Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma Agosti 15, kuhusu tathmini ya mwenendo wa bei ya bidhaa bidhaa muhimu nchini na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali kupunguza mfumuko wa bei.
Baadhi ya wanahabari wakiwa katika mkutano huo.





Baadhi ya maafisa wa serikali na wanahabari wakifuatilia kichozungumzwa na waziri katika mkutano huo.PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA


Mdau, nakuomba uendelee kusoma taarifa kamili hapo chini iliyotolewa na Waziri Dkt Kijaji...



TAARIFA KWA UMMA


_________________________________________________



TATHMINI YA MWENENDO WA BEI YA BIDHAA MUHIMU NCHINI



15/08/2021, DODOMA



1. UTANGULIZI



Ndugu Waandishi wa Habari;

Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inashirikiana na Tume ya Ushindani (FCC) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kutekeleza jukumu la kufuatilia na kufanya tathmini ya mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini. Lengo la tathmini hiyo ni kumlinda mlaji kwa kuhakikisha anapata bidhaa bora kwa bei stahiki na kuzuia upandishwaji holela wa bei za bidhaa mbalimbali; pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote atakayebainika kupandisha bei za bidhaa kiholela bila kuzingatia gharama halisi za uzalishaji au uingizaji nchini wa bidhaa husika.

Matokeo ya tathmini zilizofanyika hivi karibuni yalionesha kuwa kuna uhimilivu mkubwa wa bei (price stability) kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini, ambazo zilionesha ongezeko dogo la bei ikilinganishwa na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi ambazo zilionesha ongezeko kubwa zaidi la bei.


Ndugu Waandishi wa Habari;

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya jitihada kubwa za kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji biashara nchini, kwa kuchukua hatua mbalimbali katika kudhibiti ongezeko la bei za bidhaa ikiwa ni pamoja na udhibiti wa upandishwaji holela wa bei. Kutokana na jitihada hizo, bei za bidhaa kwenye soko la ndani zimeendelea kuwa na utulivu huku bei za baadhi ya bidhaa hususan zinazotegemea malighafi kutoka nje ya nchi zikiongezeka kutokana na kupanda kwa bei za malighafi katika soko la dunia na gharama kubwa za usafirishaji. Hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuimarisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa mbalimbali ili kupunguza utegemezi wa kuagiza mahitaji muhimu kama vile vyakula kutoka nje ya nchi. Aidha, bei za baadhi ya bidhaa zimepanda kutokana na kupanda kwa bei ya nishati hasa mafuta ya petroli kwenye soko la dunia.


Ndugu Waandishi wa Habari;

Serikali inaendelea kuchukua hatua mbali mbali kwa lengo la kuwapunguzia Wananchi athari zitokanazo na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu. Hatua hizo ni pamoja na kuwapunguzia gharama za uzalishaji au uagizaji na usambazaji wa bidhaa ili kuleta uhimilivu wa bei (price stability) kwenye soko. Hatua zilizochukuliwa na Serikali zimelenga kupunguza athari za mtikisiko wa uchumi duniani uliosababishwa na janga la UVIKO-19 na vita kati ya nchi za Urusi na Ukraine.

Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2022/2023 na Sheria ya Fedha ya mwaka 2022 ni pamoja na hizi zifuatazo:

i) Serikali imeondoa (zero rate) Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wazalishaji wa ndani wa mafuta ya kupikia yaliyosafishwa (double refined edible oil) kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa hiyo nchini na hivyo kuleta unafuu wa bei za mafuta ya kupikia kwa mlaji wa mwisho. Hatua hii imeanza kuonesha mafanikio kwani mwenendo wa bei ya mafuta ya kupikia unaonesha bei hizo zimeanza kushuka. Serikali pia inaendelea na jitihada za kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za mafuta ya kupikia nchini hasa alizeti na chikichi kwa lengo la kujitosheleza kwa mahitaji yetu na kuuza ziada nchi jirani.

ii) Serikali imeondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wazalishaji wa mbolea kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kuwapunguzia wakulima gharama za uzalishaji na hivyo kuleta unafuu wa bei za mazao muhimu ya chakula.

iii) Sheria ya Fedha ya mwaka 2022 pia imempa Waziri wa Fedha mamlaka ya kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa Wawekezaji Mahiri hususan watakao wekeza kwenye ujenzi wa viwanda kwa ajili ya kupunguza utegemezi wa nchi wa kuagiza bidhaa muhimu kutoka nje. Hatua hii ni ya kuweka uwiano kati ya Sheria ya VAT na Sheria ya Uwekezaji ili kuweka mazingira yanayotabirika kwa Wawekezaji, kuvutia uwekezaji, kuongeza uzalishaji wa ndani na hivyo kuleta uhimilivu wa bei.

iv) Serikali imeanza kutoza ushuru wa asilimia 30 au Dola za Marekani 150 kwa Tani kwenye usafirishaji wa bidhaa za shaba na chuma chakavu nje ya nchi kwa lengo la kuwalinda wazalishaji wa ndani wa bidhaa za chuma, kwa kuwahakikishia upatikanaji wa malighafi za kutosha na hivyo kuleta unafuu wa bei za bidhaa za chuma hasa nondo kwenye soko la ndani.

v) Serikali imepunguza ushuru kwa malori yanayosafirisha bidhaa (transit charges) kutoka Dola za Marekani 16 kwa kila kilomita 100 hadi Dola za Marekani 10 kwa kila kilomita 100 ili kupunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa nchini na hivyo kuleta unafuu wa bei za bidhaa hizo.

vi) Serikali imepunguza kiwango cha ushuru wa forodha kutoka asilimia 35 hadi asilimia 10 kwa waagizaji wa ngano ili kuwapunguzia gharama wazalishaji wa ndani wa unga wa ngano na hivyo kuleta unafuu wa bei ya unga wa ngano kwenye soko la ndani.

vii) Serikali pia imeondoa ushuru wa forodha kwa kutoza kiwango cha asilimia sifuri (0%) badala ya asilimia 10 kwenye malighafi za utengenezaji wa sabuni (RBD Palm Stearin) kwa lengo la kuhamasisha na kupunguza gharama za wazalishaji wa ndani wa sabuni ili kudhibiti ongezeko la bei ya sabuni.

viii) Serikali imeongeza kiwango cha juu cha ushuru wa forodha kwa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na viwanda vya ndani kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 ili kuwalinda wazalishaji wa ndani na kuongeza biashara miongoni mwa nchi za EAC. Hatua hiyo itawanufaisha wasindikaji wa ndani wa bidhaa za samaki, nyama, maziwa na mazao ya kilimo ikiwa ni pamoja na kahawa, chai, mboga na matunda, mafuta ya kupikia, saruji, chumvi, sabuni, vifungashio, bidhaa za ngozi na samani za mbao kwa lengo la kuleta unafuu wa bei za bidhaa hizo.


2. MWENENDO WA BEI ZA BIDHAA



i) MAFUTA YA KUPIKIA

Serikali inatekeleza Mkakati wa kuongeza uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wakulima kutumia mbegu bora za alizeti na chikichi (mawese) ili kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kupikia yatokanayo na mazao hayo. Ongezeko la bei ya mafuta duniani lina athari hasi kwetu Watanzania, kwani mahitaji ya mafuta ndani ya Taifa letu kwa mwaka ni tani 650,000 (MT) huku uwezo wetu wa kuzalisha mafuta ni tani 270,000 (MT), ambayo ni sawa na asilimia 41.5 tu ya mahitaji yetu kwa mwaka. Hivyo ongezeko lolote la bei ya mafuta ya kula kwenye soko la Dunia lina athari hasi za moja kwa moja kwenye bei ya bidhaa hiyo kwenye soko letu la ndani.

Wastani wa bei ya mafuta kwa mwezi Julai, 2022 ilikuwa Shilingi 5,000 kwa mafuta yaliyosafishwa mara moja na Shilingi 9,000 kwa mafuta yaliyosafishwa mara mbili (double-refined). Kwa mwezi Agosti, 2022 bei zimeshuka kidogo ambapo mafuta hayo yanauzwa kwa wastani wa bei ya Shilingi 4,500 na Shilingi 8,000 kwa mafuta yaliyosafishwa mara mbili (double-refined).

ii) SABUNI

Bei za sabuni za kufulia za mche zimeongezeka katika kipindi cha mwezi Agosti kutokana na kuongezeka kwa bei ya malighafi za kutengeneze sabuni zinazoagizwa kutoka nchi za Indonesia na Malaysia. Bei zimepanda kutoka wastani wa Dola za Marekani 500 hadi 600 kwa tani hadi Dola za Marekani 1,800 kwa tani, hasa baada ya nchi ya Indonesia kuweka zuio la kusafirisha nje malighafi hizo. Kutokana na ongezeko hilo la bei ya malighafi bei kwa mche ni kati ya Shilingi 3,000 na 4,500.

Vilevile, sabuni ya kufulia ya unga inauzwa kwa shilingi 1000 hadi 4500/- kwa kilo moja (Doffi, Niceone, Killsoft) wakati Omo ikipatikana kwa Shilingi 8000 hadi 8200/- kwa kilo moja.


iii) NGANO

Serikali inatekeleza Mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao la ngano nchini ili kukabiliana na upungufu wa tani 800,000 tunazoagiza kila mwaka huku kiasi kikubwa kikitoka katika nchi za Urusi na Ukraine. Mahitaji ya ngano nchini ni tani 1,000,000 kwa mwaka huku uzalishaji wa ndani ukiwa chini ya tani 200,000 kwa mwaka. Kwa mwezi Julai, bei ya kilo moja ya ngano hapa nchini ni wastani wa Shilingi 2,000 na kwa mikoa ya pembezoni hadi Shilingi 4,000 kwa kilo moja. Aidha, bei hii haikubadilika kwa mwezi Agosti.



iv) VIFAA VYA UJENZI


a) Saruji


Kwa sasa nchi yetu ina jumla ya Viwanda 17 vya Saruji vyenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya saruji hapa nchini. Wastani wa bei ya saruji kwa mwezi Julai ilikuwa kati ya Shilingi 14,500 na 16,500 kwa mfuko wa Kilo 50 wa Saruji ya 32.5R na Shilingi.17,200 hadi 23,000 kwa saruji ya 42.5N. Wastani wa bei ya saruji kwa mwezi Agosti ni Shilingi 14,500 kwa Saruji ya 32.5R na Shilingi. 17,000 kwa saruji ya 42.5N

b) Nondo


Nchi yetu ina jumla ya Viwanda kumi na sita (16) vyenye uwezo wa kuzalisha tani 1,082,788 za nondo kwa ukubwa wa 16mm, 12mm, 10mm na 8mm. Hata hivyo, kwa sasa uzalishaji wa nondo ni tani 750,000.

Wastani wa bei ya nondo za 16mm ni kati ya Shilingi 45,000 na 52,000 kwa mwezi Julai; na Shilingi 41,000 hadi 55,000 kwa mwezi Agosti kutokana na umbali kutoka viwandani na ongezeko la gharama ya usafirishaji na bei ya dizeli. Wastani wa bei ya nondo za 12mm ni kati ya Shilingi 24,500 na 30,000 kwa mwezi Julai na Shilingi 24,000 hadi 30,000 kwa mwezi Agosti, 2022.

Wastani wa bei ya nondo za 10mm ilikuwa kati ya Shilingi 19,000 na 23,000 kwa mwezi Julai na Shilingi 18,000 hadi 23,000 kwa mwezi Agosti; 2022. Wastani wa bei ya nondo za 8mm ilikuwa Shilingi 14,500 hadi 19,500 kwa mwezi Julai na Shilingi 10,000 hadi 18,000 kwa mwezi Agosti, 2022.

c) Bati

Mwezi Julai, 2022 bati za gauge 28 iliuzwa kwa wastani wa Shilingi 30,000 hadi 45,000 na mwezi Agosti inauzwa kati ya Shilingi 30,000 hadi 45,000. Wastani wa bei ya bati za gauge 30 kwa mwezi Julai ziliuzwa kati ya Shilingi 22,000 hadi 28,500 na mwezi Agosti zinauzwa kati ya Shilingi 22,000 hadi 28,000. Wastani wa bei kwa bati za gauge 32 kwa mwezi Julai ilikuwa kati ya Shilingi 19,000 na 26,000 na mwezi Agosti ni kati ya Shilingi 18,500 na 26,000.


v) SUKARI


Mahitaji ya Sukari nchini kwa mwaka 2021/22 ni wastani wa tani 655,000 ambapo kati ya hizo, tani 490, 000 ni kwa matumizi ya kawaida na tani 165,000 ni kwa matumizi ya viwandani. Uzalishaji wa sukari kwa viwanda vya ndani unakadiriwa kuwa kiasi cha tani 394,606 ambayo ni sawa na asilimia 80.5 ya mahitaji ya sukari nchini kwa matumizi ya kawaida. Aidha, nchi yetu ina jumla ya

viwanda 5 vya kuzalisha sukari. Kila mwaka tunalazimika kuagiza sukari kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuziba pengo la uzalishaji (Sugar gap)..

Katika kipindi cha mwezi Julai na Agosti 2022, bei ya rejareja kwenye maeneo mengi nchini ni kati ya Shilingi 2,400 na 3,000 kwa kilo. Maeneo machache hasa ya pembezoni ni shilingi 3,000 kwa kilo kutokana na ongezeko la gharama za usafirishaji.

vi) BIDHAA ZA VYAKULA


a) Maharage

Maharage katika masoko yetu yanapatikana kwa wastani wa bei ya Shilingi 1,800 hadi 2,600 kwa kilo. Bei hiyo ni ongezeko la kutoka Shilingi 1,650 hadi 2,600 kwa kilo mwezi Julai, 2022.

b) Mchele

Wastani wa bei ya mchele kwa kilo ni kati ya Shilingi 1,700 na 3,000 katika maeneo mbalimbali nchini kwa mwezi Agosti. Bei hii ni ongezeko la asilimia saba kutoka wastani wa Shilingi 1,600 hadi 2,800 kwa kilo mwezi Julai, 2022.


c) Mahindi na Unga wa Mahindi

Bei ya zao la mahindi kwa kilo moja haikuonesha mabadiliko yoyote kati ya mwezi Julai na Agosti, 2022, ambapo zao hilo linauzwa kwa Shilingi 700 hadi 1,500 kwa kilo. Unga wa Mahindi unapatikana kwa Shilingi 1,400 hadi 1,700 kwa kilo mwezi Agosti, kutoka bei ya mwezi Julai ya Shilingi 1,100 hadi 1,700.


d) Ulezi


Wastani wa bei ya ulezi ni Shilingi 1,200 hadi 3,000 kwa kilo kwa mwezi Agosti na hakuna mabadiliko ya bei kutoka mwezi Julai, 2022.

e) Uwele


Wastani wa bei ya uwele ni Shilingi 1,200 hadi 3,000 kwa kilo mwezi Agosti 2022; na hakuna mabadiliko ya bei za mwezi Julai, 2022..


g) Viazi Mviringo

Wastani wa bei ya viazi mviringo ilikuwa Shilingi 800 hadi 1,500 kwa kilo mwezi Julai, 2022; na Shilingi 900 hadi 1,400 kwa mwezi Agosti, 2022..


Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inaendelea kuchukua hatua za kumlinda mlaji dhidi ya upandishaji holela wa bei ikiwa ni pamoja na kukutana na wadau wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa mbalimbali. Vikao vya wadau kwa ajili ya udhibiti wa bei za bidhaa vilivyoandaliwa na Wizara na kuhudhuriwa na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI); ni pamoja na kikao na wazalishaji wa Saruji tarehe 31 Januari, 2022 Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa NDC; wazalishaji wa Nondo tarehe 1 Februari, 2022; na wasambazaji (distributors) wa vifaa vya ujenzi kilichofanyika tarehe 3 Februari, 2022 Jijini Dododma.


3. FURSA ZA MASOKO YA BIDHAA ZINAZOZALISHWA NCHINI



Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kutafuta masoko ndani na nje ya nchi kwa ajili ya mazao na bidhaa zinazozalishwa nchini. Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inaunga mkono jitihada za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan za kuifungua nchi, kuvutia uwekezaji na utalii kwa kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini. Matokeo ya jitihada hizo yameanza kuonekana ambapo kwa mwezi Agosti, 2022, fursa mbalimbali zimepatikana katika masoko ya Kimataifa kwa mazao yanayozalishwa nchini kama inavyoonekana kwenye Jedwali hapa chini:


Na.

Bidhaa

Kiasi Kinachohitajika (Tani)

Wanunuzi Walipo

1

Mtama Mweupe

205

Kenya


2

Mashudu ya Soya

200

Uganda


3

Maharage ya Njano

1,000

Kenya


4

Fiwi

1,000

Kenya


5

Maharage ya Soya

1,660

Kenya


6

Kunde

30,000

Uganda


7

Ulezi

3,000

Kenya


8

Mahindi

1,000

Kenya



Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) itawaunganisha wazalishaji wa mazao hayo na wanunuzi kupitia barua pepe: enquiries@tantrade.go.tz /info@tantrade.go.tz Aidha, taratibu za kusafirisha bidhaa hizo nje ya nchi zimeainishwa kwenye tovuti ya trade@tanzania.go.tz.


Ndugu Waandishi wa Habari,



Napenda kuhitimisha taarifa yangu, kwa kuuhakikishia umma wa Watanzania kwamba Serikali itaendelea kufuatilia, kufanya tathmini na kusimamia ushindani wa haki katika soko, kwani ni wajibu wa Serikali kumlinda mlaji.



Dkt. Ashatu K. Kijaji (Mb.)

WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA

15 AGOSTI, 2022

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...