Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Robert Mallya akiwaonesha maeneo ya Taasisi hiyo wageni kutoka Taasisi
ya Moyo Uganda walipotembelea JKCI leo kwaajili ya kuangalia huduma
zinazotolewa na Taasisi hiyo pamoja na kujifunza namna ambavyo Taasisi hiyo
inaendesha shughuli zake.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye pia ni Mkuu wa idara ya magonjwa ya moyo kwa
watoto Sulende Kubhoja akielezea huduma zinazotolewa katika idara hiyo kwa
wageni kutoka Taasisi ya Moyo Uganda walipotembelea JKCI leo kwaajili ya
kuangalia huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo pamoja na kujifunza namnaambavyo Taasisi hiyo inaendesha shughuli zake.

 

Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

WATAALAMU 20 kutoka Taasisi ya Moyo Uganda wametemblea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  iliyopo jijini Dar es Salaam kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinatolewa pamoja na kujifunza namna ambavyo taasisi hiyo inavyoendesha shughuli zake.

Akizungumza na waandhisi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema baada ya kusikia mafanikio yaliyopatikana katika Taasisi hiyo wataalamu hao kutoka nchini Uganda wameona ni vyema kwenda kujifunza mafanikio hayo pamoja na changamoto zake ili nao wafikie hatua kama ya JKCI.

Prof.Janabi alisema tangu Taasisi hiyo ianzishwe mwaka 2016 imekuwa na mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo kwa kufanya upasuaji kwa wagonjwa 8663 na kuona wagonjwa zaidi ya laki sita  na hivyo kuwa hospitali bora ya Serikali inayotoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo katika nchi za  Afrika Mashariki na Kati.

“Mwaka 2017 baadhi ya wabunge kutoka nchini Uganda walitembelea Taasisi yetu kwa ajili ya kujifunza na leo hii tumepokea wataalamu 20 kutoka nchini humo ambao nao wamekuja kujifunza jinsi tulivyofanikiwa katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo. Sisi tumefanikiwa kwa kuwa Serikali inatuunga mkono kwa zaidi ya asilimia 120 na hata upasuaji tunaoufanya ni salama”,.

“Taasisi yetu inapokea wagonjwa kutoka nchi za Afrika ya Mashariki na Kati ikiwemo  Uganda ambapo kwa mwaka huu tumeshafanya upasuaji wa moyo kwa watoto sita ambao walikuwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo. Watoto hawa wanaendelea vizuri na walisharudi nchini mwao”, alisema Prof. Janabi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu alisema amefurahi kuona wenzao kutoka nchini Uganda wamekuja kuwatembelea kwaajili ya kujifunza  wanachokifanya na na kuwaeleza walipofikia ili wawasaidie kutokana na mapungufu waliyokuwa nayo.

 “Ukiangalia historia ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete haitofautiani na ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Moyo Uganda kwani zote zimetokea katika Hospitali za  Taifa, jambo la muhimu ni kuwatia moyo ili wasikate tamaa na kuweza kufika  hapa tulipofika sisi kwani wao wako hatua tatu nyuma yetu”.

Prof. Mahalu ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu alisema Taasisi ya Moyo Uganda ni ya Serikali,  kwani huduma za matibabu ya moyo bila kushikiliwa na Serikali zinagharama kubwa na zikiwa na utashi wa kisiasa kuwa zinawasadia  watu wataweza kupata  kila kitu ambacho watakitaka na hivyo kuweza kufanya vizuri katika kutoa huduma kwa wagonjwa.

Dkt. James Magara ambaye ni Mwenyekiti wa bodi ya Taasisi ya Moyo Uganda alisema wamekuja nchini kujifunza katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ili wasifanye makosa kiutendaji kwani wao wako katika hatua za mwanzo tangu taasisi hiyo ianzishwe na kama wataanza vizuri wataweza  kufanya vizuri zaidi.

“Tanzania na  Uganda tumekuwa na mahusiano mazuri tangu miaka ya nyuma, tumefaidika na Tanzania kwani wakati wa vita vya Idd Amin Tanzania ilikuja kutusaidia. Na sisi leo tumekuja kujifunza kwa wataalamu wenzetu kuona ni vitu gani wamevifanya na kuweza kufikia hatua hii kwani kuwa na Taasisi kama JKCI siyo kitu cha muda mfupi”, alisema Dkt. Magara.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Uganda Dkt. John Omagino alisema Serikali ya nchi hiyo imeamua kujenga kituo cha matibabu ya moyo ili kupunguza idadi ya wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi. Pia kituo hicho kiwe na ubora sawa na vituo vingine vya  Afrika Mashariki ili wagonjwa wa moyo watibiwe ndani ya nchi hizo ikiwemo Uganda.

Dkt. Omagino alisema taasisi yao bado ni ndogo  na wanatakiwa kusonga mbele zaidi, Serikali yao imewapa  ardhi na wamepata fedha ambazo zitawawezesha kujenga jengo kubwa la Taasisi hiyo hivyo basi ili waweze kufanya kitu kizuri wameona watembelee vituo vingine vya moyo vilivyopo Afrika Mashariki na kujifunza vitu ambavyo vimewafanya wamefanikiwa hii ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu wa afya.

“Gharama za matibabu ya moyo ni kubwa na wengi wanashindwa kulipia  lakini wenzetu wa JKCI wanatoa huduma kwa watu wote wa kipato cha juu, cha kati na cha chini tumekuja kuona ni jinsi gani wamefanikiwa katika hili”,.

“Changamoto tunayokutana nayo ni namna ya kuwasomesha wataalamu nje ya nchi kwani wengine wanaenda kusoma muda mrefu zaidi ya miaka mitano na wengine hawarudi pindi wanapomaliza masomo yao, lakini kama tutakuwa na kozi za muda mfupi ndani ya nchi zitatusaidia watalamu hawa wakimaliza masomo yao wataendelea na kazi ndani ya nchi yao”, Dkt. Omagino .

Dkt. Omagino alisema wanaangalia  jinsi gani ya kuzuia magonjwa hayo na siyo kutibu kwani kama watu watafuata mtindo bora wa maisha wataepukana na magonjwa ya moyo hii ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi, kula vyakula bora, kupunguza unywaji wa pombe uliokithiri na kuacha matumizi ya tumbaku.

Wataalamu hao ambao ni wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Uganda wameambatana na watunga sheria na sera watakuwa katika Taasisi hiyo kwa muda wa siku mbili na watatembelea maeneo mbalimbali ya JKCI pamoja na kuzunguma za wakuu wa Idara ili waweze kubadilishana ujuzi wa kazi.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JCKI) ambaye pia ni mkuu wa idara ya magonjwa ya moyo kwa watu
wazima George Longopa akielezea huduma zinazotolewa kwa wagonjwa wa moyo
wanaoudhuria kliniki katika Taasisi hiyo kwa wageni kutoka Taasisi ya Moyo ya
Uganda walipotembelea JKCI leo kwaajili ya kuangalia huduma zinazotolewa na
Taasisi hiyo pamoja na kujifunza namna ambavyo Taasisi hiyo inaendesha
shughuli zake.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Tulizo Shemu akielezea huduma zinazotolewa katika chumba cha
upasuaji mdogo wa moyo bila kufungua kifua (Cathlab) kwa wageni kutoka Taasisi
ya Moyo ya Uganda walipotembelea JKCI kwaajili ya kuangalia huduma
zinazotolewa na Taasisi hiyo pamoja na kujifunza namna ambavyo Taasisi hiyo
inaendesha shughuli zake.
Msimamizi wa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU)
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prisca Kiyuka akielezea huduma
zinazotolewa kwa wagonjwa waliotoka kufanyiwa upasuaji wa moyo na
kufikishwa katika chumba hicho kwa wageni kutoka Taasisi ya Moyo ya Uganda
walipotembelea JKCI kwa ajili ya kuangalia huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo
pamoja na kujifunza namna ambavyo Taasisi hiyo inaendesha shughuli zake.Picha na: JKCI.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...