Na Karama Kenyunko Michuzi TV
MAHAKAMA Kuu, Masijala Kuu  imeamuru wabunge wa vitu maalumu 19 kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, kubaki na nafasi zao bungeni mpaka mapingamizi yaliyowekwa na Chadema yatakaposikilizwa Juni 29, 2022 na kutolewa uamuzi.

Amri hiyo imetolewa na Jaji Mustapha Ismail  anayesikiliza kesi hiyo.

Mapema leo Juni 27,2020 kesi hiyo iliitwa mahakamani hapo  kwa ajili ya kutajwa kwa maombi  kibali cha kufungua kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho baada ya kufanyia marekebisho.

Hata hivyo, kabla ya kesi kutajwa, Chadema kupitia mawakili wao, wakiongozwa  na Peter Kibatala wamewasilisha Mapingamizi matatu mahakamani hapo.

Kwa mujibu wa wakili wa Kina Mdee , Ipilinga Panya amedai  Chadema wamewasilisha pingamizi hilo likiwa na hoja tatu ambazo zote zinazozungumzia dosari zilizopo katika viapo vya wateja wao.

Mahakama hiyo imepanga kusikiliza shauri hilo Juni 29 mwaka huu ambapo Mdee na wenzake 18 wanaiomba mahakama hiyo iwape kibali cha kufungua kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho.

Aidha, mahakama imewataka wajibu maombi katika shauri hilo kuwasilisha viapo  kinzani Juni 28 mwaka huu  na waleta maombi kuwasilisha hoja za nyongeza Juni 29 mwaka huu kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo saa 8 mchana.

Juni 22, 2022 Jaji John Mgeta,  aliondoa  kesi hiyo iliyokuwa imefunguliwa na wabunge hao baada ya kukubaliana na pingamizi la awali liliowasilishwa na mawakili wa Chadema kuwa maombi ya kina Mdee yalikuwa na dosari za kisheria. 

Inadaiwa, Mdee na wenzake walikosea jina la mjibu maombi wa kwanza ambaye ni Chadema na kwamba wamemshtaki mtu ambaye kisheria hayupo.

"Mdee na wenzake walipaswa kufungua maombi hayo kwa kutaja jina sahihi la bodi hiyo kwa mujibu Sheria ambapo walitakiwa kuandika “Registered Body of Trustees” badala ya Body of Trusties, waliyoandika wao".

Amesema kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa kifunga 21 (1) ambacho kinaitaka chama chochote cha siasa kikishapata usajili wa kudumu kiwateue  na kuwasajili hao Trustees kwa mujibu wa sheria ya wadhamini.

Pia amesema taarifa hiyo ilisainiwa na mawakili wa waleta maombi kinyume cha sheria na hivyo kufanya iwe na dosari.Hata hivyo alieleza kwamba dosari hiyo wanaweza kufanyia marekebisho.

Wabunge na wanachama hao wa zamani wa Chadema, walivuliwa rasmi uanachama wa chama hicho, usiku wa kuamkia Mei 12, 2022 baada ya Baraza Kuu la Chadema kutupilia mbali rufaa zao walizozikata wakipinga uamuzi wa Kamati Kuu iliyowavua uanachama.

Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa Chadema, ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu (CC), Esther Matiko na Ester Bulaya; aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara), Hawa Subira Mwaifunga na aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.

Wengine, ni aliyekuwa Katibu mkuu wa Baraza la Vijana la chama hicho (BAVICHA), Nusrat Hanje; aliyekuwa Naibu katibu mkuu wa Bawacha (Bara), Jesca David Kishoa; Cecilia Pareso, Agnesta Lambart, ambaye alikuwa mwenezi wa Bawacha na Tunza Malapa, aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, mkoani Mtwara.

Katika orodha hiyo, wamo pia Asia Mohammed, aliyekuwa Naibu Katibu mkuu wa Bawacha (Zanzibar), Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...