Mwezeshaji kutoka Bodi ya wataalam wa Ugavi na Ununuzi (PSPTB) Jakson Musiba akitoa mafunzo ya jinsi ya kusimamia mikataba ya Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa wasimamizi wa mikataba wa Taasisi hiyo leo katika
Ukumbi wa JKCI uliopo Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ugavi na Ununuzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Idd Lema akiwaelekeza wasimamizi wa mikataba namna ya
kutekeleza majukumu yao wakati wa mafunzo ya jinsi ya kusimamia mikataba ya
JKCI yaliyofanyika leo katika Ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo Jijini Dar es Salaam.
Wasimamizi wa mikataba ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wakifuatilia mafunzo yaliyokua yakiendelea ya namna ya kusimamia mikataba ya
Taasisi hiyo leo katika Ukumbi wa JKCI uliopo Jijini Dar es Salaam
Picha na: Khamis Mussa.


 

Na: Genofeva Matemu

WASIMAMIZI wa mikataba ya Ununuzi ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamepatiwa mafunzo ya jinsi ya kusimamia mikataba ya Ununuzi ya Taasisi hiyo kwa mujibu wa vigezo, viwango vya ubora (technical specifications) na matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 kama ilivyorekebishwa mwaka 2016.

Akizungumza na wasimamizi wa mikataba ya JKCI, mwezeshaji wa mafunzo kutoka Bodi ya Wataalamu wa Ugavi na Ununuzi (PSPTB) Jackson Musiba alisema kuwa shughuli za manunuzi sio kwa Maafisa wa Kitengo cha Menejimenti ya Ununuzi (PMU) peke yake bali zinamhusisha kila aliyehusika katika mchakato wa ununuzi.

Mafunzo hayo ya siku moja kwa wasimamizi wa mikataba ya Ununuzi ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete yalifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo Jijini Dar es Salaam na kubainika kuwa na changamoto kubwa katika uandaaji wa viwango vya ubora (technical specifications).  

“Mtumiaji wa vifaa (Idara Tumizi) zina jukumu la kusimamia mikataba ya Ununuzi na kutunza taarifa zote zinazohusu mikataba lakini pia mnahitaji mafunzo maalum ya uandaaji wa viwango vya ubora (technical specifications) kwani hapa kuna changamoto kubwa ya uandaaji wa viwango vya ubora”,

“Jukumu la Ununuzi wa mahitaji ya Ununuzi Serikalini ni la Maafisa Ugavi na Ununuzi, kisheria jukumu hilo si la kila mtu hivyo pale Afisa anapotaka kufanya manunuzi ni lazima awashirikishe watumishi wa Kitengo cha Menejimenti ya Ununuzi (PMU) tofauti na hivyo mtumishi huyo atakuwa amevunja Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 kama ilivyorekebishwa mwaka 2016”, alisema Musiba.

Musiba alisema kuwa fedha nyingi za Serikali hutumika katika manunuzi ambapo Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 kama ilivyorekebishwa mwaka 2016 imebainisha adhabu atakayopewa mtumishi atakayetumia vibaya fedha ya serikali hivyo kuwataka watumishi wa JKCI wanapohusishwa katika michakato ya manunuzi ya mali za umma kuwa waangalifu.

“Watumishi tunapaswa kuwashirikisha Maafisa Ugavi na Ununuzi katika hatua zote za kuandaa mipango ya ununuzi ya Idara na Vitengo vyao, kuna kasumba ambayo ipo katika taasisi nyingi ambapo Idara moja ama zaidi wanafanya mipango ya manunuzi bila kuwahusisha watumishi wa Kitengo cha Menejimenti ya Ununuzi (PMU) halafu mwisho wa siku wanatoa lawama kwa watumishi wa PMU kwa kuchelewesha huduma wakati kama wangeshirikishwa tokea mwanzo taratibu za ununuzi zingefanyika mapema”, alisema Musiba.

Aidha, Musiba alisema kuwa uandaaji wa viwango vya ubora (technical specifications) ya vifaa ni moja ya changamoto kubwa inayokabili masuala ya ununuzi na lawama nyingi hupelekwa kwa watumishi wa PMU wakati kiuhalisia changamoto hiyo husababishwa na Idara Timizi (User Department) ambaye aliomba vifaa kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake ya kazi.

“Unapoandaa mahitaji yako lazima ujue unataka nini, kinapatikana kwa msambazaji yupi ambaye ana bidhaa bora kuliko wengine na gharama zake ni zipi, ukiyaainisha vizuri mahitaji yako itakua rahisi kuwaondoa wasambazaji wengine ambao bidhaa zao hadhikidhi mahitaji yako na kubakia na msambazaji ambaye anakidhi mahitaji yako”, alisema Musiba

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ugavi na Ununuzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Idd Lemmah alisema kuwa mafunzo hayo kwa wasimamizi wa mikataba ya Ununuzi yatasaidia kuboresha utendaji wa kazi hususani suala zima la usimamizi wa mikataba ya ununuzi ya Taasisi hiyo.

“Mafunzo kama haya yataendelea kutolewa mara kwa mara kwa wasimamizi wa mikataba ya Ununuzi ya JKCI ili kuondoa changamoto zote zinazotukabili katika manunuzi ya mali za Taasisi”,

“Michango iliyotolewa na wasimamizi wa mikataba ya JKCI wakati wa mafunzo inaonyesha ni jinsi gani somo limeeleweka, lakini katika mafunzo haya tumebaini ipo changamoto ya uandaaji wa viwango vya ubora (technical specifications) wakati wa ununuzi, changamoto hiyo tumeichukua na kuahidi kuifanyia kazi”, alisema Lemmah.

Naye Fundi Sanifu vifaa tiba (Biomedical Engineer) wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Veronica Mugendi alisema kuwa mafunzo ya jinsi ya kusimamia mikataba ambayo ipo JKCI yamempa uelewa mkubwa na kumuainishia wajibu na majukumu yake katika kusimamia mikataba.

“Mafunzo haya yataleta mabadiliko makubwa kwetu sisi wasimamizi wa mikataba kwa sababu awali hata uandishi wangu wa ripoti haukuwa katika mfumo ambao ni sahihi hivyo sasa nitabadilika kwani leo nimeweza kujua napaswa kufanya nini na mipaka yangu ya kazi ni ipi”,

“Wito wangu kwa Taasisi ni kuhakikisha kuwa mafunzo haya yanatolewa walau mara mbili kila mwaka kwasababu kila mwaka wasimamizi wa mikataba wanabadilika ili hata wale ambao hawakupata nafasi ya kuhudhuria leo wapate nafasi hiyo na wale watakaopewa jukumu hili mwakani waweze kuwa na elimu hii tuliyoipata”, alisema Veronica.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...