Na Mwandishi wetu, Rombo

MKURUGENZI Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA)  Mhandisi  Clement Kivegalo, amemuagiza Mkandarasi Kampuni ya  Best One Ltd, inayotekeleza miradi miwili ya wilaya ya Rombo itakayogharimu jumla ya  Sh. 5.3  bilioni kuikamilisha kwa wakati ili shida ya maji Rombo imalizike.

Akizungumza baada ya kukagua utekelezaji wa miradi hiyo, Mhandisi Kivegalo amesema Miradi hiyo, ambayo inatekelezwa kwa pamoja baina RUWASA na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Rombo ni lazima ikamilike kwa wakati ili wananchi wa Rombo wapate huduma muhimu ya maji.

"Nimekuja Rombo na wataalam wangu kuona utekelezaji wa miradi ya maji ndani ya Wilaya ya Rombo kufuatia wito uliotolewa na Mbunge wa Rombo baada ya kuona utekelezaji unasuasua. Aidha, nimetembelea pia Mradi wa Njiro II unaotekelezwa kwa fedha za UVIKO-19 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. Nimefarijika kuona kuwa Mradi wa UVIKO-19 umekamilika kwa kiasi kikubwa na tayari baadhi ya vijiji vimeanza kupata maji, hivyo tunataka kasi iongezeke" amesema.

Amesema kuna changamoto kidogo katika utekelezaji wa miradi miwili mojawapo ikiwa ni ucheleweshaji wa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani hivyo, amekutana na wataalam wake na Mkandarasi kujadiliana nao.

"Moja kati ya miradi hii, ambao ulilalamikiwa kuchelewa ulikuwa chini ya Mamlaka ya Maji Rombo na sasa RUWASA tutashirikiana nao  kuona unakamilika, kama ambavyo wameomba," amesema 

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo wa RUWASA amesema changamoto katika miradi hiyo zitapatiwa ufumbuzi na amemtaka Mkandarasi kuharakisha utekelezaji wa miradi ili wananchi wa Rombo wapate maji.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji  Rombo, Martin Kinabo ameaema kwa sasa miradi ambayo inatekelezwa katika wilaya hiyo ni miwili mradi wa Njoro II, ambao utagusa vijiji 15 utasaidia wananchi 24,454 ambao utagharimu Sh. 3.4 bilioni.

Amesema mradi mwingine ni mradi wa Ona ambao utahusisha vijiji 29 na utagharimu Sh. 2.9 bilioni na miradi yote inaendelea vizuri.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Best one Ltd, Juma Mvamba  ameahidi kukamilisha miradi hiyo kwa wakati endapo atawezeshwa malipo ya awali na mahitaji mengine kama msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani.

"Tunaendelea kutekeleza mradi mmoja, mwingine tayari umekamilika na wananchi wanapata maji na RUWASA wameahidi kutusaidia kukamilisha mradi kwa wakati" amesema.

Hivi karibuni Mbunge wa jimbo la Rombo, Profesa Adolf Mkenda akiwa katika ziara kwenye jimbo lake, alilalamika kuchelewa kukamilika mradi mmoja na kutaka RUWASA makao makuu kuingilia kati ili wananchi wa Rombo wapate maji. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...