Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa akipokea ripoti hiyo kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati Bw. Victor Tesha katika hafla iliyofanyika usiku wa kuamkia leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.

1.0 Utangulizi

Hakimiliki na Hakishiriki ni maeneo muhimu zaidi popote ubunifu unapotajwa. Hakimiliki na Hakishiriki ni muhimu kwa kuwa ni msingi wa kuhakikisha kwamba wabunifu (wa kazi sanaa na maandishi) wananufaika na matumizi ya kazi zao. Sheria imeweka wazi kwamba ni wabunifu pekee ndio wenye uwezo wa kuruhusu matumizi ya kazi zao katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo, kwa kuwa kuna baadhi ya haki ambazo wabunifu hawawezi kuzisimamia wenyewe, serikali nyingi duniani zimekuwa zikianzisha taasisi mbalimbali kusimamia haki hizo. Kwa upande wa Tanzania, kwa muda mrefu wajibu huu umekuwa ukifanywa na Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA). Mnamo mwezi Julai, 2022 Serikali ilifanya marekebisho kwenye Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ambapo mbali na mambo mengine imeifanya COSOTA kuwa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania na kuruhusu uanzishwaji wa makampuni au taasisi binafsi (CMOs) zitakazokusanya na kugawa mirabaha kwa niaba ya wabunifu. Kwa mujibu wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki, CMOs zinatakiwa kuwa taasisi zilizoidhinishwa kisheria chini ya Ofisi ya Hakimiliki Tanzania, kufanya shughuli za usimamizi wa Hakimiliki bila kuwa katika misingi ya kutengeneza faida. Usimamizi wa taasisi hizi unatazamiwa kuwanufaisha moja kwa moja na kwa njia rahisi waandishi, wabunifu na wamiliki wengine halali wa kazi za Sanaa.

Kwa kuzingatia usuli huo na kwa kuzingatia umuhimu wa usimamizi bora wa Hakimiliki na Hakishiriki nchini Tanzania, mnamo tarehe 01.07.2022 Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa aliteua kamati maalumu ya wajumbe 11 kwa lengo la kuratibu namna bora ya usimamizi wa hakimiliki nchini Tanzania. Wajumbe hao ni hawa wafuatao:

1. Bw. Victor Michael Tesha Mwenyekiti
2. Dkt.SaudinMwakaje
MakamuMwenyekiti 3. Bw.DimeshSMawjKatibu
4. Mhe. Hamis Mwinjuma
Mjumbe

  1. Dkt.OmaryMohamedMjumbe

  2. Bw. Paul Mattysse Mjumbe

  3. Bi. Safina Kimbokota Mjumbe

  4. Bw.TorrianoSalambaMjumbe

  5. Bw. Gabriel Kitua Mjumbe

10. Bw. Twiza Mbarouk Mjumbe 

11.Dkt. Asha S Mshana Mjumbe

Wajumbe wa kamati hii wana taaluma na uzoefu katika maeneo mbalimbali ikiwamo wataalamu wa masuala ya fedha, wanasheria na wabunifu wa kada ya Sanaa na Maandishi.

2.0 Hadidu za rejea

Kamati ilipewa hadidu za rejea zifuatazo:

  1. Kupendekeza mifumo bora zaidi ya kukusanya na kugawa mirabaha

    inayoshabihiana na mifumo mingine duniani.

  2. Kupendekeza njia bora zaidi ya kupambana na uharamia wa kazi za sanaa

    nchini.

  3. Kupendekeza mfumo bora zaidi wa uendeshaji wa Taasisi ya Hakimiliki

    T anzania.

  4. Kuratibu kikao cha wadau wa Hakimiliki cha kujadili mapendekezo ya kamati

    na

  5. Kuwasilisha taarifa ya kamati kwa Mhe. Waziri wa Utamaduni, Sanaa na

    Michezo.

3.0 Methodolojia

Ili kufanya kazi kwa mujibu wa hadidu rejea, methodolojia iliyotumika katika kupata taarifa ni upitiaji wa nyaraka mbalimbali zinazohusu hakimiliki, mahojiano, hojaji na mikutano ya ana kwa ana ambayo ilishirikisha wadau mbalimbali muhimu katika kupata taarifa kwa lengo la kukamilisha jukumu la Kamati. Mikutano hii ilifanyika katika kanda sita kama ifuatavyo:

Mosi, kanda ya Kaskazini- Mkutano ulifanyika Mkoani Arusha katika Hoteli ya Golden Rose, na kuhudhuriwa na wabunifu pamoja na wadau 216.

Mkutano huu pia ulihudhuriwa na Mhe. Pauline Gekul Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Pili, kanda ya Kati Mkutano ulifanyika katika ukumbi wa Dear Mama, mjini Dodoma na kuhudhuriwa na wabunifu pamoja na wadau 126.
Tatu, kanda ya Ziwa
Mkutano ulifanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya jijini Mwanza na kuhudhuriwa na wabunifu 87.

Nne, kanda ya Nyanda za Juu Kusini- Mkutano uliafanyika katika ukumbi wa BEACO jijini Mbeya na kuhudhuriwa na wabunifu 138

Tano, Kanda ya kusini- mkutano huu ulifanyika mkoa wa Mtwara katika ukumbi wa Halmashauri na ulihudhuriwa na wadau 181.

Sita, kanda ya Mashariki, ambapo mkutano wa wabunifu na wadau wa sekta ya ubunifu 171 ulifanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na wajumbe wote wa kamati wakiongozwa na Mwenyekiti. Ripoti za mikutano ya ukusanyaji maoni zimeambatishwa kama viambatisho Na. 4.2.

Wadau wa jinsi zote, wakiwamo wenye mahitaji maalumu walishiriki. Kwa wastani 22% ya wasanii na wadau waliohudhuria walikuwa wa jinsi ya kike na 78% walikuwa wa jinsi ya kiume. Tasnia ya Sanaa ya Maonesho na Sanaa ya Ufundi zilikuwa na uwiano mzuri zaidi wa uwakilishi kati ya jinsi ya kike na ile ya kiume. Katika watoa maoni, uwiano wa wasanii wa kike ulikuwa mdogo zaidi kwa wasanii wa muziki.

Aidha, kamati hii iliangalia uzoefu wa nchi nyingine kwenye usimamizi wa Hakimiliki na kuchambua takwimu za wabunifu na wadau. Nchi zilizoangaliwa kwa ajili ya uzoefu ni pamoja na Nigeria, Algeria, Afrika Kusini na Kenya.

4.0 Mapitio ya Mabadiliko ya Mfumo wa Sheria

Katika kujenga usuli mzuri wa mapendekezo ya Kamati kwa mujibu wa hadidu za rejea katika ripoti hii, na kwa lengo la kujenga welewa wa pamoja, kumetolewa usuli wa mabadiliko ya mfumo wa sheria wa hakimiliki nchini Tanzania. Mabadiliko yaliyojadiliwa katika ripoti hii ni:

Mosi, mabadiliko ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Namba 7 ya mwaka 1999 ambayo yalifanywa kwa lengo la kuziba baadhi ya mianya ya kiusimamizi iliyoonekana kuwapo kwa wakati huo. Sheria hii ilibadilisha maeneo manne ambayo ni kifungu cha 4, Kifungu cha 9, kifungu cha 15 na kifungu cha 42. Vifungu hivi vilifanyiwa uboreshaji ili kuendana na hali ya sasa kuhusiana na masuala ya Hakimiliki na Hakishiriki.

Pili ni mabadiliko ya sheria ya Machi, 2022 kufuatia mabadiliko ya sheria Na.1 ya mwaka 2022, ambapo kifungu cha 3 kilibadilishwa kuongezewa tafsiri na kifungu cha 12 kilibadilishwa na kuongezewa vifungu vya 12A na 12B ili kuwezesha utekelezaji wa mkataba huo. Baadhi ya marekebisho hayo ni:

  1. a)  Kuweka utaratibu unaoruhusu kunakili machapisho na kuyageuza katika muundo (format) ya maandishi kwa ajili ya watu wasiiona au wenye matatizo ya kusoma maandishi ya kawaida bila kupata idhini ya mwenye chapisho.

  2. b)  Kuweka utaratibu wa kuruhusu taasisi husika kuweza kurudufu machapisho na kuwayaweka katika mfumo wa kuweza kusomwa na watu wenye matatizo ya kuona na taasisi hizo kuruhusiwa kusambaza kwa wahusika kwa kutoza gharama za uchapishaji na si kwa ajili ya kupata faida.

Tatu, ni mabadiliko yaliyofanywa na Sheria ya Fedha ya Mwezi Julai, 2022 ambayo mbali na mambo mengine yamelenga katika kuanzisha mfumo mpya wa usimamizi wa hakimiliki hapa Tanzania kwa kuruhusu uanzishwaji wa makampuni binafsi ya ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha nchini Tanzania. Pia mabadiliko haya yameanzisha tozo mpya kwa vibebeo vya kazi za ubunifu vinavyotumika katika kudurufu, kusambaza, kuhifadhia na kuzalisha kazi hizo. Aidha, mabadiliko yamefanyika katika kifungu cha 4 kwa kuongeza tafsiri pamoja na kufuta neno chama na kuweka neno ofisi. Pia vifungu vya 46, 47 na 48 vimerekebishwa ambapo baadhi ya majukumu yaliyokuwa yakifanywa na COSOTA yameondolewa ili kuruhusu uanzishwaji wa kampuni hizo na uazishwaji wa Ofisi ya Hakimiliki T anzania.

5. Matokeo ya Utafiti

Baada ya majadiliano na wadau na kwa kuzingatia hojaji zilizotolewa mapendekezo yafuatayo yalizingatiwa:

5.1 Elimu kwa umma

Wadau wote waliohudhuria katika mikutano ya kukusanya maoni walijibu maswali kuhusu elimu ya hakimiliki, usimamizi wa maslahi ya wasanii na uharamia wa kazi za sanaa. Wadau wengi walionesha uhitaji wa elimu zaidi kwa umma kuhusu hakimiliki na masuala kadhaa yanayoambatana na hakimiliki. Aidha, washiriki wengi walionesha kuelewa zaidi kuhusu Taasisi ya Hakimiliki nchini kuliko mambo muhimu kama umiliki wa hakimiliki za sanaa; anayestahili malipo kutokana na kazi za sanaa na kuhusu uharamia wa kazi za sanaa.

Vilevile, ufahamu wa washiriki kuhusu uharamia wa kazi za wasanii ulikuwa mdogo zaidi ukifuatiwa na uelewa kuhusu umiliki wa hakimiliki na stahiki za mapato yatokanayo na hakimiliki

5.2 Umuhimu wa kuwa na Chombo kimpya cha kusimamia masuala ya hakimiliki nchini

Maeneo mengine yaliyotolewa maoni ni iwapo kuna mahitaji ya chombo kipya cha kusimamia mashauri ya hakimiliki nchini.

Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba tasnia ya Sanaa ya Ufundi ikifuatiwa na tasnia ya Muziki na Filamu zilipendekeza kwa asilimia zaidi ya 50% kuwe na chombo kipya wakati tasnia hizo za Sanaa uelewa wao kuhusu hakimiliki ya kazi za sanaa zao ulikuwa chini ya asilimia 50%. Wakati huohuo tasnia hizo tatu uelewa wao kuhusu Ofisi ya Hakimiliki ulikuwa 63%, 77% na 72% kwa Sanaa ya Ufundi, Sanaa ya Muziki na Sanaa ya filamu katika mpangilio huo.

Matokeo ya Utafiti huu yanaonesha umuhimu wa Kamati kuzingatia mambo mawili: Mosi, kupendekeza mkakati na mfumo utakaowezesha uwekezaji na jitihada za dhati kuhusu elimu kwa wasanii wa tasnia zote na umma kuhusu mambo ya hakimiliki na uharamia wa kazi za sanaa.

Pili, kupendekeza kanuni na taratibu ambazo zimeakisi kanuni bora zaidi kutoka nchi zenye mazingira sawa na Tanzania.

6.0 Mapendekezo ya Kamati

Kutokana na mabadilko ya Sheria ya mwezi Julai 2022 ambayo yameanzisha utaratbu mpya wa usimamizi wa hakimiliki ambapo kazi za usimamizi wa hakimiliki na ukusanyaji wa mirabaha zitafanywa na CMOs, na pia kwa kuzingatia maoni na mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na wadau, Kamati inapendekeza masuala ya kisera na kisheria katika maeneo manne: (1) mfumo bora wa kukusanya na kugawa mirabaha, (2) njia bora ya kupambana na uharamia, (3) mfumo bora wa uendeshaji wa taasisi ya hakimiliki, na (4) mapendekezo mengine ya jumla.

6.1 Mfumo Bora wa Kukusanya na Kugawa Mirabaha

Katika sehemu hii kuna mambo mawili ya msingi ambayo ni kanuni za usimamizi wa ukusanyaji wa mirabaha na ushirikiano na Taasisi mbalimbali za serikali

6.1.1 Kanuni za Usimamizi wa Ukusanyaji Mirabaha

Ili kutekeleza mfumo mpya wa usimamizi wa hakimiliki hapa Tanzania, Kamati inapendelkeza kanuni zitungwe kwa kuzingatia mambo yafuatayo:

  1. Kabla ya kufanyiwa usajili au kupewa leseni ya kukusanya mirahaba, CMOs zifanyiwe tathmini ya uwezo wao wa kiutawala, wawasilishe mpango wa biashara wakibainisha mbinu watakazotumia kutambua wasanii wa eneo hilo na namna ukusanyaji wa mirabaha utakavyofanyika, ziwe na mfumo unaokubalika wa kihasibu, waajiri watalaamu wenye sifa, katika bodi ya wakurugenzi kuwa na wawakilishi wa tasnia husika ya sanaa (wamiliki).

  2. Kwa kuanzia, makampuni yatakayopewa dhamana ya kukusanya mirabaha yapewe aina moja ya sanaa kwa kazi zote. Utaratibu huu utazifanya kampuni hizi zitakazopewa leseni ya kukusanya mirabaha kufanya kazi kwa ufanisi kwa kulenga aina moja tu ya kazi.

  3. Kila mwaka utendaji wa kampuni hizi ufanyiwe tathmini ili kujua kama zina ufanisi au la. Vigezo viwekwe vitakavyoongoza Ofisi ya Hakimiliki kuamua kuhuisha au kutohuisha leseni ya kampuni. Kiwekwe kiwango cha alama za chini cha utendaji katika ukusanyaji mapato.

  4. Kila mwaka wa fedha unapoanza, kampuni hizi ziwasilishe makadirio ya makusanyo kwa mwaka ambayo yatafanyiwa tathimini na kuidhinishwa na Ofisi ya Hakimiliki. Endapo kampuni itakusanya chini ya asilimia 50 ya makadirio bila kutoa sababu za msingi, Kanuni zitoe mamlaka kwa Ofisi ya Hakimili kukataa maombi ya kuhuisha leseni ya kukusanya mirabaha kwa kampuni husika.

  1. CMOs iweke mfumo wa kielektroniki ambao utaruhusu taarifa za muda mfupi

    za makusanyo ya mirahaba kuonwa na Ofisi ya Hakimiliki na wamiliki wa haki.

  2. Kwa kuwa kampuni za ukusanyaji zitakuwa zikikusanya na kubaki na fedha za wamiliki, ni vyema kanuni zikaweka ukomo wa matumizi ya uendeshaji ili

    kulinda maslahi ya wamiliki.

  3. Katika maombi ya leseni (mpya au kuhuisha), kanuni ziweke sharti kwa

    kampuni za ukusanyaji wa mirabaha kuwasilisha dhamana ya fedha kutoka benki kwa kiwango kisichopungua asilimia 50 ya matarajio ya makusanyo katika mwaka unaofuata.

  4. Katika kipindi cha mpito kabla ya Kanuni za utekelezaji wa mabadiliko ya Sheria kutungwa, Ofisi ya Hakilimili Tanzania iendekee kutambulika kama ina majukumu ya kukusanya mirabaha na kuendelea kukusanya mirabaha mpaka hapo makampuni yatakayopewa leseni ya kukusanya yatakapoanza kazi kikamili na kujisajili katika mashirika ya kimataifa ya ukusanyaji wa mirabaha.

6.1.2 Ushirikiano wa Taasisi Mbalimbali za Serikali

Masuala yanayohusu usimamizi wa hakimiliki ni mtambuka na yanahusisha taasisi nyingi za serikali na nyakati fulani zenye maslahi pingani. Hivyo Kamati inapendekeza yafuatayo:

  1. Kuundwa kisheria kwa Kamati ya Kiuratibu ya Wizarani kwa ajili ya usimamizi wa masuala ya hakimiliki ikihusisha Ofisi ya Hakimiliki Tanzania, BASATA, Bodi ya Filamu, TRA,TCRA, BRELA,TCU, na TAMISEMI. Taasisi hizi zinasimamia wazalishaji na watumiaji wa kazi za sanaa. Ni vyema kukawa na wajibu wa kisheria kwa taasisi hizi kushirikiana ili kuwa na mkakati wa pamoja katika kushughulikia uharamia wa kazi za wasanii na ukusanywaji wa mirabaha.

  2. Katika utoaji wa leseni za biashara kwa taasisi zinazotumia kazi za sanaa, kwa mfano redio, televisheni, baa na shule kuwepo na matakwa ya mwombaji kuwasilisha cheti cha utambuzi kutoka Ofisi ya Hakimiliki ya Tanzania. Hii itasaidia kuwabana wahusika kama hawatoi ushirikiano katika kuwasilisha malipo ya mirabaha kutokana na matumizi ya kazi za sanaa.


6.1.3 Njia Bora ya Kupambana na Uharamia wa kazi za sanaa

Katika sehemu hii, Kamati inapendekeza mambo mawili ya msingi ambapo kila moja limefafanuliwa katika vipengele vidogovidogo kadhaa: Mambo hayo ni kuongeza adhabu kwa makosa ya uharamia wa kazi za hakimiliki pamoja na kusajili mikataba ya wasanii. Ufafanuzi wa mapendekezo haya ni kama unavyoonekana hapa chini:

a)  Kuongeza Adhabu kwa Makosa ya Uharamia wa kazi za sanaa

Mojawapo ya njia ya kuboresha usimamizi wa hakimiliki ni kufanyia marekebisho kwa adhabu zinazotolewa. Kwa mfumo wa sasa wa adhabu, ambao unatoa adhabu ya faini au kifungo cha jela bila kuzingatia uzito wa kosa. Hapa Kamati inatoa mapendekezo yafuatayo:

b) Adhabu zitolewe kwa kuzingatia uzito wa kosa, Mahakama au Ofisi ya Hakimiliki iwekewe kiwango cha chini cha faini au kifungo, lakini iachiwe uhuru wa kuamua kiwango cha juu cha adhabu kwa kuzingatia muktadha na uzito wa kosa lililofanyika; 

Adhabu ihusishe kufutiwa leseni ya biashara endapo itathibitika kuwa mkosaji alifanya kosa hilo kwa kukusudia;

Adhabu ihusishe kutaifishwa na kuharibiwa kwa vifaa vinavyotumika katika kufanya uharamiaAdhabu ziwaguse waliofanya makosa na waliowasaidia kutekeleza uharamia. Kutanua wigo wa wahusika kutasaidia katika kuimarisha usimamizi na kuongeza uwajibikaji katika usimamizi wa hakimiliki nchini.

Kusajili Mikataba ya Wasanii

Mojawapo ya malalamiko makubwa na yanayojirudia ni kuwa wasanii wengi wanahisi wanaonewa kimaslahi katika kazi wanazofanya chini wa mwavuli wa makampuni au wasanii wakubwa. Ili kushughulikia suala hilo, tunapendekeza:

i. Katika kanuni zitakazotungwa, kiongezwe kipengele ambacho kitatoa motisha kwa makampuni na wasanii wakubwa kusajili mikataba yao katika Ofisi ya Hakimiliki. Vivutio hivi vinaweza kujumuisha kuruhusu nafuu za kikodi kwa makampuni yatakayosajili mikataba ya wasanii. Kanuni ziweke wajibu kuwa mikataba ya wasanii wanaochipukia isajiliwe katika Ofisi ya Hakimiliki.


ii. Pia, sheria itoe mamlaka kwa Ofisi ya Hakimiliki kupitia vifungu vya mikataba inayosajiliwa na endapo itajiridhisha kuwa kuna vifungu kandamizi Ofisi iwe na mamlaka ya kushauri mamlaka husika kufanya marekebisho.

6.1.4 Mapendekezo Kuhusu Mfumo wa Kisheria

Katika sehemu hii Kamati inatoa mapendekezo katika maeneo saba kama ifuatavyo:

a) Marekebisho ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya 1999

Kwa kuzingatia maendeleo ya kiteknolojia ambayo yamebadili mfumo mzima wa jinsi kazi za sanaa zinarudufiwa na maharamia, tunapendekeza:

  1. Orodha ya vifaa vitakavyotozwa kodi (blanket levy) katika mabadiliko ya sheria ya hakimiliki ya mwezi Julai 2022 iboreshwe kwa kuongezea vifaa ambavyo kwa teknolojia ya sasa vinatumika katika kuridifu na kuhifadhi kazi za sanaa. Vifaa vilivyo katika orodha ya sasa ni vya zamani na havitumiki sana.

  2. Wigo wa mfumo au njia za utambuzi wa matukio ya uharamia na ulinzi wa kazi za sanaa uboreshwe kwa kuzingatia na kutumia mifumo ya kiteknolojia iliyopo sasa. Hii itaendana na hatua ambazo mashirika ya kimataifa kama vile WIPO yamechukua kwa kupitisha na kutumia Mkataba maalumu wa kimataifa wa hakimiliki ambao umejikita zaidi katika masuala ya kiteknolojia (WIPO Copyight Treaty of 1996)

    b) Kuanzisha Mfumo wa Mahakama Tembezi

Ili kushughulikia tatizo linaloongezeka la uharamia wa kazi za wasanii, ni vyema mfumo wa utoaji haki uboreshwe ili uweze kushughulikia makosa yanayojitokeza kulingana na uhalisia na mazingira ya utendaji wa makosa ya kiuharamia. Katika mazingira ya Tanzania ambapo makosa ya kiuharamia hufanyika kwa kiwango kikubwa na kidogo ikihusisha sehemu ambazo ni rahisi kuharibu ushahidi endapo ukamataji utachelewa, inapendekezwa kuanzishwa kwa mahakama zinazotembea ambazo zitakuwa na mamlaka ya kutoa maamuzi papohapo endapo ushahidi utakuwa umejitosheleza.

c) Kuongeza Mamlaka ya Kiusimamizi kwa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania

Ili kuboresha usimamizi wa masuala ya hakimiliki hapa Tanzania, inashauriwa kuwa Ofisi ya Hakimiliki ipewe mamlaka ya kisheria ili kushughulikia utatuzi wa migogoro 9

na makosa ya uharamia na kutoa adhabu kwa wahusika watakopatikana na hatia. Mamlaka hiyo inapaswa kutumia nguvu ya kisheria kuagiza vifaa vinanvotumika kufanya kazi za uharamia kukamatwa mara tu vinapogundulika mahali vilipo, watuhumiwa wa uharamia kukamatwa, kutoa amri ya kuviharibu vifaa vitakavyothibitika ni zao la uharamia au vinatumika kufanya uharamia. Kwa kuchukua hatua hii, itawezesha Ofisi ya Usimamizi wa Hakimiliki kuwa na nguvu ya kisheria ya kutoa maamuzi ya haraka na yenye nguvu za kisheria. Pia, hatua hii itapunguza kwa kiwango kikubwa ucheleweshaji wa kesi za uharamia wa kazi za sanaa na kupunguza gharama za kuendesha kesi kwa walalamikaji.

d) Ofisi ya Hakimiliki Iongeze Wigo wa kazi Inazosimamia

Kwa ujumla, katika utendaji wake, COSOTA imekuwa ikijikita zaidi katika kazi za Sanaa ya muziki. Wakati umefika sasa wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania kujipambanua na kuweka mkakati wa kutumia rasilimali na nguvu ileile katika kusimamia kazi zote za sanaa. Inapendekezwaza kuwa Ofisi ya Hakimiliki kuzigawa aina mbalimbali za sanaa na kuanzisha vitengo vya ndani vitakavyosimamia maeneo hayo ya sanaa. Maeneo haya yanaweza kujumuisha tasnia nne za sanaa ambazo ni (1) Sanaa za ufundi (2) Sanaa za maonesho (3) sanaa za muziki na (4) Sanaa za filamu. Ili kutilia mkazo, tunapendekeza maeneo hayo yabainishwe na kutengewa rasilimali kwa ajili ya utekelezaji katika mpango mkakati wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania. Hatua hii itaongeza tija katika tansinia ya sanaa na kuongeza wigo wa mapato kwa serikali na wasanii.

e) Kutungwa Sera ya Taifa ya Miliki Dhihini (National Intellectual Property Policy)

Ili kuyashughulikia masuala ya hakimiliki kwa upana wake, maeneo mengine ya miliki ya ubunifu na taasisi nyingine zinazoshughulikia miliki ya ubunifu kama vile BRELA, FCC, BASATA, COSTECH zinahusika. Hivyo, tunapendekeza kuwa mchakato unaondelea wa kutunga na kupitisha sera ya kitaifa ya miliki ya ubunifu uharakishwe ili Tanzania iwe na sera inayotoa dira ya jumla ya jinsi masuala haya yanavyopaswa kushughulikiwa.


f) Elimu ya Hakimiliki

Kutokana na umuhimu wa tasnia yab sanaa na masuala yote ya ubunifu katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kiutamaduni na sayansi hapa Tanzania, tunapendekeza mitaaala ya elimu kuanzia ngazi ya elimu ya msingi ijumuishe moduli zinazofundisha masuala ya miliki za ubunifu na umuhimu wa kuheshimu na kuzilinda haki za wabunifu kupitia sheria zilizopo. Mbali na mitaala ya shuleni, Wizara ianzishe mpango kabambe wa kuandaa vipindi vya kuelimisha jamii kupitia television, radio, mitandao ya kijamii na njia nyinginezo zitakazosaidia kufikisha elimu kwa walengwa na wadau mbalimbali.

g) Kuridhia Mikataba ya Kimataifa Inayohusu Hakimiliki

Ili kuboresha usimamizi wa hakimiliki ni muhimu kwa Tanzania kuanzisha mchakato wa kuridhia mikataba ya kimataifa inayohusu hakimiliki na kuimarisha zaidi ushirikiano na mashirika ya kimataifa na kikanda. Miongoni mwa mashirika hayo ni:

  1. Shirika la Kimataifa la Miliki ya Ubunifu (World Intellectual Property Organization (WIPO))

  2. Shirika la Biashara la Kimataifa (World Trade Organization (WTO)

  3. Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (United Nation

    Educational Scientific and Cultural Organization (UNESCO)

  4. Shirika la Kikanda la Miliki ya Ubunifu Africa (ARIPO)

6.1.5 Muundo wa kiuongozi unaopendekezwa kwa ajili ya Ofisi ya Hakimiliki Tanzania

Kwa kuwa ofisi hii imepunguziwa kazi ya kuandikisha wanachama, kukusanya na kugawa mirahaba, idadi wa wafanyakazi inapaswa kuanza kwa kiwango kinacholingana na uhalisia wa shughuli lengwa na pia ili kuwezesha wafanyakazi watakaokuwapo a) kuwa na kazi ya kutosha na b) kulipwa stahiki zao ipasavyo na kuwezesha mchango wa rasilimali fedha kwa CMOs mpya. Inapendekezwa kuhakikisha wanaajiriwa wafanyakazi wenye weledi, mahiri na wanaostahili.

6.1.6 Mchanganuo wa kina wa idadi ya wafanyakazi kwa kila idara

Bodi ya Wakurugenzi inapaswa kuandaa mpango mkakati, kwa kuanzia wa miaka mitatu kisha wa miaka mitano mitano ili kuongoza shughuli za Ofisi ya Hakimiliki.

11

Mpango mkakati unaweza kuzingatia mapendekezo ya idadi ya wafanyakazi kuanzia ngazi ya maofisa kwenda juu kama ifuatavyo:

a) Idara ya Usimamizi wa Sheria na Kuzuia Uharamia (watu 5 - 8)

Idara hii ni moja ya idara muhimili kwa kuwa inahusu majukumu ya kisheria ya Ofisi ya Hakimiliki Tanzania. Meneja ataripoti kwa Msajili wa Hakimiliki na atawajibika pia kuwasilisha katika bodi ripoti za hali ya utekelezwaji wa sheria za hakimiliki nchini na mapambano dhidi ya uharamia. Idara hii pamoja na idara ya Utafiti, Elimu na TEHAMA vitachukua sehemu kubwa ya bajeti ya matumizi ya uendeshaji wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania.

Meneja atasaidiwa na maofisa wawili wanasheria na maofisa wawili watakaochukuliwa kutoka Jeshi la Polisi. Maofisa waliotoka jeshi la polisi kama itawezekana nao wawe wanasheria ingawa si lazima. Maoni yametolewa kuhusu umuhimu wa kuwa na wafanyakazi watakaoazimwa kutoka Jeshi la Polisi ili kuongeza ushirikiano na uharaka wa uchukuaji hatua za kuzuia uharamia na kuhakikisha sheria inafanya kazi nchini kote. Ili kutenda kwa ufanisi, idara hii itahitaji magari mawili ya kuzunguka nchi nzima.

b) Idara ya Utafiti Elimu na TEHAMA (watu 5)

Hii ni moja ya idara mhimili za Ofisi ya Hakimiliki Tanzania. Idara hii itajikita katika elimu kwa wasanii, wadau na umma kwa ujumla kuhusu hakimiliki, kazi za usanii/ ubunifu na haki za wabunifu. Ili kupangilia elimu stahiki na kwa maeneo stahiki, idara hii pia inapaswa kutekeleza jukumu la utafiti. Kwa kuwa njia za kuwafikia wadau kwa njia ya kielektroniki zinazidi kukua, pia idara hii itakuwa ndiyo ina ofisa TEHAMA wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania. Vigezo vya ajira katika Ofisi ya Hakimiliki Tanzania yapaswa kuzingatia uelewa wa msingi wa TEHAMA unazingatiwa kwa kila mwajiriwa, katika kila idara.

c) Idara ya Usimamizi wa CMOs (watu 4 - 5)

Hii nayo ni idara mhimili. Idara hii ndiyo itatoa leseni kwa CMOs, kupokea ripoti za robo, nusu mwaka na za mwaka za CMOs na kukagua CMOs. CMOs zitakaguliwa ili kuhakikisha kwamba zinaendesha shughuli zake kwa kuzingatia kanuni zilizoidhinishwa na Ofisi ya Hakimiliki Tanzania. Ukaguzi pia utafanywa kuhakikisha 12

kwamba juhudi stahiki za kukubaliana na taasisi zinazolipa mirabaha zinafanywa kwa kampuni zote, makusanyo na leseni kwa watumiaji wa kazi za wasanii yanafuata taratibu, haki na sheria na, gharama za uendeshaji CMOs haziathiri maslahi ya wanachama wake (wamiliki wa hakimiliki). Idara hii itahakikisha kwamba mgawanyo wa mirabaha ni wa haki kwa wasanii wote stahiki.

Idara itakuwa na afisa mmoja mwanasheria na maafisa wawili hadi watatu wa fani ya uhasibu. Maafisa wa kihasibu wanaweza kuongezwa kutoka wawili hadi watatu na zaidi baada ya kuwepo kwa angalau CMOs mbili.

d) Idara ya Fedha na Utawala (watu 6)

Idara hii itaongozwa na meneja mmoja. Chini ya meneja kutakuwa na wahasibu wasiozidi wawili, mtaalamu wa rasilimali watu mmoja na watunza kumbukumbu za kazi za hakimiliki wawili. Imependekezwa watunza kumbukumbu wa hakimiliki wawe chini ya idara hii kwa kuwa ndiyo itakayopokea fedha na hivyo itawajibika kupokea kazi za wabunifu na kuzitunza pia.

Meneja ataripoti kwa Msajili wa Hakimiliki. Atatoa taarifa katika kila kikao cha Bodi, pamoja na mambo ya fedha na rasilimali watu, kuhusu takwimu sahihi na kumbukumbu zilizohuishwa za hakimiliki katika daftari la kuorodhesha kazi zilizosajiliwa. Inapendekezwa kuanza na nafasi mbili ili mtu mmoja akiwa na udhuru mwingine aendelee kutoa huduma. Watunza kumbukumbu za hakimiliki wanapaswa kuwa wanasheria. Hawa ni watu ambao wanapaswa pia kuelewa kazi ngeni mfano hata za kutoka nje ya nchi au zilizolengwa kutumika kupitia mifumo mipya.

e) Miiko na Maadili ya Utendaji Kazi

Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania watatakiwa kuzingatia weledi wa hali ya juu. Hata hivyo, wafanyakazi wa idara ya usimamizi wa CMOs, wafanyakazi wa idara ya Usimamizi wa Sheria na Kuzuia Uharamia, Msajili wa Hakimiliki na Wakurugenzi wa Bodi wanapaswa kulinda haki katika maamuzi yote watakayofanya kuhusiana na hakimiliki. Ofisi ya Hakimiliki Tanzania iweke kanuni za maadili kulingana na ngazi ya maafisa husika katika maeneo tajwa katika aya hii.

f) Miundombinu

Ofisi ya Hakimiliki Tanzania haina jengo la ofisi za kudumu. Imepewa ofisi katika majengo ya Ofisi za Utumishi zilizopo Kivukoni, Dar es Salaam na Chumba kimoja kilichopo Dodoma kwenye ofisi za Wizara zilizopo jengo la PSSSF lakini bado ofisi hizo ni finyu haswa kwa majukumu mapya yaliyopendekezwa hapo juu yatakapoanza kutekelezwa.

7.0 MAKADIRIO YA MAKUSANYO YA SERIKALI

Makadirio ya makusanyo ya serikali yanatarajiwa kufanywa kwa kuhusisha vyanzo vitatu ambavyo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania, COSOTA, Mfuko wa Utamaduni na Malipo ya Mrabaha kama inavyofafanuliwa hapa chini:

a. Mamlaka ya mapato Tanzania

Endapo serikali ikikubali kupokea mapendekezo ya kamati hii ya kurekebisha vifaa vitakavyotozwa tozo ya Kifaa kitupu, inakadiriwa kuwa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania itakusanya Tsh. 681,837,257,900 kutoka kwenye tozo hii mpya kwa mwaka wa kwanza wa fedha huku mwaka wa pili wakiweza kukusanya Tsh. bilioni 712.5. Makadirio ya miaka kumi (10) ijayo ni Mamlaka ya mapato Tanzania itaweza kukusanya mapato kiasi cha trilioni Tsh. 9.838.

b. COSOTA

Kutokana na makadirio haya ya marekebisho ya tozo hii, COSOTA itaweza kupata Tsh bilioni 2.05 kwa mwaka wa kwanza wa fedha wa makusanyo haya, mwaka wa pili wataweza kupata bilioni Tsh. 2.14, mwaka wa tatu wataweza kupata Tsh. bilioni 2.24 huku katika kipindi cha miaka kumi (10) ijayo, jumla ya Tsh. bilioni 29.5 zitatolewa kwa COSOTA kwa matumizi yake ya ndani.

c. Mfuko wa utamaduni

Mfuko wa Utamaduni unatarajiwa kupata Tsh. bilioni 1.02 kwa mwaka wa kwanza wa makusanyo, Tsh. bilioni 1.07 kwa mwaka wa pili. Makadirio ya miaka kumi (10) ijayo ni Tsh. bilioni 15.616 zitatolewa kwa mfuko huu kama gawio kutoka kwenye tozo ya vifaa vitupu.

14

d. Malipo ya Mrabaha

Kwa kuzingatia vyanzo viwili vya mirabaha vilivyolengwa ambavyo ni mrabaha wa utendaji kazi (Performance royalties) na mrabaha utokanao na kutoza ushuru wa vifaa vitupu, inaonekana kuwa serikali itaweza kukusanya jumla ya Tsh. bilioni 15.59 kwa mwaka wa kwanza, Tsh. bilioni 19.14 kwa mwaka wa pili, Tsh. bilioni 23.59 kwa mwaka wa tatu na jumla ya bilioni Tsh.419.67 kwa kipindi cha miaka kumi (10) ijayo.

Aidha, kwa kuzingatia mapendekezo ya sasa ya utengano kati ya CMO’s yaani Muundo Jumuishi wa Usimamizi Menejimenti na taasisi ya kusimamia Hakimiliki, inatazamiwa kuwa vyama hivi vya usimamizi na ukusanyaji wa mirabaha, vitaweza kukusanya takribani Tsh. Trilioni 3.76 kwa miaka 10 ijayo huku ulinganishi wa takwimu za kihistoria za miaka 17 iliyopita (2004 mpaka 2021), inaonesha COSOTA imeweza kufanya makusanyo ya Tsh. 3,114,778,220.

8.0 Shukrani

Awali ya yote tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukamilisha kazi hii muhimu kwa maslahi mapana ya taifa na watu wake. Aidha, kwa namna ya kipekee tunakushukuru Mheshimiwa Waziri kwa imani uliyoionesha kwetu na kututetua kufanya kazi hii muhimu. Umeonesha imani kubwa kwetu nasi tumejitahidi kufanya kazi kwa kuzingatia hadidu za rejea tulizopewa.

Kukamilika kwa kazi hii kumetokana na ushirikiano wa dhati uliooneshwa kutoka katika makundi mbalimbali. Tunawashukuru wadau wote walioshirikiana nasi katika hatua mbalimbali za ukusanyaji wa taarifa zilizofanikisha kuandikwa kwa ripoti hii. Tunatambua kuna wadau waliojaza hojaji, waliosaidia kupatikana kwa nyaraka mbalimbali na wale walioshiriki katika mikutano iliyohusisha kanda sita kama zilivyotajwa hapo juu. Kipekee kabisa tunatoa shukrani za dhati kwa Mhe. Pauline Gekul (Mb.) Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye licha ya majukumu mengi ya kitaifa aliyonayo, aliweza kutenga muda wake na kushiriki nasi katika mkutano wa wadau wa kanda ya Kaskazini. Mkutano huu ulifanyika Mkoani Arusha katika Hoteli ya Golden Rose, na kuhudhuriwa na takriban washiriki 216.

Mwisho


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...