo Kamilius Fussi aliipongeza serikali kwa kusimamia utengenezaji wa mabomba ya chuma ili kukamilisha mradi wa maji wa kijiji cha Litola na Kumbara ambao unalalamikiwa sana na wananchi.

Naye mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi wilaya ya Namtumbo bwana Aggrey Mwansasu pamoja na kuipongeza serikali  kusimamia utengenezaji wa mabomba ya chuma na kuyaleta katika eneo la mradi ili kuhakikisha mradi huo wa maji unakamilika kwa asilimia mia kwa lengo la kutimiza ilani ya chama cha mapinduzi ya upatikaji wa huduma ya maji kiurahisi.

Yusta Nikata ni mwananchi wa kijiji cha Kumbara alisema kupokelewa kwa mabomba hayo ya chuma inawapa imani kuwa sasa mradi huo wa maji unaenda kukamilika tofauti na hapo awali ambapo walikuwa wanaamini kuwa mradi huo umetelekezwa licha ya viongozi wa chama na serikali kueleza juhudi za serikali za kuumalizia mradi huo wananchi waliondoa imani hiyo .

Mabomba ya chuma yaliyopokelewa ni yenye jumla ya urefu wa mita 4698 kati ya mita 7000 zinazohitajika ,huku gharama za malipo kwa utengenezaji wa mabomba yote kwa mita 7000 ni shilingi 499,557,708.80 na kiasi kilicholipwa ni shilingi 127,006,197.17 kama malipo ya awali.



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...