Na Janeth Raphael
TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imetengewa bajeti ya sh.bilioni 40.7 kwa ajili ya Kuimarisha utafiti na upatikanaji wa Mbegu bora katika mwaka wa fedha 2022/2023. 

Bajeti hiyo, itatumika kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora kwa kuongeza uzalishaji wa mbegu za awali za mazao ya nafaka, mikunde na mbegu za mafuta kutoka tani 226.5 hadi tani 1,453 ambazo zitakidhi mahitaji ya Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) na kampuni binafsi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Meneja wa Mawasiliano na Menejimenti ya Maarifa TARI Dk.Richard Kasuga alisema bajeti hiyo ni ongezeko la asilimia 250.

“Miche na pingili zipatazo milioni 50 ya mazao mbalimbali ambayo ni parachichi, mkonge, michikichi, minazi, mihogo, viazi vitamu na ndizi itazalishwa na kusambazwa kwa wakulima.Vilevile, aina 141 za mbegu za asili zitasafishwa na kuhifadhiwa katika vituo vya TARI kwa ajili ya kuzifanyia utafiti na kuziboresha"Amesema Dk.Richard Kasuga

Dk.Kasuga amesema utafiti wa mbegu za asili utaongeza wigo katika kukidhi mahitaji ya soko na kilimo cha biashara kwa kushirikiana na viwanda pamoja na wafanyabiashara.

Amebainisha kuwa TARI imepanga kuzalisha teknolojia mpya zikiwemo aina za mbegu zenye sifa zaidi ya zile zinazotumiwa kwa sasa ambapo aina hizo za mbegu zina sifa ya kutoa mavuno mengi, kustahimili ukame, ukinzani dhidi ya magonjwa na wadudu, zenye viinilishe vingi, pamoja na sifa zingine za soko kama vile sifa za mezani.

Ameongeza kuwa teknolojia zingine zitakazogunduliwa ni za uongezaji thamani katika mnyororo wa thamani wa mazao, kuboresha afya ya udongo, kugundua mbinu bora za ukuzaji mazao, zana bora za kilimo, na utunzaji wa mazao baada ya mavuno na kuimarisha uchumi jamii.

“Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 jumla ya teknolojia 35 zitazalishwa kati ya hizo 15 ni mbegu bora, tano agronomia, tano afya ya udongo na 10 teknolojia baada ya mavuno. wakulima 5,000 na Maafisa Ugani 500 watapatiwa mafunzo ya kilimo bora cha mazao mbalimbali na wasindikaji 2,000,000 watapatiwa teknolojia mpya za kuongeza thamani yak mazao,”ameeleza Dk.Richard Kasuga

KUIMARISHA MAABARA ZA UTAFITI

Dk.Kasuga amesema katika mwaka huu wa fedha TARI imepanga kujenga maabara moja ya kuzalisha miche kwa njia ya chupa katika kituo cha TARI Mlingano na kukarabati maabara moja na kununua vifaa na vitendanishi katika kituo cha TARI Mikocheni.

Amesema ujenzi na ukarabati wa maabara hizo utaongeza uzalishaji wa miche kutoka 5,131,835 hadi 33,500,000 kwa njia ya chupa.

Amebainisha kuwa TARI imepanga kuboresha maabara ya udongo katika kituo cha TARI Mlingano ili iweze kupata ithibati ya kimataifa.

“Tumepanga kununua magari 35, matrekta 10 na zana zake; na mashine tano (5) za kuchakata mbegu kwa vituo vya TARI Seliani, TARI Ilonga, TARI Uyole, TARI Hombolo na TARI Tumbi ambapo Matreka hayo yataoneza eneo la mashamba ya kuzalisha mbegu kutoka hekta 285 hadi hekta 854,”amesema Dk.Richard Kasuga

MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI
Katika kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji Dk.Kasuga alisema wizara ya Kilimo imeitengea TARI fedha za kujenga miundombinu ya umwagiliaji katika eneo la hekta 854 kwenye vituo 15 vya utafiti wa kilimo.

Amesema miundombinu hiyo itakayojengwa ni pamoja na mifereji, mabwawa katika kituo cha Ilonga na Tumbi, kuchimba visima, kununua vifaa vya kumwagilia kuchimba mitaro na kutandaza mabomba.

Aidha Dk.Richard Kasuga amesema kuwa TARI itaenda pamoja na ujenzi wa ghala tano zenye uwezo wa kuhifadhi tani 415 za mbegu kila moja yatakayojengwa katika vituo vya TARI Makutupora, TARI Seliani, TARI Hombolo, TARI Kifyulilo na TARI Dakawa.

“Ujenzi huo ukikamilika utaongeza uwezo wa kuhifadhi mbegu kutoka tani 20 za sasa hadi tani 2,075 kwa vituo hivyo. Vilevile, ghala tano za kuhifadhi mbegu zitakarabatiwa katika vituo vya TARI Uyole tatu na TARI Ilonga mbili,”amesema Dk.Richard Kasuga

Dk.Kasuga amesema shughuli zinazotekelezwa na TARI zinachangia katika utekelezaji a Ajenda 10/30 inayosisitiza kilimo ni biashara, na kwamba ifikapo mwaka 2030 kilimo kiwe kinakua kwa asilimia 10.

Amesema shughuli za utafiti na uzalishaji wa Mbegu bora ni miongoni mwa vipaumbele vya juu ambavyo TARI inahusika kuvitekeleza ili kufikia AJENDA 10/30.
Meneja wa Mawasiliano na Menejimenti ya Maarifa wa TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dk.Richard Kasuga akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 11,2022 wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za taasisi hiyo katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2022-2023 jijini Dodoma.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...