JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

TAARIFA KWA UMMA


WIZARA ya Maliasili na Utalii imepewa dhamana ya kusimamia uhifadhi wa maliasili, malikale na maendeleo ya Utalii nchini kwa kushirikiana na wadau. Sekta hii huchangia pato la Taifa kwa asilimia 17 na zaidi ya asilimia 25 ya fedha za kigeni.


Kwa nyakati tofauti, Wizara imepokea taarifa kuhusu uvamizi wa wanyamapori katika mashamba na makazi ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini. Katika kutatua changamoto hii, Wizara imefanya tathmini na kubaini wanyamapori hatarishi na waharibifu ni pamoja na tembo, simba, mamba na viboko ambao matukio yao yamekuwa yakijirudia  hasa katika Wilaya 53 kati ya 134 nchini. 


Uvamizi wa wanyamapori hawa husababisha taharuki, uharibifu wa mali, majeraha na wakati mwingine vifo. Aghalabu, maisha ya wanyamapori nayo huathirika pindi wananchi wanapolipiza kisasi na kuwadhuru. Migongano hii husababishwa na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja;

  1. Mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha ukame wa muda mrefu na mafuriko; 

  2. Kupungua kwa malisho kunakosababishwa kuenea kwa mimea vamizi katika baadhi ya maeneo yaliyohifadhiwa; 

  3. Uchungaji wa mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa husababisha wanyamapori kutoka kwenye maeneo ya hifadhi na hivyo kuongeza migongano kwenye maeneo ya wananchi; na  

  4. Matumizi holela ya ardhi na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu hasa katika maeneo ya jirani na hifadhi yakiwemo shoroba na mtawanyiko wa wanyamapori.


Katika kukabiliana na migongano hiyo, Wizara inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Kusimamia Utatuzi wa Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori wa mwaka 2020-2024. Sambamba na Mkakati huo Wizara inatekeleza Mwongozo wa Mbinu Rafiki za Kudhibiti Wanyamapori Wakali na Waharibifu na kuwezesha uaandaji wa mipango ya matumizi ya bora ya ardhi kwa vijiji vilivyo pembezoni mwa maeneo yaliyohifadhiwa. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inafanya mapitio ya Sera ya Wanyamapori ya mwaka 2007 pamoja na Sheria na kanuni zake. Halikadhalika,Wizara inaendelea kufanya tafiti ili kubaini mbinu na mikakati bora ya kukabiliana na changamoto hii. 


Hatua zingine ni Pamoja na; 


  1. Hatua za muda mfupi

  • Kuwajengea uwezo wananchi kwa kuwapatia mafunzo na vifaa vya kujilinda ambapo hadi sasa mafunzo yametolewa kwa wakufunzi 660 katika Wilaya 21 kati ya 53 zenye migongano. Wizara inaendelea kukamilisha mafunzo kwenye Wilaya zilizosalia;

  • Kuanzisha vituo 11 vya kudumu kwa Askari wanyamapori kwenye maeneo yanayoathirika zaidi ili kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao;

  • Kuimarisha kanzidata ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori;

  • Namba maalum za simu zimetolewa kuwezesha wananchi kutoa taarifa za matukio ya wanyamapori bila malipo ili kupata msaada wa haraka;

  • Kuhamisha wanyamapori wakali na waharibifu kutoka kwenye makazi kwenda maeneo ya hifadhi;

  • Vizimba viwili vya mfano vimejengwa Ziwa Rukwa kwa ajili ya kujikinga na mamba na viboko. Wizara inafanya taratibu za kuhakikisha wadau (Halmashauri na wadau wengine) wanaviona ili waweze kwenda kujenga kwenye maeneo yao;

  • Uvunaji wa viboko hatarishi maeneo ya bwawa la Mtera na Ziwa Babati,na  jitihada zitaendelea kwenye maeneo mengine; na

  • Kutoa vibali vya uvunaji wa mamba katika maeneo yenye migongano.


  1. Hatua za muda mrefu

  • Kununua helikopta kwenye kila kanda ili kushughulikia matatizo kwa haraka; 

  • Kuendelea kulipa kifuta jasho na machozi kwa wananchi walioathirika; 

  • Kuendelea kuimarisha doria za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu; 

  • Kuanzishwa Kamati ya Kudumu ya kuandaa, kutekeleza na kusimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi hasa katika maeneo yenye migongano;

  • Kuwajengea uwezo wananchi kwa kuanzisha miradi ya kuongeza kipato. 

  • Kupendekeza uanzishwaji wa mtaala wa namna ya kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu katika shule za ngazi zote; na


Pamoja na jitihada zinazoendelea kutolewa, Wizara inapenda kuwakumbusha wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi za wanyamapori kuzingatia yafuatayo:

  1. Maelekezo yanayaotolewa na wataalamu wa Uhifadhi ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu; 

  2. Wananchi kujiepusha kuwasogelea wanyamapori;

  3. Kuchukua tahadhari kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo au pembezoni mwa hifadhi; maeneo yenye mamba na viboko; mapito na mtawanyiko wa wanyamapori.

  4. Kujiepusha na tabia ya kupambana na wanyamapori wanapoingia kwenye maeneo yao; 

  5. Kutoshiriki katika zoezi la kufukuza wanyamapori wakali na waharibifu kwa  wazee, watoto, wajawazito, wenye changamoto mbalimbali za ulemavu, na waliotumia kilevi;

  6. Kuepuka matembezi yasiyo ya lazima nyakati za usiku kwa wananchi waishio pembezoni mwa maeneo yaliyohifadhiwa na ikibidi watembee zaidi ya mtu mmoja; 

  7. Kuepuka uvuvi hatarishi hususani kuvua nyakati za usiku na matumizi ya vifaa duni; na

  8. Kutoa taarifa za matukio ya uvamizi wa wanyamapori wakali na waharibifu haraka kupitia namba za kupiga simu bure zilizotangazwa na Wizara. 


Na.

Kituo

Namba za kupiga simu bure

1

Wizara ya Maliasili na Utalii-Dodoma

0800110076

2

Hifadhi ya Ngorongoro

0800110087

3

TAWA  Makao Makuu (Morogoro)

0800110093

4

TAWA – Kanda ya Kati (Manyoni)

0800110089

5

TAWA – Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Iringa)

0800110090

6

TAWA- Kanda ya Kusini Mashariki (Masasi)

0800110067

7

TAWA – Dar es Salaam na Pwani

0800110098

8

TAWA- Kanda ya Kusini Mashariki (Tunduru)

0800110054

  9

TAWA- Kanda ya Magharibi (Tabora)

0800110048

10

TAWA- Kanda ya Kaskazini (Arusha)

0800110027

11

TANAPA – Kanda ya Mashariki (Mikumi)

0800110099

12

TANAPA- Kanda Kusini (Mbalali)

0800110068

13

TANAPA- Kanda ya Magharibi (Bunda)

0800110059

14

TANAPA- Kanda ya Kaskazini (Mkomazi)

0800110046


HITIMISHO

Serikali itaendelea kutoa kifuta jasho na machozi kwa mujibu wa taratibu za kisheria kwa wananchi wote walioathirika na watakaoathirika. Aidha, Serikali itaendelea na jitihada za kudhibiti na kukomesha matukio haya. Wizara inatoa pole kwa wananchi wote walioathirika kwa namna mbalimbali kutokana na mgongano baina ya binadamu na wanyamapori. Maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa wananchi na mali zao wanakuwa salama kila mahali.



Imetolewa na:

Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (MB)

Waziri – Wizara ya Maliasili na Utalii

Mei 2022


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...