Na Rosena Suka, Lushoto
JAJI wa Mahakama ya Rufaa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Dkt. Paul F. Kihwelo,  leo tarehe 9 Agosti, 2022 amefungua mafunzo ya siku tano kwa Makatibu Mahsusi wapatao 56 wa Mahakama ya Tanzania yanayohusu Namna Bora ya Uendeshaji wa Ofisi. Mafunzo hayo yanayofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 09 Agosti ,2022 mpaka 13 Agosti, 2022 katika ukumbi wa Mafunzo uliopo Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Akifungua mafunzo hayo Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amewataka Makatibu Muhtasi kutoa huduma bora zinazoendana na uwekezaji katika majengo ya Mahakama nchini. Aliendelea kwa kusema kuwa, Mahakama ya Tanzania iko katika maboresho ambayo yanagusa maeneo mbalimbali ikiwemo miundombinu ya majengo na raslimali watu hivyo mafunzo haya yana lengo la kuwaandaa watumishi hao ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea.

“Hivyo lengo la mafunzo yanayotolewa ni kujaribu kuwajengea uwezo na kubadilisha fikra za watumishi wa Mahakama ili huduma wanazozitoa mahakamani ziendane na ubora wa majengo ambayo yanaendelea kuboreshwa,” amesema.

Mhe. Dkt. Kihwelo aliwasihi watumishi hao kuwa waadilifu na wachapakazi ili kuipa sifa nzuri Mahakama ya Tanzania kwa kuepuka vitendo vinavyoweza kuichafua Mahakama kama matumizi ya lugha mbaya. Pia aliwaomba watumishi hao watakaporudi kwenye vituo vyao vya kazi ni wajibu kushirikiana na kuonyesha waliochojifunza.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick amewaambia washiriki hao kuwa Mahakama imejipanga kuwajengea uwezo watumishi wake katika kada mbalimbali ili kuendana na maboresho yanayoendelea.

Bi. Beatrice Patrick amesema kundi hilo la washiriki wa mafunzo linajumuisha Makatibu Muhtasi 56, ambapo 50 wametoka katika Mahakama mbalimbali za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi, washiriki sita wakiwa ni waajiriwa wapya.

Amesema kuwa watumishi hao wanapewa mafunzo hayo kwa lengo la kuwakumbusha majukumu yao ya kazi za Ukatibu Muhtasi, utunzaji wa kumbukumbu, usimamizi wa ofisi na mawasiliano ya kiofisi, uzalendo na protokali, mipango ya Mahakama na uboreshaji, huduma kwa mteja, masuala ya saikolojia na ushauri, mwelekeo wa Mahakama kwa sasa katika mapinduzi ya viwanda kuelekea Mahakama Mtandao na matumizi ya TEHAMA.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wote wa mafunzo.
Sehemu ya Makatibu Muhtasi wanaoshiriki katika mafunzo ikifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Mkuu wa Chuo.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akisisitiza jambo alipokuwa anafungua mafunzo ya siku tano kwa Makatibu Muhtasi 56 yaliyoanza kufanyika leo tarehe 9 Agosti, 2022.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...