Adeladius Makwega-CHAMWINO
JJUMAPILI ya Agosti 14, 2022 niliamka kuelekea kanisani kusali, huku saa yangu ikiniambia nimeamka muda sahihi lakini hadi nafika kanisani nilibaini kuwa nimechelewa.

Nikapiga ishara ya msalaba na kuendelea na misa huku nikisali kwa umakini mkubwa,

“Mungu ameleta amani dunia kwa wanaomuamini, kumfuata Yesu duniani kunaleta mafarakano na matengano kwa baadhi ya watu wasiomwamini.”

Hayo yakiwa maneno ya awali yaliyoyakaribisha masikio yangu katika misa hiyo na hapo ikiwa saa 12.na dakika 24 ya asubuhi. Gafla nikaisikia sauti nyingine ambayo ilikuwa na mikwaruzo kidogo ikisema,

“Uwajalie wakubwa na wenye mamlaka serikalini, kulinda uhuru wa kuabudu kwa wananchi wao, ee Bwanaa (msomaji), twakuomba utusikie (waumini wakaitika).”

Hapo nilibaini kuwa yalikuwa maombi ya misa hiyo, nikiwa nimechelewa kwa dakika 24, nikiwa nimekosa kuyasikiliza masomo yote matatu ya jumapili hii pamoja na mahubiri, nikitambua ninapaswa kutubu kwa kosa hilo la kuchelewa misa hiyo. Nilisali hadi mwisho na kurudi zangu nyumbani nikinuia kutochelewa tena dominika ijao.

Nilifika nyumbani kwangu nilifanya shuguli zangu kadhaa, baadaye nikapata mgeni kijana mmoja ambaye ni rafiki yangu, nikamkaribisha, ndugu huyu ndiye aliyesababisha nipafahamu Chamwino-Ikulu kwa hiyo kumkaribisha katika Dawati langu la Ujamaa hakukuwa na budi.

“Mjomba na mimi siku hizi nimeanza kusali, maana tangu nitoke Tanga nilikuwa naishi maisha mengine kabisa, lakini leo nimeenda kusali kanisani kwetu.”

Msomaji wangu mwanakwetu ninaambiwa hilo, nikamjibu hilo ni jambo zuri,

Lakini mjomba nimekwazika mno, nikamuuliza kwa nini? Akanijibu mimi mfukoni kwangu nilikuwa na sarafu ambazo zilikuwa ndiyo fedha zangu za mwisho, wakati wa sadaka niliamka na kwenda kutoa pesa hiyo. Kanisani kwetu kumbe sadaka huwa inahesabiwa kabla ya ibada haijaisha kwa hiyo zilipohesabiwa kumbe ikabainika kuwa leo kanisani kuna mgeni mtoa sarafu, kwa kuwa utaratibu wa kanisa hili wamekubaliana hakuna kutoa sarafu.

Kiongozi wa dini mara baada ya sadaka kuhesabiwa alijulishwa leo zimetolewa sarafu, kwa hiyo aliposimama alisema jamani leo kuna shilingi 600 ya sarafu lakini tulikubaliana kuwa tusitoe sarafu tutoe noti. Nadhani leo kuna mgeni, kweli kwa juma zima Mungu amekujalia kupata sarafu? Mchungaji aliuliza.

Kanisa lilikuwa kiimya, mchungaji aliendelea kulizungumzia jambo hilo, jamani Mungu amekupa uhai, haujaugua kwa juma zima, kweli sarafu kanisa letu itasaidi nini?

“Jamani ninawaombeni tumtoleee Mungu sadaka njema, huku tukiheshimu yale mema ambayo Mungu ametutendea.”

Ndugu huyu alikuwa kimya na hata walipotambulishwa wageni aliamua kukaa kimya, maana yake kama angesimama basi ingejulikana kuwa yeye ndiye aliyetoa sarafu, akaniambia aliomba Mungu ibada hiyo imalizike haraka.

“Shilingi mia sita hizo ni mia mbili mbili na mia moja mbili.”

Hizo zikiwa ndizo fedha alizotoa yeye, ndugu yangu huyu akisema jambo hilo limemuumiza mno, akaniambia, hivi amekuja kwangu angalau apoteze mawazo, maana badala ya kupata amani kanisa amepata huzuni na ameamua hatokwenda tena kusali.

Mwanakwetu nilimsikiliza vizuri sana ndugu yangu huyu ambaye kwa hakika yeye ndiye aliyenileta eneo la Chamwino-Ikulu, awali nilikuwa silifahamu kabisa eneo hili. Ndugu yangu huyu anasali dhehebu tafauti na mimi, huku dhehebu lake kwa mkoa wa Dodoma ni kanisa lenye Wakristo wengi.

Nikamuuliza mjomba kwani wiki hii umefanya kazi yoyote? Akanijibu kuwa wiki hii hakufanya kazi yoyote bali alikuwa na pesa ya kutosha katika akiba yake ambayo alitumia kuwapeleka watoto wake jandoni kwa kuwa sasa shule zimefungwa ili vidonda vipone wakati wa likizo na pesa yote imetumika huko, kwa hiyo ndiyo amerudi hana pesa na akadamkia kusali.

Nikamwambia mjomba, kwa kuwa hiyo sadaka kama unavyosema ndiyo uliyokuwa nayo, kama unayosema ni ya ukweli wa Mungu, wewe endelea kusali tu Mungu mwenyewe anatambua kuwa wewe leo hauna kitu, lakini hauna leo siyo ya kesho, endelea kusali.

Nikamwambia mjomba yule mchungaji usimchukie, nia yake kile kinachopatikana kitumike kusaidia kulijenga kanisa, siyo vinginevyo, wewe unawajibu wa kulijenga kanisa lako siyo mtu mwingine.

Nikamsimulia ndugu yangu huyu kuwa leo mimi nimechelewa lakini nilipofika tu nilimsikia Padri Mapalala akisema maneno haya,

“Mungu ameleta amani dunia kwa wanaomuamini, kumfuata Yesu duniani kunaleta ufarakano na matengano kwa baadhi ya watu wasiomwamini.”

Nikamwambia na wewe japokuwa siyo mkatoliki naomba tilia maanani maneno hayo hili usilete mafarakano na matengano ili kuepuka kuwa wale wasiomwamini.

Tulicheka na kufurahi na ndugu huyu akisema jumapili ijayo atakwenda kanisani kwao kusali.
Tulipiga soga zingine na baadaye ndugu yangu huyu aliniaga na kwenda zake.
makwadeladius@gmail.com
0717649257

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...